Mgombea Urais wa
Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia
mkutano mkubwa wa aina yake wa kampeni katika mji mdogo wa Nungwi katika mkoa
wa Kaskazini Unguja na kuwataka wananchi kukichagua chama hicho kwa kuwa ndicho
kinachothamini na kinachotekeleza malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Aliwaambia maelfu ya
wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa wanapaswa kuichagua CCM kwani ndicho
chama chenye uwezo na kimeonesha mfano wa utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi
na ahadi za Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Mzee Abeid Amani Karume.
“Mapinduzi ndiyo
yaliyoweka msingi wa usawa na kuondosha ubaguzi ambao uliwanyima haki na
kuwakandamiza wananchi walio wengi wa Zanzibar” Dk. Shein alieleza.
Katika mnasaba huo alisema
kuwa Mapinduzi yalileta usawa na kujenga mazingira ya kuijenga nchi yetu kwa
ushirikiano na kwa umoja wetu na kwa maslahi yetu wote.
Mgombea huyo wa CCM
alisema Zanzibar ni maarufu ulimwenguni kote tokea karme nyingi zilizopita
lakini umaarufu huo hautakuwa na manufaa kwetu endapo hatutaweza kulinda na
kuienzi amani na utulivu uliopo.
Katika kipindi
kijacho aliahidi kuimarisha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, umeme na maji pamoja
na miundombinu ya barabara ili kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hizo kutokana
na mji huo kupanuka sana kutokana na shughuli za biashara ya utalii.
“Tutaimarisha huduma
za umeme kwa kuweka transfoma kubwa yenye KVA 200 katika mji mpya ulioko Ras
Nungwi itakayoweza kuhudumia wateja wengi na kwa uhakika zaidi” Dk. Shein
alisema na kuongeza kuwa mji huo mdogo utawekewa taa za barabarani hadi
Kivunge.
Dk.Shein aliwaeleza
wananchi hao kuwa biashara ya utalii ndio inayoipatia Zanzibar fedha nyingi za
kigeni hivyo lengo la Serikali katika miaka mitano ijayo ni kuongeza idadi ya
watalii wanoitembelea Zanzibar ifikie 500,000 ifikapo 2020 kutoka 300,000 hivi
sasa huku jitihada zikielekezwa katika kuimarisha uwezo wa wananchi kitaaluma wa
kuweza kuhudumia sekta hiyo.
Aliwaeleza wananchi
hao kuwa kupanua haraka kwa mji Nungwi ni uthibitisho kuwa Nungwi inaendelea kusonga
mbele kwa kujenga majengo mengi na hoteli nyingi za kitalii.
Dk. Shein aliahidi
atakapochaguliwa tena Serikali yake itawajengea uwezo wavuvi nchini kwa
kuwapatia boti zenye ukubwa wa kati na kubwa ili waweze kuvua kwa uhakika na
kupata mapato makubwa zaidi.
Kwa upande wa kilimo
cha mwani, dk. Shein alisema ataiamarisha masoko la mwani kwa kutafuta masoko
mapya ya zao hilo ili wakulima waweze kupata bei nzuri na kufaidi jasho lao.
No comments:
Post a Comment