Habari za Punde

Magufuli aitikisa ngome ya CUF Pemba


  • Mapokezi yake asema yamedhihirisha kuwa atashinda
  • Aahidikuwa  Rais wa watanzania wote
  • Atadumisha Muungano
  • Avunja kambi ya CUF:80 WAJITOA CUF
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli ameahidi akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha kuwa atakuwa kiongozi wa wananchi wote bila kubagua.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni huko Gombani ya Kale Chake Chake Pemba alisema yeye hakuomba nafasi hiyo kufanya majaribio bali amedhamiria kufanyakazi kwa bidii kuwatumikia watanzania kwa bidii zote.

“Sikuomba nafasi hii kwa majaribio, nimedhamiria kufanyakazi na nyinyi na mapokezi yenu ni ishara kubwa kuwa mmenikubali kuwa Rais wenu”alisema Dk. Magufuli.
Alinainisha kuwa akichaguliwa moja ya malengo ya uongozi wake ni kuulinda Muungano wa Tanzania ambao aliueleza kuwa una umuhimu wa kipekee.

“Tanzania ni moja na yenye watu wamoja ndio maana wametapakaa kote kila kona ya Tanzania wakiishi kwa amani bila kubugudhiana”alieleza Dk. Magufuli huku akisalimia wananchi kwa lugha mbalimbali za Tanzania.

Aliwaeleza maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa yeye akichaguliwa atashirikiana bega kwa bega na mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama chake Dk. Shein ambaye alimuelezea kuwa mtu makini na mchapakazi.

“Nimefanya kazi na Dk. Shein akiwa Makamu wa Rais ananifahamu na ninamfahamu amefika hata kijijini kwangu. Nitaendelea kumuheshimu na naahidi kushirikiana naye katika kudumisha Muungano wetu na kuleta maendeleo ya nchi yetu” Dk. Magufuli alieleza.

Aliongeza kuwa akichaguliwa atashirikiana na Dk. Shein kusimamia rasilimali za nchi kwa kukomesha ufisadi ili kuleta maendeleo ya haraka kwa Tanzania na hatimae kuinua kiwango cha maisha ya watanzania wote.


Mgombea huyo wa CCM alisema kuwa alifurahi alipoomba kugombea nafasi hiyo kuwa atapata nafasi ya kufanyakazi na Dk. Shein mtu ambaye anamuamini kuwa mtu anayeleta matumaini kwa wananchi.

Katika kuimarisha Muungano alieleza kuwa ataendelea kuzifanyia kazi kero za Muungano ambazo alisema zimebaki 4 tu na kwamba kwa kuwa Mgombea Mwenza wake ni Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa waziri anayeshughulikia Muungano haitakuwa tatizo kuzipatia ufumbuzi.

“Ninawahakikishia wananchi wa Unguja na Pemba kila nitakachokipata kwa maendeleo yenu nitakileta bila ya kinyongo” alisema Dk. Magufuli na kusisitiza kuwa kama ilivyokuwa awamu iliyopita ushirikiano katika miradi ya pamoja utaendelezwa.

Kwa hivyo aliwaomba wananchi Pemba kukichagua Chama cha Mapinduzi kupata Makamu wa Rais mwanamke ambaye alihidi kufanya mambo makubwa kwa maslahi ya wanawake na watoto wa nchi yetu.

Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa Pemba warejeshe mshimakamano wao kwa kuwachagua yeye na Dk. Shein kushika madaraka na hakuna wakati mwingine kwao kufanya mabadiliko kwa wananchi wa Pemba ila hivi sasa kwa kuwachaguwa wagombea hao wa CCM.

Aidha aliwataka wananchi wa Unguja na Pemba kutokubali kuchonganishwa na kutengenishwa na wanasiasa ambao wengi wao wamewekeza biashara kubwa kubwa, makaazi na maisha yao Tanzania Bara na kwengineko.

“Wote wanaowachonganisha wamejenga Bara, wanafanya biashara zao kubwa kubwa Tanzania Bara, wanakaa Bara; msikubali, semeni inatosha. Anayetaka muandamane mwambieni atangulie yeye, mke wake na watoto wake na nyie mfuate nyuma.

Hata hivyo alisema yaliyopita si ndwele wagange yajayo hivyo kuwataka wahakikishe wanatunza amani ili Zanzibar iendelee kuwa tulivu kuweza kupokea wageni mashuhuri kama ilivyo sasa.

“Wanapokuja wageni Zanzibar inapata fedha na tunatumia kufanyia shughuli za maendeleo”alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Alisisitiza kuwa atashirikiana na Dk. Shein kuwaletea wananchi maendeleo na kuwaambia wananchi hao“Mimi sitawaangusha kabisa, ninaomba mnichague niwe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini na wafuasi wa CUF na wasio na vyamawatanichagua kwani wamefika kunisikiliza”

Katika mkutano huo wanachama 80 wa chama cha CUF walikihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi.

2 comments:

  1. hamna lolote nyinyi CCM mumekusudia muibe na huko Pemba mara hii ndio mana hamutoki Pemba

    ReplyDelete
  2. Rais ni Magufuli taka usi take. Kila kitongoji kikipata kura 15 tuu tayari CCM watakuwa wameshinda kwa asilimia 78 .

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.