Habari za Punde

Mji Mkongwe kutumia njia moja ( One Way Traffic)

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mjimkongwe Issa Sarboko Makarani akizungumza na waandishi wa habari pichani hawapo juu ya kutumia njia moja ya kuingilia Mjimkongwe kuanzia tarehe 8/2/2016
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam akizungumzia namna Jeshi la Polisi lilivyojipanga kuhakikisha Wananchi wananchi wanafuata sheria zitakazowekwa na Mamlaka ya Mji mkongwe
Mkurugenzi Mipango Miji Dk.Mohammed Juma akijibu maswali kutoka kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano wa kutoa taarifa ya njia moja ya kuingilia Mjimkongwe kuanzia Februari 8 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Aboud Hassan Serenge akielezea mashirikiano waliyonayo na Mamlaka ya Mjimkongwe katika kuimarisha matumizi ya njia ya Mjimkongwe
Mwandishi wa Habari wa Coconut FM Tabia Makame akiuliza maswali kuhusu zoezi zima la utumiaji wa Njia hiyo na namna wananchi watakavyoepuka usumbufu katika Mjimkongwe.Picha na Abdalla Omar Habar-Maelezo Zanzibar.
Mwashungi Tahir    Maelezo. 4-2-2016.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua  kuanzisha utaratibu wa  kutumia njia ya upande mmoja  kubwa ya kuingia Mji Mkongwe kuanzia tarehe nane mwezi huu ili kupunguza usumbufu unaowapata  wageni na watumiaji wengine wa Mji huo.

Akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake Mamlaka ya Mji Mkongwe  Forodhani, Mkurugenzi Mkuu Issa Saidi Makarani amesema uwamuzi huo umefikiwa  kutokana na  ongezeko kubwa la vyombo vya moto linalohatarisha  usalama wa mji huo ambao ni urithi wa kimataifa.

Amesema mji wa Zanzibar umekuwa ukipokea  watalii na wageni  wengi na wakati wa matembezi yao wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kutokana na kuongezeka vyombo hivyo.

Ameongeza kuwa ongezeko hilo la magari  pia limepelekea athari kubwa kwenye majengo kutokana na mtikisiko mkubwa wa magari yenye uzito mkubwa na kubomoa  baadhi ya majengo  ya mji.

“Watumiaji  wa Mji huu na wanaofika kila siku kwa shughuli zao za kimaisha wanapata usumbufu na kubwa zaidi wingi wa vyombo hivyo tayari vimesababisha athari ya baadhi ya majengo,”alisisitiza Mkurugenzi Makarani.

Amesema njia kubwa ya ndani ya kuingilia Mji Mkongwe itaanzia Vuga  kupitia Afrika House , Hoteli ya Serena , Wizara ya Ardhi , Makaazi, Maji na Nishati , Benki ya NBC , Jengo La zamani la Watoto Forodhani , njia ya Mizingani hadi kuishia lango kuu la kuingia bandarini Malindi.

Amezitaja njia zitakazofungwa kuanzia tarehe nane kuwa ni ile inayoanzia jengo la Wizara ya zamani ya Mawasiliano na Uchukuzi kupitia Kiponda na kumalizikia Darajani, njia inayoingia Mkunazini na kumalizikia Skuli ya Sunni Madrassa na njia inyozunguka nyuma ya jengo la sinema ya zamani Majestic.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis amesaema lengo la  kuweka zoezi hilo ni kuweka usalama  kwa wenye magari  na wanaokwenda kwa miguu.

Amewaomba  wananchi kuunga mkono  zoezi hilo ambalo  litaweka mji Mkongwe katika  hadhi  na ubora wake uliopelekea kuwa miongoni mwa Miji ya Urithi wa kimataifa duniani.

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaaa Aboud Hassan Serenge  amewataka wananchi  wanaoishi katika maeneo ya Mji Mkongwe  kubadilika na kuanzisha utamaduni wa kuimarisha  suala la usafi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.