Habari za Punde

Spika mpya BLW ala kiapo na aahidi uadilifu na umakini mkubwa ili kupata ufanisi

Na Ali Issa Maelezo Zanzibar 

Spika mpya wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid amesema kuwa atakiongoza  chombo hicho, ambacho ni muhimili wa tatu wa Dola, kwa uadilifu na umakini mkubwa ili kuona  wajumbe wanafanyakazi ya kuwatumikia wananchi majimboni na kuisaidia Serikali katika kuleta maendeleo.

Hayo ameyasema leo huko Baraza la Wawakilishi mara baada ya kula kiapo cha nafasi  ya Spika kufuatia  kuchaguliwa kwa kura zote za wajumbe 76 waliokuwepo barazani hapo.

Amesema kazi hiyo ataifanya kwa kufuata Katiba ya Zanzibar, sheria na kanuni  zinazoongoza  Baraza la Wakilishi.

“Nitakitumikia chombo hichi  kwa uadilifu na kufuata sheria na taratibu zote za baraza ili kuhakikisha kinapata ufanisi katika utekelezaji wa kazi zake”, alisema Zubeir.


Aidha Spika huyo aliwataka Wakilishi kuwatumikia wananchi wao Majimboni bila ya kuangalia itikadi zao za kisiasa ili kuharakisha maendeleo yao na Taifa kwa jumla.

Spika huyo aliwashukuru wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kumchagua kwa kura nyingi na kusema kuwa ni wazi amekubalika,hivyo atakuwa msikivu na muadilifu katika kusimamia zake.

Nae mwakilishi wa jimbo la Chumbuni Miraji Khamis Mussa alisema kuwa atafanya kazi ya kuwatumikia wananchi wake jimboni bila ya mitazamo  ya kisiasa ,na kusema kuwa wananchi wote katika jimbo hilo ni wake na watafanyakazi pamoja

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.