Habari za Punde

Amani kwanza kisha uchaguzi wa marudio


 Na Haji Nassor, Pemba      

OKTOBA 28, mwaka 2015 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, Jecha Salim Jecha, alitangaaza rasmi kuyafuta matokeo ya uchaguzi mkuu ngazi ya udiwani, uwakilishi na urais wa Zanzibar.

Kila mmoja ni shahidi wa hili, na wala sina nia ya kukumbushia pakubwa, maana wapo waliofurahia wakiwa na sababu kadhaa, lakini pia wengine walinuna nao wakiwa na sababu tunasema zenye akili.

Yote kwa yote ndio tumeshashuhudia kwamba matokeo hayo yamefutwa, na mfutaji akiwa na sababu kadhaa, ikiwemo uchaguzi huo kutawaliwa na ghilba.

Kisha ufutaji huo ukasindikizwa kisheria zaidi kwa taarifa hiyo, kuingizwa kwenye gazeti rasmi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wengine kufikiria kwamba ni Gazeti la Zanzibar leo, kumbe silo hili ni maalum hilo.

Niende mbele kwanini uchaguzi ulifutwa……hapana kila mmoja anaelewa sababu kadhaa, na kisha Mwenyekiti wa ZEC Jecha Salim Jecha, kutangaza kwamba uchaguzi huo, utarejewa na vyama kuingia tena dimbani.

Wala sio siri…. na wala sioni aibu kusema kuwa Chama kikuu cha upinzani Zanzibar CUF walishatangaaza mara kwa mara na kwa hati nyeusi kwamba, wao hawafahumu kufutwa huko na wala hawana habari na uchaguzi wa marejeo.

Huku chama kinachotetea kiti chake cha urais cha CCM, kikitofautiana maana, kwanza kikikubaliana na ufutwaji huo, na kisha kimeshajipanga ili kuingia tena kwenye marejeo ya uchaguzi huo.


Na hii ndio demokrasia, kwamba mmoja akisema hii nguo ni nyeusi, basi atokea mwengine aseme sio  nyeusi, bali ina rangi tu nyeusi, lakini wote wanasema hayo sio kwa utashi bali kwa nguvu ya hoja tena nzito.

Kama ZEC ilishatangaaza kwamba kuna uhakika wa kurejea kwa uchaguzi Machi 20 mwaka huu, akina mimi na yule tumekuwa tukisema kila mara kwamba, lazima amani na utulivu katika uchaguzi huo, itawale.

Walishasema wazee kwamba ‘hakuna harusi ndogo wala isio na gharama, basi tusema kwa pamoja kwamba, na lolote kwenye uchaguzi laweza kujichomoza.

Wiki tatu kabla ya uchaguzi wa mwanzo Oktoba 25 mwaka 2015, viongozi wa dini zote unazozijua wewe, makabila, vyama vya siasa, wanawake, vijana na mashirika kadhaa yalismama na kuomba amani na utulivu hadi nykati za usiku.

Sasa tumekwama wapi kwa uchaguzi huu ambao vyombo vyenye mamlaka vinasimama na kusema utarejewa, kisha tukose kujiombea amani?

Nakumbuka sana mikutano yote ya kampeni iliofanywa kabla ya kuhitimishwa pale 0ktoba 24 mwaka 2015, hakuna kiongozi wa chama cha siasa, ambae hakuna neneo amani na utulivu kwenye hutuba yake.

Kumbe kila mmoja aliona umuhimu wa kudumisha na kuendelea amani na utulivu, tena kabla, wakati na baada ya uchgauzi, tukiamini kuwa kumbe bila ya vitu hivyo hakuna linalofanyika.

Mgombea urais wa chama cha CUF maalim Seif Sharif Hamad kwenye mkutano wake wa kampeni alioufanya kijiji cha Mtambwe, alisisitiza umuhimu wa amani na utulivu wakati wote.

“Ndugu wananchi nasema Jeshi la Polisi sasa limeshatufahamu sisi CUF nini lengo letu, sasa lazima tuhakikishe tunatunza amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu’’,alisema.

Kwani alikuwa yeye tu….. hata Mgombea wa nafasi kama hiyo kutoka AFP Said Soud Said, yeye alisema lazima kila mmoja neno amani na utulivu liwe mbele kisha ndio chama.

Alikwenda mbali zaidi kwamba, hakuna umuhimu wa uwepo wa chama chochote Zanzibar, kwamba hakitozingatia amani kwa wananchi, maana urais, umakamu na uwaziri hautafanyika kama amani haitotawala.

Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akimuombea kura mgombea wa chama hicho Dk Ali Mohamed Shein, kwenye mkutano uliofanyika Kiwani, alisema chama hicho hakijapanga vijana kufanya fujo.

“CCM ni mwalimu wa demokrasia, CCM ndio chama mama, hakina haja ya kuvunja amani, maana chenyewe kinatetea amani na utulivu’’,alisisitiza.

Sasa iwe wewe unaeshiriki au uko kando kwenye uchaguzi wa marejeo, ni vyema suala la amani na utulivu likapewa kipaumbe na cha pekee, maana hakuna asietaka utulivu.

Kama vyombo vyenye mamlaka vimeshasema uchaguzi unarejewa mbona hatuoni shamra shamra za hutuba za viongozi wa dini na vyama vya siasa kusimama kidedea juu ya kuhimiza amani.

Juzi kwenye kongamano la kuelekea uchaguzi wa marejeo lililofanyika ukumbi wa wizara ya habari mjini Zanzibar, mhariri mtendaji wa shirika la magaezti ya Serikali Nasim Haji Chumu, alishasema kuwa suala la amani na utulivu ndio jambo la pekee.

“Tayari tume ya uchaguzi imeshatangaza tarehe 20 mwezi Machi mwaka huu ndio uchaguzi wa marejeo, lazima waandishi wawe makini na habari zao wakizingatia amani na utulivu’’,alisema.

Lakini hata Mkurugenzi mtendaji wa ZBC Hassan Abdalla Mitawi, alisema lazima wananchi wasome kutoka nchi za Burundi na Kenya kutokana na machafuko yalioko.

“Mimi nadhani amani na utulivu ndio iwe ajenda yetu kwa waandishi na hata makundi mengine ndani ya jamii, maana hakuwezi kufanyika lolote kama vitu hivyo vitatoweka’’,alisfafanua.

Maana hapa narejea tena iwe wewe ni mshiriki wa uchaguzi au wa kukaa kando, lakini je amani na utulivu huna shida navyo tena, naamini jawabu sio, sasa tuipige chapuo.

Kijana Omar Kombo Daudi (22) wa Mkoani, anasema chakuhubiri kwa sasa kama mamlaka zimeshamua kurejea uchaguzi, ni amani na utulivu maana bado wananchi wanahitaji hilo milele.

“Hakuna hata kiongozi mmoja wa dini, chama, au NGOs na wengine asietaka amani na uutulivu, sasa lazima tuone yale maombi kadhaa yaliofanywa yarejewe’’,alifafanua.

Bibi Asha Hassan Makame (50) wa Chakechake, anasema lazima kila mmoja apigie chapuo suala la amani na utulivu, maana  hakuna uchaguzi uliohakikishiwia amani na utulivu kwa asilimia mia moja.

“Inawezekana kuna vyama havitoshiriki uchaguzi wa marejeo, lakini bado vinastahili kuomba amani na utulivu, maana hata wao watakaobakia majumbani wanahitaji amani’’,alisema.

Ingawa Mwanaidi Mbarawa Hija (35) anasema suala la amani na utulivu sio tu kwenye mambo ya kisiasa pekee, bali hata wakati wowote kila mmoja aombe amani na utulivu.

“Unajua suala la amani ni wakati wote, lakini kama kuna shughuli za kisiasa kama uchaguzi, lazima kila kiongozi kwa nafasi yake akemee, maana amani ni kwa sote na machafuko pia’’,aliweka wazi.

Bado upo umuhimu kwa kila mmoja, iwe wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa marejeo au hata katika maisha ya kila siku, suala la amani na utulivu pia ni sehemu ya maisha.

Mshauri wa mambo ya habari kutoka shirika la Internews Valarie Msoka, yeye anasema kitu amani ndio tunu ya taifa, sasa suala la kushiriki ama kutoshiriki katika uchaguzi sio la kuzingati, lakini amani na utulivu ni jambo pekee.

“Mimi nimshashuhudi vita Sudan, Kenya na Burundi sasa ndio maana napigia sana chapuo umuhimu wa amani na utulivu hapa Zanzibar wakati kukiwa na uchaguzi wa marejo’’,alisema.


 Yote kwa yote suala la amani na utulivu, ambalo dini zote inalikubali lazima kwa Zanzibar kuelekea uchgauzi wa marejeo, iwe ndio ajenda kuu, maana athari na faida ni kwa wote.

3 comments:

 1. Wimbo huu hauna tena mvuto mshachelewa waumiani mna kunywa damu za wanyonge ikisha munahubiri amani! Mnazani wazanzibari hawajui nani aliekuwa haitakii mema hii nchi!
  Jecha ana mamlaka gani yakufuta uchaguzi na kwa sheria ipi!
  Mwaka huu mutaondoka au mutawale minazi tumechoka na dhulma kila chenye mwanzo ujuwe kina mwisho

  ReplyDelete
 2. Sheikh kama huna cha kuandika ka kimya! You will be safe and happy!! Hii maada yako labda watoto wa darasa la kwanza ndio wanayo I Ihitaji kwani ni sasa na hadith za paukwa na pakawa! Sahamani but wengi humu naamini we don't need it!!! Samahani sana

  ReplyDelete
 3. Ni jambo la kuzingatia sana amani na utulivu lakini hakuna asijejua kuwa CCM ni wababe na wamekusudia kumwaga damu kwa gharama yoyote ile muhimu nchi iwepo katika milki yao, nashangaa sana kusikia kwamba CCM wanahubiri amani wakati wakiwatawanya kila kona vijana wao almaarufu Mazombi! tena jambo la kuchekesha wao wanasema hawa mazombi hawawajui wanatokea wapi huku mazombi hao wakimiliki silaha za moto na magari ya vikosi vya ulinzi na usalama.
  Mungu atuepushe na vurugu lakini kiukweli Zanzibar kuna kila dalili ya harufu ya damu ya wazanzibari.

  ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.