Habari za Punde

‘MEO’ kikundi kinachotarajia kufaidika na upandaji miti


Kupata sh/=35.5 milion, ilisaidiwa shilingi 9 milion na TASAF

 Na Haji Nassor, Pemba
‘’TULILICHAGUA eneo hili, maana likukua kama kichwa cha mtu alieokosa nywele, lilikuwa jeupe kama uwanja wa mpira tu, leo unaona kiza kimetanda’’,.

Niliguna huu..!!!!.. na kushangaa kweli, hapa palikuwa na uwanja, kutokana na nini…. nikamuuliza aliekuwa karibu yangu, kisha kajibu mbio, ndio palikatwa miti.

‘’Aaaa !!!! acha tu wewe huwezi kuamini, kwamba miti hii iliopo tuliipanda hata kabla ya kupata mradi huu kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF, leo pazuri’’,alisema Mwenyekiti wa kikundi hicho Khamis Ali Juma.

Wakati tukiutembelea mradi huo, huku tukipigwa na vitawi vya Mivinjem Misaji, Mikungu na Mitondoo, ule upepo wa asili unaotokana na miti, ndipo hasa unapojitokeza kwa mbali.

Hatukujali jua lililokuwa kiliwaka wakati huo, maana hapo ni mithili ya ofisi ya kiongozi, iliopambwa kwa viyoyozi zisivyokatiwa umeme daima, na huwezi kutamani kuondoka.

Kumbe miti ndio asili ya upep bora, tena usiolipiwa kodi, na wala usio na madhara, ni mazungumzo ya chini chini yaliokuwa yakisikika kutoka kwa baadhi ya watu tuliokua katika msafara.


Mwenyekiti huyo, baada ya ‘kukiet’ chini kati ya mti mmoja ndani ya shamba lao hilo lililoko bonde la Dobi Wawi Chake chake Pemba, ndipo hapo alipopata fursa ya kunipa utandu na ukoko.

Kwenye shamba hili la ‘MEO’ wenyewe bila ya kuona uvivu na kwa lengo lilelile la kuhifadhi mazingira, wameotesha miti zaidi ya aina tisa, huku wakiendelea kuitunza ile ya asili kama Mzambarau.

 Sikuwa na hamu ya kutaka kuondaoka ndani ya shamba hilo, maana kila kona ya jicho langu linavyokwenda, hukumbana na Mivinje, Mitondoo, Mikungu, Mikeshia na hata zao la Mkorosho.

Kwani kiujumla hii aina ya miti ninayoiona imo mingapi, niliuliza na mwanachama wa ‘MEO’ Ali Khamis Omar ndie aliepewa jukumu na Mwenyekiti kunipa idadi halisi.

Bila ya kuchachawa…. mwanachama huyo aliekuwa amevalia mavazi rasmi ya shambani, alisema wanayo Mivinje 9,000, Mitondoo 300, Mikungu 700, Misaji 100, Miembe 250, Mikeshia 100, Mikorosho 200, bila ya kusahau zao la nanasi 4,000.

Lakini pia MEO kwa vile lengo kuu ni kulirejeshea hadhi yake eneo hilo lenye urefu za zaidi ya ekari tisa, (9) wameamua kuitunza miti ya asili kama Mizambarau, Mitope tope na Mifuu.

Mwanachama huyo wakati akizungumza na ukurasa wa makala, hakuacha kusema kumbe upandaji wa miti unaweza kumvua mtu na umaskini alionao, kama atalijua hilo mapema.

Kihistori ya Kikundi hicho cha shehia ya Wawi Wilaya ya Chake chake, Mkoa wa kusini Pemba, kilianza mwaka 2011, ambapo hapo chini ya wanachama wao 19.

“Unajua ndani ya MEO yaani ‘Mchekeni Environmental Organization’ wapo pia na wanawake, lakini wanawake waliomo ni majasiri maana kila kazi wanafanya’’,alisema Mwenyekiti

Wanachama wa MEO walikuwa wakichacharika kwa nguvu, na hasa walikuwa wakipata hamasa, baada ya wananchi wa Wawi wakiwacheka kutokana na kupannda miti isio na chakula cha haraka.

“Hapa sisi tulichekwa na jamii ya Wawi na vitongoji vyake, na wengine walitoka, lakini tulishikamana na kutoa fedha zetu mfukoni, ili eneo hili tulipande miti’’,alisema Katibu wa MEO Kombo Yahaya Juma.

MEO pamoja na fedha taslimu na nguvu kazi, walijikuta wameshatumia zaidi ya shilingi 10 milioni, ambapo kama ukizichanganya za zile za TASAF, utakuta shilingi 19 milioni zimewekezwa msituni.

‘’Tulifika hata kijiji cha Vitongoji, Wete kusaka mbegu za Mivinje, Mitondoo na Mikungu, wananchi wengine walitushangaa’’,alinifafanulia.

Mvua za masika kuanzia mwaka 2011 na mwanzoni mwa mwaka 2012, walizitumia vyema kwa upandaji miti, na leo hii wakizisubiri kwa hamu fedha za mavuno ya miti, pale watakapoanza kuvuna.

Ingawa Mwenyekiti huyo, aliswenenaka sana kwamba walipata kazi kubwa sana wakati ilipokuwa michanga miti hiyo, kutokana na wafugaji kutumia kama sehemu ya malisho ya wanyama wao.

‘’Wengine sisi wanakamati tulikaribia kuachana na mradi huu, maana wanaotufungia Ng’ombe ni ndugu na jamaa zetu, na kila siku hua tunawambia, sasa ukienda jioni mifugo imo’’,alisikitika.

Ingawa alieleza kuwa wapo baadhi ya wananchi walikuwa mstari wa mbele kuwapa nguvu, hasa kutokana na kuelewa kuwa mradi huo ni kwa ajali zaidi ya kuhifahdhi mazingira.

Lakini kazi nzito zaidi ya mradi huo, ni pale walipofika wakati wa kuipalilia kwa maana ya kuisafishia hapo ilibidi wanachama wahamie bondeni na wakafanikiwa.

“Ama kweli kila mazigo ukikaribia kufika, ndio machofu houngezeka, maana na sisi wakati wa kuilimia ugumu ulijitokeza, lakini tulifanya hivyo hadi leo imekuwa safi’’,alisema wakati akiwa ameegemea Mvinje Mwenyekiti huyo.

Wakati huu kwa mujibu wa wanaushirika hao, ni kwamba baadhi ya miti kulingana na aina ya matumizi inaweza kuvunwa, lakini hilo hawajalifikiria kwa sasa.

‘’Unajua ukitaka Mvinje hasa uunvune na kupata fedha nzuri, uusubiri alau miaka mitano, nadio hapo ukitaka guzo la umeme, ukitaka ya kujengea na kazi nyengine’’, alielezea kitaalamu Mwenyekiti.

Mradi huu ualionza baina ya mwaka 2010 na 2011, kwenye mradi huo TASAF awamu ya pili iliwapa ‘MEO’ jumla ya shilingi 9 milioni kwa ajili ya kujiendeleza.

Kwa mujibu wa aliekuwa Mratbu wa ‘TASAF’ Pemba, Issa Juma Ali, miradi ya aina hiyo, walengwa huwa hawapaswi kuchangia, fedha taslim bali ni nguvu kazi pekee.

‘’Miradi ya aina hii wananchi hupata mteremko, kama wanaosukuma mlevi tu, wao mchango wao ni jasho lao, na sio fedha kama ilivyo miradi mengine ya kimaendeleo’’, aliweka bayana.

Kama Jumuia hiyo ya ‘MEO’ itavuna kwa pamoja miti yote wanaweza kujipatia zaidi ya shilingi 35.5 milion, kwenye idadi yote ya miti ifikayo 25,000.

Ingawa uongozi wa MEO ulisema lengo hasa, sio kuotesha miti hiyo na kisha kuvuna, bali uvunaji wake utaenda samba mba na uhifadhi wa mazingira.

“Unajua hatutaki kuotesha miti hii na kurejesha hali yake ya zamani, kisha akija mtu aone pana jangawa, bali uvunaji wake tutaomba wataalamu watuelekeze’’,alisema Katibu.

Juma Mohamed ambae ni mwananchi wa Wawi, alisema mradi huo awali hawakuona kwamba, unaweza kuleta maslahi, lakini kwa sasa hali ya eneo hili limeimarika.

Lakini Amini Haji Ali na Asha Kombo Hilali wanasema suala la upandaji miti pamoja na kuhifadhi mazingira, ni chanzo kikuu cha kujipatia fedha na mvua ikiwa mradi huo utatunzwa.

Wakati suala la ukataji miti ovyo na uchafuzi mwengine wa kimazingira ukifanyika sheria ya usimamizi wa mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2015 haikukaa kimnya.

Maana katika kifungu cha 51 (1) kimeweka marufuku kwa mtu yeyote kuchafua au kumruhusu mtu mwingine kufanya kitendo hicho kitakachosababisha uchafuzi wa mazingira kwa kukiuka viwango vyovyote vya kimazingira vilivyoweka na sheria yoyote inayotumika.

Na ndio  maana kifungu cha (2) kimeweka adhabu kwa kwa yeyote atakayekwenda kinyume na masharti ya kifungu hiki atahesabiwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo kwa muda kisichopungua miaka miwili na usiozidi miaka mitano au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii, misitu kadhaa ya Tanzania inabailiwa na changamoto kubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu, uvunaji holela wa mbao, miti ya majenzi na utipagaji mkaa.

Tanzania inakisiwa kuwa na hekari milioni 33 za misitu na miti ya mbao, ambapo taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa na Kilimo kwenye utafiti wale wa mwaka 2010 (Forest Resources Assessment) ulieleza kuwa imekuwa ikipoteza wastan wa hekari 400,000 ya misitu kwa kwa miongo miwili mfululizo sasa.

Ingawa juhudi za serikali ya Tanzania baada ya kujitokeza hilo mwaka huo huo, ilianzisha shirika huru lenye dhamana ya kusimamia ustawi wa misitu (Tanzania Forest Services Agency) ingawa taarifa zainaeleza shirikia hilo lilishinwa kusimamia vyema, alisema Felician Kilahama.

Yeye ni Afisa Misitu Mwandamizi aliekuwa akifanya kazi katika Idara ya misitu na nyuki Wizara ya Maliasili, Misitu na Utalii.


Asasi za kirai kama zikisimamiwa vyema na serikali kuu kwa kushirikiana na Idara za mazingira na misitu, zinaweza kuimarisha misitu na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.