Habari za Punde

Hujuma, Uchomaji moto Mashamba ya Mikarafuu ni kikwazo kwa Maendeleo ya Sekta ya Karafuu Z’bar


 Baadhi ya Eneo la Ekari Tisa za Mikarafuu lililounguzwa Moto na Watu wasiojuilikana   katika Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba

Ø Sheria ya Maendeleo ya Karafuu itumike kuilinda sekta hiyo

Karafuu ni Zao la Kilimo linalotegemewa  sana na Wakulima wa zao hilo na Wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kwa kukodi mashamba na vibarua wanaoajiriwa kuchuma kwa makubaliano ya kulipwa ujira kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Pia zao la karafuu ni zao kuu la Uchumi wa Zanzibar kutokana na kuingiza fedha nyingi za kigeni ambazo hutumika katika kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, kusambaza umeme, maji safi, miundombinu ya bara bara na huduma nyengine muhimu.

Takwimu zinaonesha kuwa  zao la Karafuu ndilo linalochangia zaidi pato la Taifa kuliko mazao mengine ya biashara, ambapo inakadiriwa kuchangia pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 20.5.

Kutokana na umuhimu wa zao hili, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) linaendesha mpango maalum wa kuongeza idadi ya mikarafuu na kuongeza uzalishaji kwa kuotesha miche 1,000,000 kila mwaka na kuwagaia Wakulima bila ya malipo.

Pamoja na jitihada hizo za Serikali za kuimarisha zao la karafuu kwa maslahi ya Nchi na Wananchi wake lakini tukio la hivi karibuni la watu wasiojuilikana kuchoma moto eka tisa za Mashamba ya Mikarafuu linarudisha nyuma jitihada hizo.

Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea Januari 22/2016 katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba mikarafuu 151 imeungua moto ambapo kati ya hiyo 36 haiwezi kuota tena kutokana na athari hiyo ya moto.


Mikarafuu hiyo iliyoungua ni kutoka katika mashamba matatu tofauti yaliyokuwepo katika sehemu moja ambapo kwa pamoja yana ukubwa wa ekari tisa (9). Tukio hilo limesababisha hasara yenye thamani inayokisiwa kufikia shilingi milioni 24.5.


Imeonyesha kuwa kitendo cha kuchoma moto kwa mashamba hayo ni hujuma za makusudi kutokana na moto huo kutokea katika maeneo tofauti. Kitendo hicho ni kibaya kwa sababu ni hujuma kwa uchumi wa nchi na Wananchi wake.

Ni wazi kuwa kiitendo hicho kimewaumiza sana Wakulima wa mashamba hayo kwa sababu Mkarafuu ni mti unaohitaji huduma kubwa katika ukuaji wake, hata ukifikia hatua ya kuzaa Mkulima huwa kafanya kazi kubwa. Sasa anapotokea mtu mwengine kufanya hujuma huyo ni maumivu makubwa kwa Mkulima.

Mkarafuu mmoja una uwezo wa kuzalisha zaidi ya pishi ishirini kulingana na ukubwa wa mkarafuu wenyewe, kwa bei ya sasa ni zaidi ya shilingi laki nne hivyo mikarafuu 151 iliyoungua moto imesababisha hasara kubwa ya kiuchumi na kimazingira.

Kutokana na umuhimu na thamani ya zao la karafuu kwa uchumi wa Nchi na Wananchi wake Serikali ilipitisha Sheria ya Maendeleo ya Karafuu, Namba 2 ya mwaka 2014 ili kuulinda Mkarafuu na karafuu zenyewe.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo ni kosa kwa mtu yoyote kuchoma moto mikarafuu. Kifungu cha 13(1) (a), kinakataza kuchoma au kutengeneza makaa, kuchimba mawe, udongo au mchanga kuangusha, kung’oa, kukata, kuharibu au kuathiri mikarafuu kwa aina yoyote ile.
Waliofanya tukio hilo la uchomaji moto mashamba ya mikarafuu wajue kuwa wamefanya kosa kwa mujibu wa Sheria ya Maendeleo ya karafuu. Ni vyema Jeshi la Polisi likafanya  uchunguzi wa kina kuwagundua waliofanya tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria.
Miongoni mwa madhumuni ya kuundwa kwa Sheria hiyo ya Maendeleo ya Karafuu ya Mwaka 2014 ni kulinda na kuweka ulinzi imara wa Mikarafuu na Karafuu zenyewe. Kuimarisha, kustawisha, kuthaminisha na kuendeleza zao la karafuu Zanzibar, hivyo kuchoma moto mikarafuu ni kwenda kinyume na Sheria hiyo.

Sheria hiyo pia inapiga marufuku kutumia mkarafuu kwa matumizi ya aina yoyote, iwe kwa ujenzi wa nyumba, kuchonga mbao, kuchonga vinyago au mapambo ya aina yoyote, hivyo Sheria hiyo inatoa ulinzi wa kutosha kwa sekta ya karafuu. Linalotakiwa ni usimamizi wa utekelezaji wa Sheria hiyo.

Hujuma nyengine inayokwaza jitihada za Maendeleo ya Sekta ya Karafuu ni kwa baadhi ya watu kukata matawi na mikarafuu midogo kwa dhamira ya kuiba karafuu kutokana na kuzoeleka kwa uuzaji na ununuzi wa karafuu kwa njia isiyokuwa rasmi ‘vikombe’.

Wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kukatiwa mikarafuu yao hasa wakati wa msimu wa uchumaji jambo ambalo linachangiwa sana na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaonunua karafuu mbichi jambo ambalo ni kosa kwa vile Shirika la ZSTC ndio taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu.

Kwa mujubu wa Sheria hiyo mtu atakaetiwa hatiani kwa kosa la kuuhujumu mkarafuu kwa aina yoyote ni kulipa faini isiyopungua Shilingi Milioni tatu au kifungo kisichopungua miaka mitatu (3) au vyote kwa pamoja kulingana na ukubwa wa kosa.

Shirika la ZSTC, taasisi ambayo ni dhamana ya kuimarisha zao la karafuu kwa kushirikiana na wadau wengine limekuwa likitoa elimu juu ya namna ya kuimarisha zao hilo na thamani yake kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Mwezi Disemba 2011, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein alitia saini Sheria mpya ya ZSTC Na. 11 ya mwaka 2011, inayoipa Mamlaka na uwezo Shirika la ZSTC kulisimamia, kulihudumia, kuliimarisha zao la karafuu na kuhakikisha linakuwa endelevu kwa maslahi ya wakulima, wananchi na Taifa kwa ujumla, kuchoma moto mikarafuu kwa makusudi ni kurejesha nyuma jitihada za uimarishaji wa zao hilo.

Kutokana na uchumi wa Zanzibar kutegemea sana zao la karafuu, Sera ya Serikali juu ya zao la hilo ni kumnufaisha Mkulima zaidi, hivyo Serikali inaendelea na azma yake ya kutekeleza uamuzi wake wa kuwapatia Wakulima bei ya karafuu ya asilimia 80 ya bei ya kuuzia nje ya nchi ili kuwahamasisha Wakulima kuimarisha zaidi zao hilo.

Zao la karafuu ninawanufaisha wengi kutokana na kutoa ajira kwa Wananchi wengi na mzunguko wa fedha unaotokana na biashara ya zao hilo unajenga ustawi wa Wananchi wengi na kuongeza pato la Taifa, hivyo kuichoma kwa makusudi ni kuwakosesha kipato Wananchi wengi.

Pia kuna athari za kimazingira ambapo mikarafuu kama ilivyo miti mengine huwa ni chanzo kikubwa cha mvua. Unapochoma moto mikarafuu unakaribisha jangwa katika eneo hilo na kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa mvua. Kitendo hicho husababisha kukosekana kwa mvua na kupelekea ukame katika maeneo husika.

Moshi mwingi ambao hutolewa baada ya uchomaji wa Mikarafuu huleta athari katika mfumo wa hewa. Pia uwepo wa mikarafuu ni kinga kwa mmongonyoko wa ardhi ambapo katika maeneo ya mabonde ambapo mikarafuu hupandwa husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mmongonyoko wa ardhi.

Wito kwa Wakulima, Wafanyabiashara na Wadau wote wa Zao la Karafuu na wananchi kwa jumla  kutokufanya makosa kama hayo ya uchomaji wa mashamba ya mikarafuu. Kuchoma moto mikarafuu ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika uimarishaji na uendelezaji wa zao hilo.

Ni vyema Wananchi wote wakasaidia katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda mikarafuu yetu na ubora wake ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuifanya Sekta ya karafuu kuendela kuwa tegemeo katika kukuza uchumi na kujenga ustawi wa Wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.