Mkurugenzi wa Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Nd. Mohammed Suleiman Khatib akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi changamoto zinazokabili uendelezaji wa miundombinu ya uimarishaji wa Kiwanda hicho hapo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alifanya ziara hiyo fupi ili kujionea harakati za kukamilisha Awamu ya Pili ya uimarishaji wa Kiwanda cha Uchapaji Maruhubi uliopata ufadhili kutoka Serikali ya Oman kwa gharama ya Shilingi Bilioni 12.5.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Kiwanda cha upigaji chapa na Mpiga chapa Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba kazi ya kukamilisha miundo mbinu ya uwekaji Umeme pamoja na majengo kwa ajili ya ufungaji mashine kubwa za Kiwanda hicho inamalizika katika kipindi kifupi.
Alisema kudorora kwa kazi hizo kunakotokana na upatikanaji finyu wa fedha za kuwalipa wakandarasi wa ujenzi wa miundo mbinu hiyo ikiwa ni muendelezo wa ukamilishaji awamu ya Pili ya Mradi Mkubwa wa uimarishaji wa Kiwanda cha Uchapaji lazima upatiwe ufumbuzi wa haraka.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua ujenzi wa Miundombinu hiyo ambao umesimama kutokana na ukosefu wa fedha hapo katika Majengo ya Kiwanda cha Uchapaji Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif aliutaka Uongozi wa Taasisi hizo mbili kuhakikisha kwamba lile agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alilolitoa mapema mwaka huu la kutaka machapisho yote ya vitabu vya Bajeti ya Mwaka huu yanafanyika katika kiwanda hicho cha Serikali.
Alisisitiza kwamba Mradi huo mkubwa wa Serikali wa awamu ya Pili ya uimarishaji miundombinu ya Kiwanda hicho uliopata ufadhili kwa kuungwa mkono na Mataifa rafiki na Zanzibar lazima ukamilike kwa wakati uliopangwa ili utoe huduma zilizolengwa.
“ Huu ni mradi mkubwa wa Serikali uliopata baraka ya kusaidiwa nguvu za vifaa na wenzetu wa Mataifa rafiki tena kwa gharama kubwa ya fedha lazima ukamilike kwa wakati uliopangwa kama alivyoagiza Kiongozi wetu wa Nchi ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutanabahisha Uongozi wa Kiwanda cha Uchapaji na Mpiga Chaka Mkuu wa Serikali kwamba atatembelea tena kuangalia ukamilishaji wa ujenzi huo ndani ya kipindi cha Wiki mbili ili kuona harakati alizoziagiza zimechukuliwa hatua zinazofaa mara moja.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Nd. Mohammed Suleiman Khatib alisema mitambo pamoja na vifaa vyote vinayokusudiwa kufungwa katika awamu ya Pili ya uimarishaji wa Miuondombinu ya Kiwanda hicho vimeshawasili hapa Nchini.
Nd. Mohammed alisema kinachosubiriwa kufungwa kwa mitambo hiyo ni kukamilika kwa ujenzi wa Banda pamoja na miundombinu ya umeme itakayokidhi mahitaji halisi ya kiwanda kutoka Kilowats 200 ziliazokuwa zikitumika hivi sasa hadi Kilowats 500 ili viendane na vifaa vikubwa vitakavyofungwa.
Mkurugenzi huyo wa Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kazi za uzalishaji Kiwandani hapo zitakwenda kwa ufanisi baada ya kukamilika kwa usambazaji wa umeme, huduma za maji kwa ajili ya mashine kubwa pamoja na milango mikubwa.
Hata hivyo Nd. Mohammed alielezea changamoto zinazokwaza kudorora kwa kazi hiyo akizitaja kuwa ni pamoja na ufinyu wa fedhakwa ajili ya Taasisi za uwekaji Umeme na wajenzi wa majengo ya kuwekea mashine hizo.
Alisema Jumla ya shilingi Milioni 252,000,000/- zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi ya usambazaji wa huduma ya Umeme kwenye kiwanda hicho pamoja na shilingi Milioni 185,000,000/- kumalizia majengo na miundombinu mengine.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim alisema kinachosubiriwa kwa sasa ili kufungwa kwa mashine hizo ni ukamilishaji wa miundombinu ya huduma za Umeme katika eneo hilo la Kiwanda cha Uchapaji.
Nd. Ahmad alisema wataalamu wa ufunguaji wa mashine hizo ambao wengine watatoka nje ya Nchi watahitaji kupata wiki mbili tu kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo baada ya kukamilika kwa miundombinu ya usambazaji wa Umeme.
Mradi huo Mkubwa wa awamu ya Pili wa uimarishaji wa Kiwanda cha Uchapaji Maruhubi ulioanza ujenzi wake mapema Mwezi wa Febuari mwaka huu umefadhiliwa na Serikali ya Oman kwa Gharama ya Shilingi Bilioni 12.5.
Gharama hizo zilielekezwa katika ununuzi wa mashine 34 tofauti kwa ajili ya kuendeleza kiwanda hicho zikiwemo mashine za rangi, Mabango, mashine za kuchomea pamoja na Plate.
No comments:
Post a Comment