Habari za Punde

WAWEKEZAJI KATIKA MIGODI TANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WAKAZI WAISHIO MAENEO HAYO ILI KUPUNGUZA MIGOGORO.

Baadhi ya Washiriki wa Mdahalao huo wakifuatilia mada iliyokuwa ikijadiliwa wakati wa mdahalo.

Nchi mbalimbali duniani zimekuwa na sera mahususi kwa ajili ya kukaribisha wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza kwenye nchi zao ili kuweza kupata kipato kupitia kodi mbalimbali na faida nyingine kama ajira kwa wenyeji, uboreshwaji wa miundo mbinu n.k. Moja ya nchi hizoni pamoja naTanzania. 

Tanzania ilibadilisha sera zake za kiuchumi mwanzoni mwa miaka ya 1990, kwa kutoa fursa kwa sekta binafsi kuweza kumiliki uchumi. Sera hii ilivutia wawekezaji wengi toka nje na ndani kuwekeza katika sekta mbalimbali, moja ya maeneo ambayo wakezaji wamejikita ni sekta ya madini. 

Shinyanga ni moja kati ya mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini nchini na hivyo kuvutia wawekezaji wakubwa katika sekta hiyo. Mfano mzuri ni kampuni ya Barrick inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani humo.

Mgodi huo unazungukwa na vijiji vitatu ambavyo ni Mwendakulima, Mwime na Chapurwa.  Lakini kutokana na hali halisi kumekuwa na kelele nyingi za manung’uniko toka kwa jamii zinazoishi karibu na maeneo hayo kuachwa bila maendeleo yoyote wakati wageni wanachukua madini kwa kiwango ambacho hakijulikani.

“Kitu kingine uwepo uwazi waweke uwazi katika haya masuala ya madini mapato wamepata kiasi gani wawekezaji na serikali yenyewe imepata kiasi gani, ikibidi hata kwa wale wananchi wanaozunguka mgodi huu au migodi mingine ya Tanzania. Waweze kuwa  wanawabandikia kwamba mwezi huu mgodi umeingiza kipato hiki na serikali imepata hiki angalau kidogo inaweza kupunguza manung’uniko. Kwa watanzania wengine ambao wanaishi sehemu ambapo hapana madini wapeleke hata kwenye magazeti matangazo ya mapato,” anafafanua mkazi wa Mwime.


Haya yamejiri kwenye mda- halo uliondaliwa na waraghabishi wa Chukua Hatua toka kijiji cha Mwime. Ambapo wananchi walipata fursa yakuchangia mawazo kama madini ni laana ama neema. 

Katika mdahalo huo ambao ulifanyika katika shule ya sekondari ya Mwendakulima washiriki toka kada mbalimbali za kijamii Kama wachungaji, mashekhe, wakulima, walimu, watendaji wa vijiji, wanafunzi na waandishi wa habari walipatafursa ya kuchangia mawazo yao kama madini ni laana ama neema. Mwanafunzi wa kike toka katika shule ya sekondari ya Mwendakulima yeye aliona kwamba madini yanaweza yakawa ni janga la mazingira pale aliposema kwamba,

 “Suluhisho jingine angalau wangebadilisha mfumo wa uchimbaji, kwa sababu mfumo wanaotumia ule yaani kadri siku zinavyokuja kutakuwa na janga kubwa sana, angalia udongo uliofika pale huku chini kuna nini.” 

 Ukiacha changamoto ya mazingira, suala jingine lililojitokeza ni athari zinazoletwa na kemikali mbalimbali ambapo mwalimu mraghabishi

Paul Chui wa shule ya msingi Mwime alisema,  “Kwa kweli kutokana na sera  ya elimu, bado tunafundisha elimu kwa kuzingatia sera ya elimu. Hivyo kwa mimi kama mwalimu najitahidi sana kuwaelekeza wanafunzi kuhusu suala zima la athari za kemikali kama vile sunlight pamoja na mekyuri.” 

 Wakati washirki wengine waliojitokeza wao walielezea tatizo la kiungozi na mikataba mibaya. Katika kuelezea tatizo hilo walielezea usiri uliopo kwenye mikatabana hivyo kushauri wananchi kuhusisha siasa na mali zao  kwa kuhakikisha kwamba wakati wa kupiga kura ni wakati sahihi wa kudhibiti maliasili za umma kwa kuchagua viongozi wanaofaa. 

 Mapungufu katika sera pamoja na sheria za madini ni moja ya sababu zilizotajwa kufanya  madini yaonekane laana kwa wananchi wanaozunguka migodi hiyo.

Katika maelezo yake kwa washiriki, George Kingi ambaye ni mtendaji wa kijiji cha Mwime alisema, “Kuna mapungufu kwenye sheria zetu hata ungemweka leo mwingine hata kila siku kama sheria  hujaiboreshwa bado unarudi kulekule kwa hiyo suala la sheria lifanyiwe marekebisho. 

Kingine ni sera.  Sera kama haisemi Mwime waachiwe  asilimia fulani, hata ungemleta mwingine kesho na mwingine atakwamishwa na sera ambayo haisemi wanamwendakulima mbaki na nini.”  Katika hili ushauri uliotolewa ni wa kukaa vikao wananchi wanatakiwa kutoogopa na wanapokaa kwenye vikao kweli wasema.

Kwa kuwa kama kuna watu wa kupiga  kelele kule juu sheria na sera zibadilishwe na zikabadilishwa basi kila kitu kitakuwa sawa. Kama anavyomalizia George,

“Ukishabadilisha sheria na sera hata maji Mwime unayapata hata gari unaletewa si sera inasema uletewe gari kama sera haisemiutaletewa gari?”

Akitoa majumuisho ya mdahalo huo uliondaliwa na waraghabishi walimu na wakulima Toka kijiji cha Mwime, mwenyekiti Maimuna Said alisema

“Madini sio laana lakini viongozi wenyewe ni laana kwa sababu hawatendi haki ipasavyo kulingana na katiba ya jamhuri wa muungano wa Tanzania. Hii ni neema toka kwa Mungu.”

Suala jingine ambalo limejitokeza katika mdahalo huo ni wananchi kutokuwa na furaha jinsi ambavyo serikali haiwashirikishi katika  kufanya maamuzi muhimu yanayohusu mustakabali wa maeneo yao.

Hivyo ili madini yasiwe laana ni muhimu sana kwa serikali kuwashirikisha wananch toka hatua za mwanzo.

Lakini pia suala zima la kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.  “Kuna haja kubwa ya kutolewa elimu hususani elimu ya uraia. Watu kwanza watambue haki zao, mtu akishatambua haki zake kuna kuwa na uwezekano wa yeye kuzidai, lakini kama watu bado hawatapata elimu hiyo ni kwamba watu watakuwa wananung’unika tu pembeni. Lakni hajui aanzie wapi na hajui aishie wapi,” anafafanua Maalim Daudi Athman Imamu wa Masjid Noor Nyandekwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.