Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege la AVIC

 Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic kutoka Jamuhuri ya Watu wa  China Bwana Duan Bao Rong akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic  Afisini kwake Vuga.

 Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic Bwana Duan Bao Rong akimueleza Balozi Seif azma ya Shirika lake kutaka kuwekeza mradi wa Shirika la Ndege la Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mwakilishi wa Shirika hilo Nchini Tanzania  Bibi Carol Meng.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic kutoka Jamuhuri ya Watu wa  China limejitolea  kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha  mradi wa Kiuchumi wa pamoja wa Shirika la Ndege la Zanzibar.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo lenye Makao Makuu yake Mjini Beijing China Bwana Duan Bao Rong alieleza hayo wakati alipokuwa  akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Duan Bao Rong  alisema  Uongozi wa Shirika hilo hivi sasa uko katika hatua za awali za kuwasiliana na Viongozi Waandamizi wa Taasisi zinazohusika na Sekta ya Mawasiliano na Uwekezaji kwa nia ya kuandaa taratibu zinatakazofanikisha  kuanzishwa kwa Shirika hilo katika mfumo wa Ubia na Serikali.

Alisema Wataalamu wa Shirika hilo kwa kushirikiana na wale wa Zanzibar  wataendelea kufanya utafiti wa pamoja katika kuona namna gani mradi huo mkubwa unatekelezwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Taifa ambapo pia  alieleza kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China itakuwa tayari kuunga mkono uanzishwaji wa mradi huo.


Alifahamisha kwamba wakati mafunzo ya kiufundi yakiendelea kutolewa kwa Wahandisi Wazalendo  ili kuwaweka tayari wakati utakapoanza mradi huo Mipango itaandaliwa pia katika kuanzisha Kara kana  itakayotoa huduma za Matengenezo ya Ndege zitakazopata hitilafu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Naibu Mkurugenzi huyo wa Shirika la Avic Bwana Duan Bao Rong  alifafanua kwamba Shirika hilo tayari limeshatengeneza Ndege Mpya kadhaa tokea kuanzishwa kwake  karibu Miaka Kumi iliyopita na hivi sasa zaidi ya Ndege 56 kati ya hizo zimeuzwa na shirika hilo katika Mataifa ya Zimbabwe, Zambia, Congo Brazaville,Kenya na Tanzania.

“ Lengo letu tulilopanga katika kuzingatia uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni kuongeza mapato makubwa kwa Zanzibar na pia ifikie hatua ya kujitegemea yenyewe katika kutoa huduma za usafiri wa Anga ”. Alisema Bwana Duan Bao Rong.

Aliipongeza  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inayoendelea kuchukuwa katika kutoa ushirikiano wa karibu kwa Uongozi wa Shirika  hilo la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic.

Akitoa shukrani zake kwa uamuzi uliyochukuwa na Shirika hilo la Ndege la Avic Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kufanikiwa kwa mradi huo muhimu wa mawasiliano kutatoa fursa pana kwa Wananchi wa Ukanda wa Afrika Mashariki kupata huduma za uhakika za usafiri wa Anga.

Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi huo wa Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege  la avic kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wote kuupa ushirikiano unaohitajika ili kuona azma hiyo mpya inafanikiwa kwa kiwango kinachokusudiwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.