Habari za Punde

Skuli za msingi Wingwi zapatiwa vitendea kazi

 Mwalimu Yussuf Shoka Hamad alipokabidhi vifaa kwa Mwalimu mkuu shule ya msingi Simai, Wingwi, Mw. Muhammed Hamad pamoja na Walimu wengine wakiwa katika picha ya pamoja

 Mwalimu Yussuf Shoka Hamad akitoa maelekezo kuhusu vifaa alivyokabidhi kwa Walimu wa Shule za msingi Wingwi
Mwalimu Yussuf Shoka Hamad akikabidhi vifaa kwa Mwalimu Khamis Rashid wa Shule ya Msingi Wingwi


Na: Waandishi kutoka Pemba

Shule za msingi Mtemani, Wingwi msingi na Simai zote za Wingwi, wilaya ya micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, zimepatiwa msaada wa vifaa vya kisasa vya kutendea kazi kwa ajili ya kuleta ufanisi kazini.

Msaada huo uliotolewa na  mhadhiri kutoka chuo kikuu cha SOAS, London, nchini Uingereza  Mwalimu Yussuf Shoka Hamad, ulijumuisha mashine ya kompyuta za dawatini, mashine ya kutolea fotokopi, kupigia skani na kuchapishia barua na hati mbali za kiofisi.

Katika hafla fupi iliyoandaliwa na shule hizo jana (Jumatatu) mchana, Bwana Yussuf alisema kuwa lengo na nia yake ni kuzisaidia shule zote za  Wingwi kwa kuzipatia vitendea kazi vya kisasa ili kukuza ufanisi na kuendana na maendelea ya sasa ya dunia ya sayansi na teknolojia.

‘Lengo langu si kujijenga kisiasa. Mimi si mwanasiasa, naruadia kusema hivi na naisitiza tena kwamba sitoi misaada hii kwa madhumuni ya kisiasa. Mimi ni mzaliwa wa Wingwi na ari  ya uzawa na mchango nilioupata kwa jamii yangu ya Wingwi ni miongoni mwa misukumo inayonipelekea kutoa misaada hii bila kuchoka na bila kujali thamani, ukubwa au udogo wa vitu hivyo ninavyotowa’.


Bwana Yussuf pia aliongezea kwa kusema nia yake hasa ni kuzibadilisha shule zote za Wingwi na kuzifikisha katika kiwango cha ubora wa shule za kisasa kivitendea kazi ifikapo mwaka 2020. Moja kati ya mikakati yake ya kufikia lengo hilo ni kuhakikisha kila shule inapata mashine za kutolea kopi (photokopi) zenye uwezo wa kuchapisha mitihani ya ndani ya wanafunzi, kujenga maktaba za ndani ya shule hizo na kuzipa uwezo wa vifaa vya asili na vile vya kisasa ili kukuza kiwango cha elimu nchini.

Katika hafla hiyo, Bwana Yussuf aliahidi kuzipatia shule hizo mashine za kutolea photokopi (kubwa) ifikapo mwakani ambapo kila shule itaweza kujitegemea kwa vitendea kazi  vyenye uwezo na ubora wa kisasa.

Wakitoa shukrani zao kwa Mwalimu huyo, Walimu wakuu wa shule  hizo walimpongeza Mwalimu Yussuf kwa uzalendo na moyo wake wa kujitolea na  hasa katika kusaidia sekta ya elimu ya shule hizo za Wingwi.

‘Kwa kweli msaada huu ni mkubwa kwetu kiasi ambacho hatujui jinsi gani tufikishe shukrani zitakazofikia thamani ya msaada huu. Tunashukuru sana na tunakutakia heri na fanaka katika kazi zako ili uweze kusaidia zaidi katika sekta hii ya Elimu ya shule zako za Wingwi.’ Aliema Mwalimu Mohammed Hamad wa Shule ya Msingi Simai.

Naye Mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya msingi Wingwi, Bwana Khamis Rashid alimshukuru na kumpongeza Bwana Yussuf Shoka kwa hatua yake hiyo ya kukumbuka kusaidia shule za Wingwi ambako yeye (Yussuf) alisomea hapo.


Msaada huu wa zawadi uliotolewa ni moja ya sehemu za ahadi alizitowa Bwana Yussuf wakati wa hafla ya kuwazawadia wanafunzi waliofaulu mitihani yao ya darasa la saba mwaka jana ambapo kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo kimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.