Habari za Punde

Dk Shein: Juhudi zinahitajika katika kupambana na maradhi ya kipindupindu

Viongozi waandamizi wa Wizara ya Afya wakisikiliza kwa makini mazungumzo kati ya  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein na   Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO hapaTanzania Dr.Chatora Rufaro akiongoza Ujumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa UN 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na   Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO hapaTanzania Dr.Chatora Rufaro akiongoza Ujumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa UN walipofika Ikulu Mjini Zanzibar [Picha na Ikulu.]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                              19.4.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa juhudi za makusudi sambamba na mashirikiano ya pamoja zinahitajika katika kupambana na maradhi ya kipindupindu ambayo yameonesha kushika kasi hivi sasa hapa nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo katika mazungumzo kati yake na uongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa Tanzania, ukiongozwa na Mwakilishi wa Shirika hilo Dk. Chatora Rufaro pamoja na viongozi wengine wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) wanaofanya kazi zao hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliyapongeza mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanya kazi zake hapa nchini likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na UNICEF katika juhudi zao za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika mapambano ya maradhi ya kipindupindu yalioibuka hivi sasa.

Dk. Shein alisema kuwa ujio wa Mwakilishi huyo wa (WHO) hapa nchini katika kipindi hichi ni muhimu sana na utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya katika kusaidia mapambano ya maradhi hayo.


Alisema kuwa iwapo juhudi za makusudi zitachukuliwa na kila mmoja akafanya wajibu wake ipasavyo sambamba na kuwa na mwamko katika kuchukua tahadhari kuhusu kujikinga na maradhi ya kipindupindu hatua hiyo itasaidia katika kupambana na maradhi hayo ambayo hatimae yatapungua ama kuondoka kabisa.

Dk. Shein alisema kuwa maradhi hayo yana historia hapa Zanzibar na yaliwahi kuibuka katika miaka ya nyuma lakini baada ya juhudi kubwa za kuyatokomeza kuchukuliwa na Serikali kwa mashirikiano na wananchi pamoja na washirika wa maendeleo yalichukua muda kuibuka tena kutokana na juhudi za pamoja zilizochukuliwa wakati huo.

Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kudumisha usafi hasa katika maeneo yote ya visiwa vya Zanzibar yakiwemo maeneo ya Manispaa ya mji wa Zanzibar ambayo hali ya usafi wa mji huo haiko vizuri hali ambayo inachangia kuibuka kwa maradhi hayo.

Akieleza umuhimu wa kutumia dawa za kutia kwenye maji yaani vidonge vya “water guard” Dk. Shein alisema kuwa mbali ya hatua hiyo watendaji wa Wizara ya Afya nao wanajukumu kubwa katika kutekeleza majukumu yao na kusisitiza ulazimu wa kutumia maadili yao ya kazi katika kuwasidia wananchi.

Akigusia suala zima la elimu kwa jamii, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi mara kwa mara kupitia vyombo vya habari juu ya athari, kinga na maambukizi ya maradhi hayo.

Dk. Shein alisema kuwa mripuko wa maradhi hayo katika kipindi hichi ni changamoto kubwa kwa Wizara ya Afya na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuzisaidia sekta zote katika kupambana na maradhi hayo.

“Maradhi ya kipindupindu ni rahisi kupambana nayo iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia maji yasiyo salama ambayo ni moja ya chanzo kikubwa cha kupata maradhi haya….. kama tulivyofanikiwa kupambana na Malaria nalo hili linawezekana”,alisema Dk. Shein.

Nae Mwakilishi wa (WHO) nchini Tanzania Dk. Rufaro Chatora alimueleza Dk. Shein azma ya Shirika hilo katika kuisaidia Zanzibar kwenye vita ya kupambana na maradhi hayo hapa nchini na kusisitiza umuhimu wa kuwepo mashirikiano na uratibu wa pamoja kati ya taasisi za Serikali, taasisi za kiraia na watu binafsi katika kutekeleza wajibu wao juu ya kukabiliana na kipindupindu.

Mwakilishi huyo alieleza kuwa tokea mwezi wa Septemba mwaka jana yalipoibuka maradhi hayo hapa Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Afya na kuahidi ushirikiano zaidi katika kupambana na tatizo hilo huku akisisitiza haja kwa vyombo vya habari kusaidia juhudi hizo.

Aidha, Mwakilishi huyo wa (WHO) amesema kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Kimataifa litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi hayo ili kuhakikisha yanamalizika.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo alieleza kuwa chanzo kikubwa cha maradhi hayo ni maji hivyo kuna kila sababu ya kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutumia maji yalio safi na salama ikiwa ni pamoja na kutumia ‘water guard’ pamoja na kuimarisha usafi katika maeneo yote.

Akizitaja tahadhari juu ya maradhi hayo, Dk. Chatora alisema ni pamoja na kuweka mazingira safi, kufuata masharti ya afya, kuchemsha maji ya kunywa ama kutumia maji yaliyotiwa dawa ya kuulia bektiria wanaosababisha maradhi ya kipindupindu.

Pia, Mwakilishi huyo alieleza haja kwa wananchi kuwapeleka mapema katika vituo vya afya watu wanaobainika na dalili za maradhi ya kipindupindu kwa vile imeonekana wagonjwa wengi wanapopelekwa vituoni afya zao zinakuwa mbaya na hatimae matibabu yanakuwa magumu.

Mapema aliekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Mohammed Saleh Jidawi alieleza mashirikiano na uhusiano mwema uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo (WHO) jinsi linavyotoa ushirikiano wake katika vita ya kupambana na maradi hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.