Ninawatakia wanawake wenzangu Ulimwenguni kote, Heri ya Siku ya Mwakamke
"Wanawake Tunapashwa Kuona Jinsia yetu kama rasilimali na sio Dhima". ( Women should view their gender as a resource rather than a liability) - MJ
Ningependa kutumia fursa hii kama Dada, Mke, Mama, mfanyakazi, Mwanaharakati na mjasiliamali kuwapongeza wanawake wote kwa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuwaenzi wanawake wote ulimwenguni.
Historia ya Maisha yangu, ni kielelezo cha maisha ya wanawake wengi ulimwenguni wanaopitia changamoto mbalimbali.
Nililelewa katika mazingira kandamizi ya Jinsia ya kike-kwenye jamii ambayo mtoto wa kiume alipewa nafasi ya kipekee katika masuala mbalimbali dhidi ya mtoto wa kike...Kwa mfano kipaumbele cha kupata elimu walipewa watoto wa kiume wakati watoto wa kike wakitarajiwa kushughulika na kazi za nyumbani, kupika,kuchota maji na kusaidia shughuli za kilimo na hatimaye kuolewa.
Bibi yangu (Apumzike kwa Amani) alikuwa mhanga wa mfumo huo kandamizi.
Kwa taabu alizopita Bibi yangu alijiwekea nadhiri kwamba Mjuu wake, hatopitia shida alizopitia yeye...na hivyo siku zote alikuwa akiniasa kwamba "Niyu (jina langu la nyumbani),Unaweza kila kitu kinachofanywa na mtoto wa Kiume". Aliniimarisha kifikra na kiakili.
Na siku zote alikuwa na msemo wake "Niyu Kasome, Ukasome umshinde Babu yako, Usije kuwa unanyanyasika kama sisi"- ushauri wake ndio ulikuwa dira yangu ya maisha ambapo nilisoma kwa bidii na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamili katika masuala ya fedha kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde cha Uingereza.
Hadi hivi leo, sauti ya Bibi haijakoma masikioni mwangu, sijaacha kutafuta elimu na maarifa ya masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo katika jamii...ni kwa sababu hiyo nilipata mafunzo ya muda mfupi ya uongozi na majadiliano kutoka Chuo kikuu cha Harvard cha nchini Marekani.
Nitaendelea kuitafuta Elimu na pia kusaidia wenzangu, sababu naamini moja ya njia ya Mwanamke kujikomboa katika ukandamizaji wa kijinsia ni kuongeza kiwango cha elimu kwake mwenyewe na kwa wanawake wenzake.
Waswahili wana msemo usemao maisha ni shule.....msemo huu nimeuishi katika maisha yangu ya baada ya masomo.
Nimefanya kazi katika mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi. nimefanya kazi na taasisi ya ISHI iliyokuwa inashughulikia masuala ya Ukimwi, baada ya hapo nimefanya pia katika kampuni ya Philips Medical Systems ya Uholanzi na baadaye nimefanya kazi kampuni ya mawasiliano ya Maktech.
Kwote nilipopita nimekumbana na changamoto mbalimbali zilizohusiana na jinsia yangu. Utekelezaji wa majukumu yangu ulinilazimu kuwa na mikutano na watu mbalimbali Serikalini na kwenye taasisi za fedha ambapo watu niliokuwa nakutana nao ni wanaume ambao baadhi yao wamekuwa na mawazo ya mfumo dume yaliyojaa dharau na manyanyaso.
Wengine kwenye fikra zao wanadhani mwanamke yeyote mwenye mafanikio, iwe kwenye biashara, siasa, ajira, lazima anabebwa na wanaume. Wakiona mwanamke amefanikiwa tu, utasikia..huyu 'hawala wa fulani'. hii ni dhana potofu na inayolenga kumdhalilisha na kumnyanyasa mwanamke.
Mimi binafsi sikukubali kuyumbishwa na watu wenye mawazo ya aina hiyo. Kila nilipokumbana na changamoto za aina hiyo nilipata hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuwadhihirishia kwamba NINAWEZA, ilee sauti ya bibi ndio ilikuwa ikinitia hamasa zaidi na zaidi na hatimaye kuniwezesha kufanya vizuri hadi kufikia kuaminiwa kupewa majukumu makubwa zaidi kama vile Mkurugenzi Mkuu katika kampuni ya Mokasi Medical Systems ambayo ni wakala wa kampuni ya Philips ya Uholanzi.
Hasama hiyo iliniwezesha pia kuanzisha kampuni yangu inayotoa Huduma za kifedha - Monfinance Investment Group Ltd. Mbali na shughuli hizo nimeweza pia kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya FINCA Microfinance Tanzania.
Kwa ujumla siku zote za maisha yangu nimejihusisha na harakati za kupigania haki za wenye shida na mahitaji katika jamii kutokana na msingi niliojengewa na bibi yangu wa kukataa unyonge na kusaidia wanyonge.
Hulka hiyo ndio ilipelekea ajira yangu ya kwanza kuwa kwenye taasisi ya uhamasishaji wa masuala ya ukimwi ya ISHI. Niliguswa kujihusisha na kampeni hizo kwasababu binafsi nimepoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ugonjwa huo.
Mbali na ISHI,nimekuwa nikijihusisha na kampeni ya kuzuia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) iitwayo IMETOSHA. Ni jambo la udhalilishaji uliopitiliza kuwakata binadamu wenzetu viongo vyao kwa imani za kishirikina.
Pia nimeshiriki kwenye uhamasishaji wa magonjwa yasiyojulikana (Rare diseases).
Tunaposherehekea siku ya Mwanamke duniani rai yangu kwa wanawake wenzangu, tushirikiane, tusaidiane, tupeane moyo na tuwezeshana ili tufikie lengo letu la usawa 50/50 kufikia mwaka 2030.
Kila mwanamke atimize wajibu wake kwa kujitambua na kuhakikisha haki yake hainyongwi.
Mimi nimejitambua, ninasimamia haki yangu, na wala siipiganii, ni yangu, Jinsia yangu hainitofautishi kiutendaji na jinsia ya kiume.
Ninachoangalia ni Mchango wangu katika maendeleo ya Uchumi, jamii na familia na sio Jinsia yangu.
Ninachotambua katika jinsia yangu ni kuwa mimi ni Dada, Mama, rafiki, na Mke. Mengine yote,nipo sawa na wote, wanaume na wanawake.
Happy Women's Day 2016.
No comments:
Post a Comment