Habari za Punde

Unyama huu wa kwa watoto wenye VVU hadi lini?

Na Haji Nassor, Pemba

…HUU ni zaidi ya unyama...

Ahaa…kumbe hawakukosea wahenga waliosema kuni inayoteketea jikoni, huchekwa na ilio kando…….

Naamini walikua na maana pana, kwamba ile kuni ilio kando haijui kuwa ikimaliza iliojokoni ni zamu yake.

Kwenye jamii, watoto ndio kuni zilizojikoni, na kuni za kando ni wazeeo, wengi husema watoto ni taifa la kesho.

Wengine husema ni taifa la leo, kauli zote hizo zinaingia akili, maana, wapo watoto wameshatoa mchango mkubwa taifa kama vile michezo ya riadha, usanii na hata kuhifadhi kura-an au bibilia.

Sasa kama hayo yote yanaaingia akili, iweje jamii ya leo na wanaoitwa watu wazima wa taifa hili, kuwafanyia unyama watoto wetu ambao tunakubaliana ndio taifa la leo.

Kwani hawapo watu wanaoonekana na heshima zao na akili zao wanawanyanyapaa watoto wanaoishi na VVU au hata wazazi wao waliokufa kwa sababu hizo.

Kisiwa cha Pemba kama kilivyo cha Unguja, nacho kimejipatia umaarufa mkubwa ukanda wa Afrika Mashariki na kati, kutokana na wakaazi wake kuwa ni wakarimu na wapenda watu.

Wageni wangi walivutika sana kufikia Kisiwani Pemba, ili kujionea ukarimu wa watu wake uliojaa neema na uaminifu hali iliopelekea kisiwa hicho kujipatia majina kadhaa.

Wengine hukitaja kisiwa cha Pemba kama cha marashi ya karafuu, jazzira, makka ndogo majina yote hayo pamoja na mengine yalikinyanyua juu kisiwa hicho.


Leo tukiwa ndani ya miaka 25 tokea wagonjwa wa mwanzo kutambulika kuwa na VVU kwenye hospitali ya Mnazi mmoja Unguja, mwaka 1886, na hatimae kisiwa cha Pemba.

Yote kwa yote, inaingia akili kwamba eti kuja kwa VVU ndio iwe sababu wa wakaazi wa Kisiwa hicho, waachane na mila na desturi zao nzuri wa ukarimu na ubianaadamu na kufikia pahala kuwa wakuu wa unyanyapaa?

Mbona zipo tafiti zilizofanya na Tume ya Ukimwi Zanzibar, zimekuwa zikionyesha kuwa kisiwa hicho miaka 1990, wakaazi wake walikuwa wanaongoza kwa kuwanyanyapaa watu wanaoishi na VVU.

Wengine waliona hilo ni ahuweni, maana unyanyapaa huo ulikuwa kwa watu wenye umri mkubwa na wakati mwengine anaenyanyapaa anaweza kujitetea.

Sasa hili lililopo ni zaidi ya unyama maana wananchi hawa wa kisiwa cha Pemba, wamekuwa midomoni mwa watu wanaoishi na VUU na Ukimwi kwamba sasa unyanyapaa umehamia kwa watoto.

Wapo wazazi na walezi ambao wanaishi na VVU na Ukimwi kisiwani Pemba, wamekuwa wakilalamikia hilo kwamba, sasa jamii ya kisiwani humo imewaacha wao na wa kuwafanyia unyama watoto wao.

“Unyanyapaa anaofanyiwa mwanangu ni jirani zetu na hata wapiti njia hupewa majina mabaya kama vile, msambaazaji umeme, mwenye wali wetu, na hata kumuita muuwaji’’,sasa hii ndio hali ya Pemba alisema Mzazi.

Mzazi huyo ambae alisema alikaa na kuishi na VVU kwa miaka minne bila ya kujitangaaza, alihofia sana unyanyapaa ndani ya jamii ya kijiji cha Wawi anapoishi, ingawa baadae aliamua.

“Mimi nilijitangaaza mara baada ya kufariki mumewangu mwaka 2011, lakini adha na kebehi ya wapemba ilinifika, maana nilisusiwa kila kitu’’,alinikumbusha.

Moza Haji Kombo (49) wa Chake Chake, yeye anasema hakukaa muda mrefu alijitangaaza, ingawa unyanyapaa hasa ulimkumba mwanawe hadi sasa.

Mwanangu hana hamu ya kutoka nje, maana hapa mtaani anacheza na watoto hawazidi wanne, waliobakia anasema anawaogopa, maana wamekuwa wakimuita majina mabaya.

Mama huyu anasikitishwa sana na majirani zake, amabo ni wenye umri mkubwa, kwa kubuni majina mabaya na kumuita mwanawe ambapo anasema hilo humkosesha furaha na amani kucheza.

“Watu wazima ambao kukicha wanaingia masikitini na kanisa, wanamuita mwanagu mwenye sumu, anaesubiri kufa, sio mwenzetu au hata kumuita mtu wa Tume’’,alisema kwa kusikitika.

Kaimu Mratibu wa Tume wa Ukimwi Zanzibar ZAC kisiwani Pemba, Ali Mbaroku Omar, yeye anasema linalofanyika nchi nzima la kuwanyanyapaa watoto ni zaidi ya unyama.

Yeye anashangaa kuona watu wenye akili zao timamu, kubuni majina ya mabaya na kuwaita watoto ambao pengine wazazi wao walishakufa kwa Ukimwi au wenyewe wanaishi na VVU.

“Mwenye Ukimwi au Virusi ameshajielewa na ndio maana akapewa majina mabaya, sasa huyu anaemnyanyapaa mwenzake anaahadi gani na Muumba, kwamba atakua salaama daiama’’, alihoji.

Na ndio maana Kaimu Mratibu huyo, anasema wamekuwa wakipokea malalamiko hayo kila muda, kwa watoto kunyanyapaliwa kwa kupewa majina ya kishenzi.

Lakini akasema kila mmoja akilia anashika kichwa chwake, na ndio maana yeye anaona unyanyapaa mkubw ani ule wa kukoseshwa haki zao za msingi.

Makame Juma Hamad wa kijiji cha Msuka wilaya ya Micheweni Pemba, yeye anasema kama sheria ya masuala ya Ukimwi haijaanza kazi vyema, basi kila mtu atakua na nafasi pana ya kuwafanyia unyanyapaa watoto.

“Imekua ni jambo la lazima kwa watoto hata wanaoishi tu nyumba ya mtu mwenye VVU, basi unyanyapaa pia humfika na mtoto ambae hajui lolote”,alifafanua.

Ama kweli mtoto wa mwenzio sasa sio wako, yawaje jirani ambae alitajwa na maandiko matakatifu kuwa ndio ndugu, lakini aanze kwa ubaya.

Maryam Said Abdalla, ambae ameolewa na mwanamme asie na Virusi, anasema hata huyo mtoto wao amekuwa akiipata pata kwa majirani.

Anakiri kuwa hali ya nyanyapaa kwao wenye umri mkubwa sasa 
umepungua, lakikini mashambulizi yamelekezwa kwa watoto wao kwa nguvu.

‘Mimi sasa sinyanyapaliwi tena, maana wameshaniona kama nimekomaa, lakini adhabu wa watoto wetu, ndio kwenye kazi huko’’,alifafanua.

Aliyataja majina ambayo husikia watoto wenye VUU au wazazi wao waliokufa kwa tatizo hilo kama vile, majeneza, mava, wauwaji jambo ambalo huwasononesha sana.

Mtoto (11) ambae pia anaishi na VVU kwa muda huo, mkaazi wa Mtambile wilaya ya Mkoani, ingawa hajapenda kujitangaaza rasmi, anasema aliishi na tatizo kwa muda wa miaka saba bila ya yeye kuelezwa.

“Sasa niko shuleni na nimeleewa kwamba nna tatizo hilo mwaka 2012, ingawa nilishituka, lakini nilikuwa nanyanyapaliwa ikawa sijui nini tatizo’’,alisema.

Yeye anasema na hata baada ya wazazi wake kumuleza, na kuwaeleza marafiki zake, wapo walioachana na yeye hadi leo, na wengine hata kumuita jeneza kutokana na kuwa VVU.

Sheikh Said Ahmad wa Chake Chake, yeye anasema suala la istizai ‘unyanyapaa’ halikubaliki maana humpa mzingira magumu mwenye uongojwa wa aina yoyote.

Yeye anasema muislamu wa kweli aliepata mafunzo ya dini na kuyafuata kwa vitendo, haweza kuwafanyia unyanyapaa watoto na hasa kwa kuwabandika majina mabaya.

“Uislamu haukatazi mtu kuwa na jina la umaarufu, lakini liwe zuri mfano ‘amini’ hafidhi na sio kumuita mtu sumu, au kaburi haya ni makosa’’,alisema.

Yohona Kalagwa ambae ni mchungaji katika kanisa la usharika lililopo Chake Chake, anasema hakuna mtu alieruhisiwa kumuita mwenzake jina analokasirika nalo.

“Mimi sijaona katika bibilia kwamba, eti mtoto aitwe jina tu lolote, basi lazima apewe jina lenye maana na tija na sio la kupotosha au kubeza’’,alisema.

Mratibu wa Jumuia ya watu wanaoishi na VVU Pemba ZAPHA+ Mmanga Seif Massoud, anasema idadi ya watoto 62 walionao kwenye jumuia kwa Pemba ni ndogo na shaka yake ni unyanyapaa.

“Ingawa juhudi tumeshazifanya sisi kwa kushirikiana na Tume ya Ukimwi, lakini wapo wachache hawataki kubadili tabia na huwanyanyapaa watoto’’,alifafanua.

Mmanga, yeye anaona sasa suala la watoto wenye VVU kupewa majina ya ajabu limepungua, maana kabla ya kutoa elimu walikuwa wanapokea kesi moja kila mwezi, lakini sasa ni miezi mitatu hawajapokea.

Aliyataja majina ambayo huitwa watoto hao kama vile’maukimwi, wasambaazaji, wenye sumu, lakini akasema kwa sasa hali inaridhisa kidogo.

Kwa upande wa Zanzibar tayari ipo sheria ya masuala la Ukimwi na ikikataza suala la kumnyanyapaa mtu kwenye Ukiwmi au Virusi kwa njia yoyote, ile na wakati wowote itaanza kufanya kazi.

Ingawa kwa Tanzania bara yenyewe ipo, na ndio maana kifungu cha 32 cha Sheria ya Kudhibiti Ukimwi namba 28/2008 kupiga marufuku unyanyapaa, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).

  Kutokana na hali hiyo, jamii ya wenye VVU imedai imekuwa ikilazimika kukubaliana na unyanyapaa unaofanywa na baadhi ya watu, ili kulinda CD4 zisipunguwe mwilini.

  Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waviu Washauri kutoka wilaya sita za Mkoa wa Simiyu, waliotembelea Kituo cha Matunzo na Tiba (CTC) cha Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.

Shija Mashimba, Mviu Mshauri wa hospitali hiyo, anadai kuwa tatizo la unyanyapaa kwa watu wenye VVU ni kubwa, na njia pekee ya kukomesha hali hiyo ni kukubaliana na matakwa ya jamii ili kutunza kinga za mwili (CD4).

Happiness Malamala, mkazi wa Bariadi mjini ambaye anaishi na VVU na Mviu Mshauri, alidai Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu inavyo vituo vitatu vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo kwa wenye VVU, ambako hadi kufikia Julai 2014 idadi ya wateja waliopotea walikuwa 875.

Anafafanua kuwa kati ya hao 769 walikwishaanzishiwa dawa za ARV huku 106 wakiwa hawajaanzishiwa dawa hizo, ambapo katika kipindi cha Julai 2014 hadi Machi 2015 idadi ya wateja waliofuatiliwa ni 319 ambapo kati yao 272 wanatumia dawa za ARV huku 47 wakiwa hawajaanza kutumia dawa hizo.

Mtandao wa Kanda ya Afrika Mashariki ya Mashirika yanayotoa Huduma za Ukimwi, umekiri kuwa  kundi kubwa la watoto wanakabiliwa na unyanyapaa na ubaguzi na hakuna sheria wala sera za kuwalinda katika kanda.

 Mtando huo ulisema kuna ripoti za walimu wakuu wanaokataa wanafunzi ambao wana VVU huku wakikabiliwa na unyanyapaa, na kukataa shule.


Nchi za EAC zimetia saini mikataba kadhaa ya kimataifa kuhusu ubaguzi wa VVU/UKIMWI ikiwa ni pamoja na Azimio la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Haki za Watoto, katika ngazi ya kanda, nchi pia zina vifungu kuhusu haki za watoto. 

Hata hivyo, mapengo ya haki za binadamu kuhusiana na watoto na VVU bado yapo, ikiwa ni pamoja na haki ya kulindwa kutokana na ubaguzi.


Suala la unyanyapaa limekuwa likitajwa na wanaharakati wa masuala ya kupambana na Ukimwi, kwamba yanaweza kuwa kizingiti cha kupunguza maambukizi mapya ya VUU.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.