Na Mwandishi Wetu Pemba.
MGOMBEA
nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameahidi ndani ya miaka miwili kukamilisha mpango mkubwa wa kuimarisha sekta ya
uvuvi utakaojumuisha kuwapatia wavuvi boti maalum za kufanyia shughuli za uvuvi.
Amesema mpango huo
ambao matayarisho yake tayari yameanza utashirikisha sekta binafsi ambapo
tayari makubaliano ya awali yamefanyika ambapo katika hatua ya awali boti 20
kumi zikiwa za mita 6 na nyingine 10 za mita 9 watapewa wavuvi kwa majaribio.
Akizugumza katika
mkutano wa kampeni uliofanyika katika kiwanja cha Shamemata huko Micheweni,
Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk. Shein alieleza kuwa endapo wavuvi watazikubali
boti hizo baada ya majaribio boti nyingine zaidi zitatengenezwa na kupewa
wavuvi.
Dk. Shein alifafanua
kuwa baada hatua hiyo kukamilika itafuata hatua nyingine ya ujenzi wa boti za
ukubwa wa zaidi ya mita 18 kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu hivyo kutoa fursa
kwa wavuvi wa Zanzibar kuvuna rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
“Tunaamini kuwa
tunaweza kuwawezesha kuvua samaki eneo la bahari kuu ndani ya miaka mitano kwa
kushirikiana na kampuni moja kubwa ya kutengeneza boti na meli za uvuvi ya Sri
Lanka” Dk. Shein aliwaambia wananchi hao waliokuwa wakimshangilia.
Katika mkutano huo
Dk. Shein ambaye anagombea nafasi hiyo kwa mara ya pili baada ya kumalizika
kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano amewataka wananchi kumchagua tena ili
kupata fursa ya kuendeleza mipango ya kujenga Zanzibar.
Mgombea huyo
aliwahakikishia wakulima wa mwani ambao wengi wao ni kinamama kuwa serikali
imejidhatiti kuhakikisha kuwa kilimo cha mwani aina ya ‘cottonii’ wenye thamani
zaidi ambao majaribio yake yalifanyika katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya
Micheweni kinaimarishwa.
Aidha aliahidi katika
kipindi kijacho wizara tatu (za Kilimo, Biashara na Uvuvi) zitashirikiana
kuhakikisha kuwa mwani wa aina ya spinosum unapatiwa soko la uhakika na kwa bei
muafaka ili wakulima waweze kufaidi jasho lao.
Kwa upande mwingine
Dk. Shein amesema serikali atakayoiunda akichaguliwa tena itawapatia ndani ya
miaka mitano kinamama wakulima wa mwani vihori 500 vya kubebea mwani baada ya serikali
kuwapatia vihori 100 mwanzoni mwa mwaka huu.
Kuhusu ahadi zake
alizozitoa wakati alipokuwa katika mkutano wake wa kampeni mwezi Oktoba mwaka
2010, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ahadi hizo amezitekeleza na
nyingine zimo katika maandalizi ya utekelezaji.
“Nimekamilisha ahadi
zangu kwenu kuhusu barabara, maji na afya na kuhusu hili la uendelezaji wa eneo
huru la kiuchumi la Micheweni limeshafanyiwa usanifu tayari kwa utekelezaji”
Dk. Shein alibainisha.
Alifafanua kuwa hatua
zimechukuliwa kuimarisha hospitali ya Micheweni ambapo maabara ya kisasa
imejengwa yenye uwezo wa kuchunguza maradhi mengi,jengo la upasuaji na wodi
mbalimbali za wagonjwa zimejengwa.
Alisema kilichobaki
ni kuongeza baadhi ya majengo, baadhi ya vifaa pamoja na madaktari bingwa wa
upasuaji, watoto na kinamama ili hospitali iweze kufikia kuwa hospitali ya
wilaya.
Aliahidi kuimarisha vituo
vya afya vya Kiuyu Mbuyuni na Maziwang’ombe kwa kuvipatia wahudumu zaidi wa
afya na kuongeza vifaa.
Aliahidi katika
kipindi kijacho ataongeza kasi ya usambazaji na uimarishaji wa wa huduma za
jamii kama maji katika wilaya hiyo ambapo vijiji vya vya Kwansa, Bondeni,
Mvuleni, Mkunguwachini, Kijogoo, Kijangwani, Chaleni na Sipwese vitapatiwa
maji.
Kwa upande wa umeme
vijiji vya Kijangwani, Sipwese na Mtukwao vitapatiwa huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment