Na Mwandishi Wetu.
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamewataka wanaCCM kuendeleza amani na utulivu
iliyopo hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika
mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi na
wanaCCM uliofanyika katika viwanja vya MnaziMmoja, mjini Zanzibar walisisitiza amani kuelekea uchaguzi mkuu
ujao.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ali Hassan Mwinyi alimuomba MwnyeziMungu kuufanya uchaguzi mkuu ujao
uwe wa amani na salama.
Mzee Mwinyi aliwaomba wanaCCM kuhakikisha
kuwa wanalinda amani na kutaka ibakie ili uchaguzi mkuu ujao uwe wa amani.
Alisisitiza kuwa ni lazima kufanyike
juhudi za makusudi ili kupatikana ushindi na CCM itashinda kwani ina sifa na
inastahiki kushinda huku akimuelezea Dk. Magufuli na Dk. Shein kuwa ni wachapa
kazi.
CCM ni chama chenye maarifa na kinachojua
mambo ila kuna watu wachache wanao haribu mambo na kusema kuwa tayari Dk.
Magufuli ameshawapiga darubini kwani ana sifa za uongozi, mkweli, muadilifu,
mpenda watu, muaminifu hana ubaguzi na akishinda atakuwa mwema kwa watu wote.
Aidha, alisisitiza kuwa kwa upande wa
Zanzibar kura zote apewe Dk. Shein na kwa Tanzania nzima apewe Dk. Magufuli ili
kuanza nchi mpya na kuuliza Zanzibar ya leo sawa na ya zamani.
Alisema kuwa Zanzibar imebadilika
kutokana na maendeleo makubwa yaliopatikana katika sekta mbali mbali na
kusisitiza kuwa kura zote wapewe viongozi wa CCM wanaogombania nafasi.
Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Muhammed Kharib Bilal
kwa upande wake alisema kuwa chama cha CUF kimekuwa na kauli za kuibiwa kila
kipindi cha uchaguzi kinapofika na kueleza kuwa kauli hizo zinaonesha wazi kuwa
chama hicho hakikubaliki.
Alisema kuwa Dk. Magufuli ni mchapa kazi,
muadilifu, anakipenda chama chake, anapenda Muungano, hapokei rushwa, hajawahi
kushughulikiwa kwa ufisadi hata mara moja.
Nae Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif
Idd akiwasalimia wananchi alisema kuwa wapinzani wapende wasipende ushindi wa
CCM ni jambo la lazima na kuwasisitiza wanaCCM wapambe maskani zao na matawi
yao kwa ajili ya kusherehekea ushindi.
Alisema kuwa hivi sasa wapinzani wamekuwa
wakisema maneno yaliopo na yasiopo huku akirejea kauli ya Maalim Seif
alipokwenda Tume ya Uchaguzi kutaka kuapishwa eti akisema kuwa yeye tayari
ameshashinda uchaguzi.
Balozi Seif alisema kuwa ni vyama vya
siasa vimekubaliana kuendesha kampeni za kistaarabu hivyo kuna kila sababu ya
kundesha kampeni hizo kistaarabu ili kuiweka Zanzibar iwe ya utulivu na amani.
Aidha, alilaani kitendo cha kuwekwa rangi
nyekundu katika picha za kampeni za Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya
CCM, Dk. Ali Mohamed Shein katika maeneo ya Chukwani na kusema kitendo hicho ni
cha kichokozi.
Alieleza kuwa Zanzibar haitaki vurugu na
kama ameshaamua kuwaambiwa wafuasi wake wafanye vurugu CCM haiko tayari na hilo.
Aidha, aliwaonya wale wote walioamua
kufanya vurugu siku ya uchaguzi mkuu vyombo vya dola havitokuwa tayari kuona
hilo likitendeka.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania
ambaye pia, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM Alhaj Gulembo aliwataka Wazanzibari kutokuwa na wahaka kwani viongozi
wote wa CCM wanaogombania nafasi watashinda na waliobaki ni kalagabao.
Akieleza kuhusu mabadiliko walieleza kuwa
wanamnukuu vibaya Mwalimu kuhusu mabadiliko kuwa wakiyakosa ndani ya CCM
watayapata nje ya CCM, hiyo ni kwamba CCM ikiendelea kuwaweka mafisadi ndani ya
chama hicho ndio hilo linalotokea na kuuliza kati ya Magufuli na Lowasa nani fisadi.
Alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar Maalim
Seif Sharif ndio ni fisadi kwani alichokuwa akikitaka yeye ni ukubwa ili aweze
kupata ulinzi na kueleza kuwa Ikulu ni sehemu ya pekee na wanaenda watu maalum.
Alisema kuwa Maalim Seif alikuwa na
Lipumba na Lipumba baada ya kuondolewa kwenye dili la urais na kuingia Lowasa
akaamua kuachia ngazi kwani hakuwa tayari kununuliwa.
Akimnadi Dk. Shein, Dk. Bilal alisema
kuwa Dk. Shein ni mchapakazi, muaadilifu, anaependa watu anaetetea wananchi,
anaependa chama chake na wanachama wake na anaetetea Muungano na Mapinduzi ya
Januari 12, 1964.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
alitoa pongezi kwa wanaCCM waliofurika katika mkutano huo na kusema kuwa umati
mkubwa uliohudhuria katika mkutano huo ni ishara tosha kuwa Dk. Magufuli
atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Shein kuwa
Rais wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mjini, Borafya
Ame Silima alieleza kuwa tayari CCM imeshapata ushindi na kilichobakia kwa
viongozi hao ni kuapishwa akiwemo Dk. Shein kwa upande wa Zanzibar na Dk. John
Magufuli kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment