STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 18.9.2015

VIONGOZI wa CCM Zanzibar wamewataka wananchi na wanaCCM kumpigia kura Dk.
Ali Mohamed Shein ili aendelee kuiongoza Zanzibar katika miaka mitano ijayo kutokana
na uwezo wake wa kuongoza na kutowapa kura viongozi wa upinzani kwani hawana
sifa za kuongoza na Sera zao ni za ubabaishaji.
Maneno hayo waliyaeleza kwa nyakati
tofauti katika mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika Chokocho,
Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na
wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa
tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Viongozi hao wa CCM walipata fursa ya
kusalimiana na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano huo na
kuwapongeza wananchi hao wa Pemba kwa kuonesha azma ya kuendelea kuiunga mkono CCM.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
Mhe. Pandu Ameir Kificho alitoa shukurani kwa uongozi bora wa Dk. Shein ambao
umewafanya wanaCCM, wakerekwetwa na viongozi wa chama hicho wapenda amani
kumshauri wakati wa ziara zake Unguja na Pemba na kumtaka achukue fomu ya
kugombania tena nafasi ya Urais.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuja kutokana
na maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyoletwa na CCM katika uongozi
wa Dk. Shein, na kueleza kuwa Dk. Shein hakutoa fedha ili achaguliwe katika
kuwania nafasi hiyo kama wanavyofanya wagombea kutoka vyama vyengine lakini wao
ndio waliomchangia fedha ili akachukue fomu ya kugombania nafasi hiyo.
Spika Kificho alisema kuwa hivi sasa
kilichobaki ni kumpa zawadi Dk. Shein ambayo ni kumpa kura zote za ndio na
kusema kuwa ili Dk. Shein afanye kazi vizuri pia, ni lazima wawapigie kura
mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli na Mgombea
Mwenza wake Mama Samia Suluhu Hassan, Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wa CCM.
Nae Omar Yussuf Mzee, ambaye ni Waziri wa
Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema kuwa Ikulu haijaribiwi na
kuwataka wananchi na wanaCCM wasimjaribu mtu ambaye hana sifa za kwenda Ikulu
na kuwaeleza kuwa kuna kila sababu za kumchagua Dk. Shein.
Alisema kuwa Dk. Shein ni mwadilifu,
muaminifu, si mbaguzi, anasimamia maendeleo Unguja na Pemba na kusisitiza kuwa
jengo la uwanja wa ndenge atalifungua yeye sambamba na kuizindua meli mpya ambayo inatarajiwa kuwasili mapema
mwezi ujao.
Omar Yussuf alisisitiza kuwa sababu
nyegine ya kumrejesha tena Dk. Shein madarakani ni kuwepo kwa amani na utulivu
ambayo yeye ameweza ,kuisimamia vizuri na kueleza kuwa kazi iliyopo ni kumpigia
kura Dk. Shein pamoja na viongozi wote
wa CCM.
"Walinikimbia siku niliyosoma Bajeti
ya Serikali ambayo ni bajeti yetu sote na inayotusaidia katika mambo yetu mbali
mbali ya maendeleo...msiwachague hawafai",alisema Omar Yussuf.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Vuai Ali Vuai, alitoa pongezi kwa wanaCCM wa Pemba kwa kuendelea kukiunga mkono
Chama Cha Mapinduzi na kutoa pongezi kwa niaba ya wanaCCM kwa uwamuzi wake wa
kuwaeleza wananchi kuwa mwaka wa kwanza atakapochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar
ataongeza mshahara hatua ambayo inatokana na Dk. Shein kuwajali na kuwapenda
wananchi wake.
Pongezi kwa uwamuzi wake na kuwapenda
watu kwa kumuagiza Waziri wa Fedha kuhakikisha kuwa meli mpya inanunuliwa na
tayari hatua hiyo imechukuliwa na hivi karibuni meli hiyo itafika na
itawasaidia wananchi wote wa Zanzibar katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Nae, Bi Zainab Omar Mohammed ambaye ni
Waziri wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana , Wanawake na Watoto nae
alieleza kuwa hana wasi wasi wowote kwani tayari Dk. Shein ameshashinda
uchaguzi wa mwaka huu na kusisitiza kuwa siku ya kupiga kura wawapigie kura viongozi wote wa CCM bila ya
woga na wasi wasi wowote.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohammed Aboud alisema kuwa CCM haitoondoka madarakani kutokana
na mazuri iliyoyafanya na kuwataka wanaCCM na wananchi kuendelea kuiunga mkono huku
akieleza kuwa chama cha CUF tayari kimejipanga kuiba kura za Pemba kama ilivyo
kawaida yao.
Aidha, alisema kuwa chama hicho cha CUF
kina mpango wa kuwanunua mawakala na Maafisa wa Uchaguzi, na kutoa onyo kwa yeyote
atakae nunuliwa na akanunulika hatua zinazofaa zitachukuliwa dhidi yake.
Alisema kuwa njama za chama hicho zinajulikana
na kueleza kuwa maendeleo ya kweli ya Zanzibar yanaletwa na yataendelea kuletwa
na CCM huku akishangazwa na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif kwa kutowasaidia ndugu zake wa Pemba hata kuwachimbia kisima.
Waziri Aboud alisema kuwa Dk. Shein ndio
atakae ibadilisha Zanzibar, kwani nia yake ni kuimarisha uchumi kwa kasi kubwa
zaidi ili kuondokana na umasikini na kuongeza ajira na kuwaeleza kuwa tayari
Kisiwa Panza na Makoongwe umeme umeshafika ambazo hizo zote ni ahadi na juhudi
za Dk. Shein.
Alieleza kuwa CCM haina wasi wasi kwani
wanaenda kushindana na Ukawa sio vyama vya siasa, huku akisisitiza kuwa CCM ina
Ilani yake inayoinadi na kuwataka kuwaacha wapinzani waendelee kupiga porojo na
wao waendelee kutangaza Sera madhubuti za CCM pamoja na Ilani yake
Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa, akiwakaribisha viongozi na WanaCCM pamoja
na wananchi katika Mkoa huo na wamelaani tabia za wapinzani za kuchana mabango
na picha za wagombea wao zikiwemo picha za viongozi wanaogombania.
Alisema kuwa tayari kuna choyo
zilizokuwepo kwa wanachama wa chama cha CUF hali ambayo inawapelekea kuanza
kuzichana picha za wagombea wa CCM jambo ambalo linatokana na choyo hicho kwa
kuona kuwa picha hizo ni nzuri, zinavutia wakiwemo wagombea wa chama hicho
wakifananishwa na wengine.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment