Habari za Punde

Dk Shein awaongoza wananchi kwenye kisomo maalum kumuombea Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
 Zanzibar                                   7.4.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaongoza viongozi na wananchi mbali mbali katika kisomo maalum cha kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ikiwa pia, ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 44 ya kifo chake.

Marehemu Mzee Karume ambaye pia, alikuwa Kiongozi wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuawa siku ya Ijumaa tarehe 07 April, 1972 saa 12:05 jioni katika Makao Makuu ya ASP ambayo sasa ni Ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyopo Kisiwandui mjini Unguja.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Ofisi Kuu ya CCM ambako ndipo alipozikwa marehemu, Dk. Shein na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi walishiriki kisomo maalum cha kumuombea dua kiongozi huyo ambaye kifo chake kiliushitua ulimwengu mzima.

Baada ya kisomo hicho viongozi hao walizuru kaburi la marehemu wakiambatana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ambao walipewa fursa za kumuombea dua marehemu wakiwa kaburini hapo.

Kisomo hicho cha kumuombea dua Marehemu Mzee Karume kilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni  Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh  Abubakar Zubeir, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Sheikh wa Mkoa wa Dar-es- Salam Sheikh Mussa Salum.


Aidha, Mama Mwanamwema Shein alihudhuria katika tukio hilo akiungana na akina mama wengine akiwemo, Mama Fatma Karume na Mama Asha Balozi na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa pamoja na viongozi wa serikali zote mbili na wakiwemo viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge, Wawakilishi, Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar na wananchi kutoka sehemu mbali mbali.

Kisomo hicho cha kumuombea dua marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia, ni miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, kilitanguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na kuongozwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka Masjid Noor Mohammad,iliopo Kwa Mchina Mwanzo.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Hamid Masoud Jongo kutoka Tanzania Bara, alitoa mawaidha yalioendana na maudhui ya kumbukumbu hiyo na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi bora kutokana na kuwafaa watu waliowengi hapa nchini na kumuombea MwenyeziMungu ampe makaazi mema Peponi.

Sheikh Jongo alisema kuwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano zimefaidika na Muungano huo ulioasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na Marehemu Julius Kambarage Nyerere huku Sheikh Jongo akishangazwa na wale wanaoupinga Muungano huo.

Katika mawaidha yake hayo alisisitiza umuhimu wa kumuombea dua kiongozi huyo kutokana na msisitizo na msimamo wa kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad (S.A.W) wa kupita makaburi kwa kila mwaka kwa ajili ya kuwaombea dua wale wote waliouhami Uislamu na kutoa mchango wao mkubwa katika dini hiyo.

Sambamba na hayo, Sheikh Jongo alieleza kuwa kutokana na juhudi zake Mzee Karume ndio zilizopelekea kupatikana uhuru sambamba na kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu hapa nchini.

Mara baada ya tukio hilo, tukio lililofuata lilikuwa ni kuweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu Mzee Karume kitendo kilichofanywa na viongozi wakuu pamoja na muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Meja Jenerali Issa Nassor, wawakilishi wa familia, muwakilishi wa wazee waasisi Mzee Suleiman Omar pamoja na  muwakilishi wa Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar.

Marehemu Mzee Karume aliongoza harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar hadi kuongoza Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Kisultani uliokuwa ukihamiwa na Serikali ya Kingereza baada ya watawala hao kufanya kila njama za kuwanyima uhuru wananchi wa Zanzibar.
Mzee Karume anakumbukwa sana na wananchi wa Zanzibar kwa namna alivyoweza katika kipindi kifupi cha utawala wake kuleta mageuzi makubwa katika jamii ya Wazanzibari ambapo alisimamia haki na usawa katika umiliki wa njia za uchumi kama ardhi na kuondoa kabisa ubaguzi katika elimu, afya, ajira na kuwapatia wananchi makazi bora sambamba na mambo mengine muhimu ya kimaendeleo na kimaisha.
Mwenyezi Mungu alilaze roho ya marehemu mahala pema peponi-amin

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.