Habari za Punde

Mkutano wa CUF Mwambe, jimbo la Kiwani Pemba


 Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wanachama wake katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwambe jimbo la Kiwani.
 Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wanachama wake katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwambe jimbo la Kiwani.
 Wafuasi na wapenzi wa CUF wakisikiliza mkutano huo
 Wafuasi na wapenzi wa CUF wakisikiliza mkutano huo

 Fundi wa kiwanda cha uzalishaji chumvi cha Mkamandume Bw. Ramadhan Zaral Haji, akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusiana na namna ya uzalishaji wa bidhaa hiyo.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiingia katika mabwawa ya uzalishaji chumvi Mkamandume, kuangalia hali ya uzalishaji.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia kifaa kinachopima kiwango cha maji kwa ajili ya uzalishaji chumvi “Hydrometer” alipotembelea mabwawa ya uzalishaji chumvi Mkamandume. (picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad, OMKR.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema anakusudia kujenga taifa lenye umoja, usawa na haki bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Akihutubia mkutano wa kampeni za chama hicho uliofanyika viwanja vya Mwambe jimbo la Kiwani, amesema kwa kipindi kirefu wananchi wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi, na kwamba serikali yake itahakikisha kuwa kila Mzanzibari aliyetimiza sifa atapatiwa haki hiyo.

Sambamba na hilo, Maalim Seif amesema anakusudia kujenga taifa linaloheshimu haki za binadamu na utawala mwema, na hakuna mtu atakayekuwa juu ya sheria.

Amesema katika msingi huo Zanzibar inahitaji kuwa na mamlaka yake kamili, ili kujenga uchumi madhubuti utakaowanufaisha wananchi.

Amesema chini ya serikali itakayoongozwa na CUF, huduma za afya na elimu zitatolewa bila ya malipo, tofauti na ilivyo sasa ambapo wagonjwa na wazazi wamekuwa wakikabiliwa na michango mikubwa wanapohitaji huduma hizo.

Nae msaidizi mratibu wa kampeni za CUF kisiwani Pemba Said Ali Mbarouk amesema bila ya mamlaka kamili Zanzibar haitoweza kujikomboa kiuchumi na kijamii.

Amewataka wanachama wa Chama hicho kumchagua Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar, kwani ni kiongozi mwenye ujasiri, uwezo na uzalendo wa nchi yake.

Amewasisitiza wanachama hao kupuuza vitisho vinavyotolewa dhidi yao, na badala yake wajipange kuweza kupiga kura tarehe 25 Oktoba mwaka huu.

Katika mkutano huo ambao jumla ya wanachama 678 wamejiunga na chama hicho baadhi yao wakitoka vyama vya ADC na CCM, Maalim Seif ameelezea matumaini yake kuwa ushindi wake katika uchaguzi ujao hautopungua asilimia 80.

Kabla ya mkutano huo uliojumuisha majimbo ya Kiwani na Chambani, Maalim Seif alitembelea mabwawa na kiwanda cha uzalishaji chumvi katika eneo la Mkamandume na kuahidi kuwa serikali atakayoiongoza iwapo atachaguliwa itatoa msukumo mkubwa kwa wazalishaji hao wa chumvi.

Katika risala yao iliyosomwa na Baraka Shaib Baraka, wazalishaji hao wa chumvi maarufu kiswani Pemba wamesema wanakabiliwa na uchakavu mkubwa wa mashine zao, jambo ambalo limepunguza uzalishaji kutoka polo elfu saba hadi polo elfu mbili.

Hivyo wameomba kusaidiwa mashine hizo pamoja na mabomba ili kukifanya kiwanda hicho kiende na wakati na kuongeza uzalishaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.