Habari za Punde

WanaCCM watakiwa kutambua historia yao na kutambua maendeleo yaliopatikana baada ya Mapinduzi

VIONGOZI wa CCM Zanzibar wamewataka wananchi na wanaCCM kuwachagua viongozi wa chama hicho ili waendelee kuwaletea maendeleo endelevu yaliotokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Hayo waliyaeleza leo huko katika mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika Jimbo la Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Viongozi hao wa CCM walipata fursa ya kusalimiana na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano huo waliwataka wanachi na wanaCCM kutambua historia yao na kutambua maendeleo yaliopatikana baada ya Mapinduzi.

Bi Fatma Karume nae alipata fursa ya kusa,limiana na wananchi na wanaCCM katika mkutano huo na kueleza kuwa Bumbwini mpaka Makoba pamoja na Kiongwe kumshukuru MwenyeziMungu kwa kuwapa neema.


Alisema kuwa ASP iliundwa kwa lengo la kuwatetea wanyonge na kuwasifu watu wa Bumbwini kwa kuiunga mkono CCM na kueleza kuwa Mapinduzi ndio yalioleta na kama si Mapinduzi maendeleo Bumbwini yasingepatikana.

Bi Fatma alisema kuwa watu wa Bumbwini lazima wawe macho na wawakatae wapinga maendeleo na badala yake kinachotakiwa hivi sasa ni maendeleo yanayoletwa na CCM na kuwaombea kura viongozi wa CCM.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambaye pia, ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alisema kuwa kabla ya Mapinduzi kulikuwa na skuli mbili katika Mkoa huo ya Mkwajuni na skuli ya Donge lakini katika maeneo yote ya Mkoa huo na baada ya hapo ndipo ikajengwa skuli ya Bumbwini na Kinyasini.

Alisema kuwa watu wa maeneo mengine yaliobakia katika Mkoa huo hawakupata fursa ya kusoma na mara baada ya Mapinduzi ndipo walipopata fursa na skuli nyengine zilipoanza kuenea pamoja na kuwa na kituo kimoja tu cha afya cha Mkokotoni kabla ya Mapinduzi ambapo wanaume waligeuzwa kuwa magoigoi katika majahazi.

Alisema kuwa kwa hivi sasa elimu, afya na sekta nyengine nyinzi zimeimarika na hivi sasa maendeleo makubwa yapo katika mkoa huo ambayo yamekuja baada ya Mapinduzi chini ya ASP na hatimae CCM.

Waziri Kheir alishangwa za na wale wanaodai mamlaka kamili wakati tayari Zanzibar ina mamlaka yake kamili na kusema kuwa anaamini kuwa CCM itarejeshwa madarakani kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani  na Sera zake.

Alisema kuwa wafuasi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakileta usumbufu mkubwa barabarani na kwa lengo la kutafuta sababu za kuleta vurugu na kusema kuwa mwaka huu Zanzibar vurugu hazipo na kuwataka wanaCCM kuvihifadhi vizuri vitambulisho vyao vya kupigia kura.

Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa ushindi wa CCM hauna shaka wala hakuna wa kuuzuia na kusisitiza kuwa mwaka huu ndio mwisho wa chama cha CUF.

Balozi Seif aliwataka wananchi wa Kaskazini B kuanza kupamba maskani zao kwani ushindi wa CCM unakuja na kusema kuwa upinza hivi sasa hauna hoja na hoja yao ni kumsema yeye katika mikutano yao ya hadhara.

Katika maelezo yake alishangazwa na kauli zinazotolewa na viongozi wa CUF kuwa yeye pamoja na Haji Omar Kheir na Hamza Hassan watampelekwa The Hague, na kueleza kuwa viongozi wa kulepekwa huko ni wa CUF kutokana na matukio mengi waliyoyafanya yakiwemo kusababisha maafa kwa wananchi katika matukio kadhaa waliyoyatengeza kwa makusudi.

Balozi Seif alieleza kuwa CUF inaandaa vurugu katika uchaguzi ujao kwa kutaka kujipanga huko Bwawani kwa lengo la kusubiri matokea na yakiwa hayajawaridhisha wanakusudia waanze vurugu kuanzia eneo hilo na kusisitiza wasijaribu kufanya hivyo kwani wenye kazi zao wapo.

Alisema kuwa chama hicho cha upinzani hivi sasa kina mpango wa kutafuta fulana za CCM ili wafuasi wao wavae siku ya uchaguzi kwa lengo la kufanya fujo, na kusisitiza kuwa CCM itahakikisha inasimamia amani na utulivu na kusisitiza kuwa vyombo vya Dola vitasimia na kuwadhibiti wale wote watakaofanya vurugu.

Aliwataka wapinzani kuacha kumsingizia mambo ambayo hajayafanya kwani hizo sio siasa wala demokrasia ya vyama vingi, ambapo pia alitumia fursa hiyo kuwaombea kura viongozi wa CCM akiwemo Dk. Shein, John Magufuli na Mama Samia na kusema kuwa viongozi hao wakishirikiana pamoja maendeleo makubwa yataendelea kupatikana nchini.

Naibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alitumia fursa hiyo kueleza mambo kadhaa ambayo ndiyo yanayokifanya chama cha CUF kumchukia Balozi Seif Idd huku akieleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM nalo pia limekuwa ni mwiba kwa CUF.

Alisema kuwa watu wanaoweza kuwaunganisha na kuwaongoza watanzania na wazanzibari ni Dk. Shein na Dk. Magufuli na Samia, Wabunge, Wawakilishi  na Madiwani wa CCM.

Balozi Amina Salum Ali kwa upande wake, alipongeza maendeleo yaliopatikana katika Jimbo hilo pamoja na Mkoa mzima wa Kaskazini ikiwa ni pamoja na uimarishwaji wa miundombinu ya barabara, huduma za afya, umeme, maji safi na salama.


Alisema kuwa Dk. Shein ana mapenzi makubwa na wananchi wakiwemo akina mama ambapo hali hiyo imekuwa ikionekana kutokana na juhudi kubwa alizozichukuwa za  kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo huduma za afya hasa katika Jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.