Habari za Punde

Zantel yatoa msaada wa shilingi milioni 10 kwa Maktaba Kuu ya Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu.
Kampuni ya simu ya Zantel leo imetoa shilingi milioni 10 kwa Maktaba Kuu ya Zanzibar kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa vitabu na kusaidia maktaba katika uendeshaji wa shughuli zake pamoja na kurahisisha upatikanaji wa maarifa mtandaoni kwa wakazi wa Zanzibar.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo,Afsa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Benoit Janin alisema msaada huo kwa maktaba ya Zanzibar unalenga katika kusadia kurahisisha upatikanaji wa maarifa miongoni mwa jamii ya Wazanzibar.

Maktaba ni njia pekee na rahisi ya kusaidia upatikanaji wa maarifa miongoni mwa wanajamii bila kujali tofauti zao za kiuchumi’ alisema Benoit.

Maktaba ya Zanzibar, kama sehemu ya majukumu yake, inayo wajibu wa kuhakikisha inatoa huduma bora na zenye ufanisi zinazokidhi mahitaji ya wakazi wanaoishi mijini na vijijini katika kuhakikisha upatikanaji wa taarifa za elimu, habari, utamaduni na burudani.

‘Upatikanaji wa maarifa kwa wanajamii ni jambo la muhimu na suluhisho la changamoto hii ni kuhakikisha tunatoa fursa sawa kwa kuwezesha upatikanaji wa maarifa katika maktaba za jamii’ alisema Benoit.

Kwa upande mwingine, Benoit alibainisha kuwa kama kampuni ya simu inayoongoza Zanzibar, Zantel inaona fahari kushiriki katika kuchangia ukuaji na ustawi wa jamii.

‘Tunamini kwamba kujifunza ni muhimu kwa maendeleo na ndio sababu kampuni ya Zantel inashiriki katika kusaidia kukuza maendeleo ya elimu kama moja ya maeneo ya shughuli zake za kusaidia jamii’ alisema Benoit.

Naye mgeni rasmi wakati wa makabidhiano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Ufundi, Mheshimiwa Abdalla Mzee, aliipongeza kampuni ya Zantel kwa mchango wao katika kukuza maendeleo ya elimu Zanzibar.

‘Tunatoa pongezi na shukurani za dhati kwa kampuni ya simu ya Zantel kwa ajili ya mchango wao katika kukuza maendeleo ya elimu ya Zanzibar, na msaada huu uliotolewa leo kwa maktaba ya Zanzibar utasaidia katika kurahisisha upatakanaji wa vitabu na hivyo kuimarisha mazingira ya utoaji maarifa miongoni mwa wazanzibar’ alisema Mzee.

Mheshimiwa Mzee pia amesema msaada uliotolewa na Zantel utasaidia katika uboreshaji wa maktaba katika Visiwa vya Zanzibar hasa ununuzi wa vitabu pamoja na utafutaji wa maarifa kutoka mtandaoni.


‘Kazi kubwa ya maktaba Zanizibar ni kuhakikisha inatoa huduma kwa lengo la kuongeza ujuzi na maarifa miongoni mwa wazanzibar, na hivyo basi msaada huu kutoka Zantel utaleta msukumo wa utekelezaji wa azma yetu hiyo' alimaliza Mheshimiwa Mzee.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.