Habari za Punde

Makala ya Kilimo Hai (ORGANIC FARMING)

Na Pili Khatib na Zuhura Omar, MUM
Uhai ni maisha na maisha ni uhai ili kuwa na uhai tunahitaji chakula na chakula bora ni chakula kinachotokana na kilimo hai, kilimo hai ni kilimo kilicho bora zaidi. Je unakifahamu kilimo hai?
Kilimo hai au organic farming ni aina ya kilimo kinachozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Kilimo hicho kinatumia mbolea na madawa yasiyotengenezwa viwandani na kinazingatia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya manufaa kwa jamii, kiuchumi na kiafya.
Tumeirithi ardhi kutoka kwa vizazi vilivyotangulia ikiwa na ubora wa asili, lakini kutokana na matumizi ya muda mrefu, ardhi huzeeka na kushindwa kutoa mazao bora, hivyo kumfanya binadamu kutafuta namna nyingine ya kuifanya ardhi hiyo itoe mazao mengi.

Baada ya kuona ardhi imechoka Wakulima wengi huamua kutafuta maeneo mengine yaliyo bora na kuanza kuyatumia. Wakati mwingine hulazimika kufyeka misitu ili kupata mashamba mapya, hali ambayo siyo tu inaharibu mazingira, lakini pia inaweza kututia umaskini wa milele kwa sababu ardhi iliyoachwa awali huwa haitafutiwi njia muafaka ya kuifanya irejee kwenye ubora wake.
Wakulima wengine hutafuta mbolea, hasa za chumvi chumvi, na kuzitumia katika ardhi ile inayoonekana kuzeeka. Lakini matatizo mengi huibuka kutokana na matumizi ya mbolea pamoja na madawa ya kemikali kwenye kilimo.
Mbolea hizo zina kemikali na madawa ya kuua wadudu yana madhara yake kwani yana sumu isiyoonekana. Sumu hiyo tunakula au tunakunywa na ndizo zinazoleta madhara kwa binadamu na udongo.
Mazao yanayotokana na kilimo cha mbolea za kemikali yanaleta athari kubwa zisizoonekana kwa binadamu na hata wanyama. Lakini jambo la kuzingatia kwa sasa, kila mtu anatakiwa kuvuta kumbukumbu zake kulingana na umri alioishi na kuangalia yafuatayo: Hali ya udongo enzi zile na sasa ikoje? Kiwango cha maradhi wakati ule na sasa kikoje? Uwezo wa udongo kuzalisha mazao umepungua au unazidi mwaka hadi mwaka.
Inaonyesha kuwa mbolea za chumvichumvi zimechakaza udongo na hivyo kufanya uzalishaji upungue. Hata mazao yanayotokana na matumizi ya mbolea hizo yamekosa ubora wa asili unaotakiwa.
Hali hiyo inatia shaka kama umaskini wa Mkulima utakwisha ikiwa hatabadili aina ya pembejeo kuokoa ardhi yake isizidi kuchakaa na wakati huo huo kupunguza sumu isiyoonekana kwenye udongo na vyanzo vya maji.
Ni ukweli usiopingika kwamba, mbolea za chumvi chumvi zikiisha muda wake hugeuka sumu na baadaye Mkulima analazimika kutumia gharama kubwa kuweka mbolea za mboji ili kurudisha udongo katika hali nzuri. Sumu hii isiyoonekana inaharibu udongo, vyanzo vya maji na hata mwili wa binadamu wanaotumia vyakula hivyo.
Katika Mataifa yaliyoendelea, mbolea za chumvi chumvi zinatumika kupandia na kukuzia miti, hasa ya mbao. Vile vile inatumika kutengenezea mazingira kwa maeneo ambayo hayatumiki kuzalisha mazao ya chakula cha binadamu.
Wao wamekuwa wakipiga sana vita vyakula vilivyolimwa kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi na ndiyo maana hivi sasa katika soko la dunia bidhaa zilizozalishwa kwa kutumia mbolea hizo za chumvi chumvi zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya chini kuliko zile zinazolimwa kwa kutumia kilimo hai.
Sasa tujiulize, kwa nini sisi tunaendelea kutumia mbolea hizo zinazoua udongo wetu na kuweka sumu? Hivi hakuna mbolea nyingine mbadala? Jibu ni kwamba, mbolea mbadala zipo.
Mbolea mbadala ni zile zinazotokana na marejea na uozo wa asili, uozo wa asili unaotokana na majani mbalimbali, samadi ya mifugo asili, mabaki ya nafaka au mazao mbalimbali (kama maganda na mabua ya mahindi na mpunga).
Mbolea hizi zinaweza kupatikana au kutengenezwa katika mazao tunayolima, kwenye mazingira tunayoishi. Mbolea hizi zinasaidia kurudisha udongo katika hali ya rutuba na asili yake na gharama za mbolea hizi ni nafuu kabisa na zinadumu ardhini kwa muda mrefu.
Mazao yatokanayo na kilimo cha mbolea za kemikali hayana bei kubwa katika soko la dunia ikilinganishwa na mazao yatokanayo na kilimo hai, ambacho kwa sasa ndicho kinachohamasishwa ulimwenguni kwa sababu kinatumia viuatilifu asilia ambavyo siyo tu vinaongeza tija ya mazao, lakini pia ni rafiki wa mazingira.
Kwa mfano, wastani wa bei ya karafuu ya kilimo hai ni TZS 170,000 kwa kilo ambayo niasilimia ya bei ya karafuu isiyo ya kilimo hai kutoka Shirika la ZSTC.
Ili bidhaa zikubalike katika Soko la Kimataifa kuwa zimezalishwa kwa kutumia mbinu za kilimo hai, zinapaswa kwanza kupitishwa na Taasisi zinazosimamia ubora wa bidhaa hizo.
Wazalishaji wa mazao ya kilimo hai huwa hawachanganyi mazao ya kilimo hai na yale ya kawaida, hivyo hutumia  kanuni za kilimo hai katika kusindika mazao katika mfumo huo wa kilimo hai.
Kilimo hai Tanzania kilianza kupata umaarufu katika miaka ya 1990 baada ya Serikali kuruhusu Taasisi kadhaa za Serikali na zisizo za Kiserikali (NGOs) kueneza elimu na teknolojia za kilimo hai kwa Wakulima nchini.
Kwa upande wa Zanzibar Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ZSTC limeanzisha na kuendeleza mradi wa mazo ya kilimo hai ambapo kwa hatua ya awali Shirika limeanza na mazao manne (4) ya viungo ambayo ni Karafuu, Pilipili manga, Mdalasini na Pilipili hoho.
Hii ni habari njema kwa Wakulima wa Zanzibar kwani mazao ya kilimo hai  yanafaida kubwa kwa Afya ya mtumiaji na yana bei nzuri hasa katika soko la nje hivyo ni vyema Wakulima wakachangamkia kilimo hicho  kwa ajili ya kuongeza kipato na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika hilo la Biashara Zanzibar Mwanahija Almas Ali mpango wa kilimo hai ni Mradi maalumu wenye lengo la kuwaongezea kipato Wakulima Nchini.
Hivyo Shirika la ZSTC limeunga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza kilimo hai kwani ambapo linaitoa elimu kwa Wakulima na Wasindikaji wa mazao ya kilimo hai ya Karafuu, Pilipili manga, Pilipili hoho na Mdalasini.
Kanuni ni maelekezo ya utekelezaji wa mambo ili yaende sawa kama yanavyotakiwa na kanuni hufuatwa kwa ajili ya kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kilimo hai kina kanuni zake ambazo kila Mkulima anawajibu wa kuzifahanu na kuzifuata.
Kanuni hizo ni kanuni za Afya, mazingira, kuhifadhi udongo, haki na usawa na kanuni ya uangalizi ambazo zote hizo ni muhimu katika kuweka uwazi katika mfumo wa kilimo hai.
Ni lazima kuzingatia kanuni hizo za  kilimo hai katika kulinda ubora wa mazao ya kilimo hai ya Karafuu, Mdalasini, Pilipili hoho na Pilipili manga kuanzia kuyapokea kutoka kwa Mkulima hadi yanachambuliwa na hatimaye kuhifhadhiwa na kusafirishwa kuelekea sokoni.
Miongoni mwa kanuni hizo ni kuwepo na orodha ya Wakulima waliopasishwa kwa kilimo hai katika msimu husika na kuwepo kwa orodha ya Wakulima walioruhusiwa kuuza mazao ya kilimo hai ambapo wamepasishwa baada ya ukaguzi wa nje.
Kanuni nyengine ni kuwepo taarifa ya kiasi kinachohitajika kupokelewa na kilichokuwepo. Kuwepo kwa orodha ya Wakulima waliouza mazao ambayo yanapokewa kwa hati za kusafirishia mazao hayo.
Wakati wa kupokea mazao kutoka kwa Wakulima wa kilimo hai lazima kuzingatia uwepo wa usahihi wa nyaraka na kumbukumbu hizo za kila Mkulima wa kilimo hai.
Katika ufungashaji, mazao ya kilimo hai hufungashwa kwa vifungashio maalum vinavyokubalika kitaalumu na inatakiwa iwekwe nembo maalumu ya kilimo hai ili bidhaa itoa utambulisho.
Kanuni hizo na nyengine zote za kilimo hai zinazingatia urutubishaji wa udongo, mimea, wanyama na uzalishaji wa chakula chenye ubora na usalama wa hali ya juu kwa binadamu, hivyo   ulimaji, uvunaji, uhifadhi, usafirishaji na usambazaji unahitaji uangalifu wa hali ya juu.
Pamoja na uzuri na faida wa kilimo hai, uzalishaji wake unakabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo ukilinganisha na mahitaji hasa katika soko la nje.
Wakulima wengi wanakosa uwezo wa kuzalisha kwa wingi kutokana na kukosa mahitaji ya msingi katika uzalishaji wa kilimo hicho hasa mbolea isiyokuwa na kemikali.
Ni jukumu la Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwasaidia Wakulima wa kilimo hicho kwa kuwapatia pembejeo ili waweze kuzalisha kwa wingi kukidhi mahitaji ya soko hasa soko la nje ambapo itachangia kukuza kipato chao na Taifa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.