Habari za Punde

Uongozi wa Elimu Zanzibar watembelea skuli


Na Mwashungi Tahir, MAELEZO-ZANZIBAR


WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali  Riziki Pembe Juma, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha  usafi wa mazingira katika maeneo ya skuli ili kudhibiti maradhi ya  mripuko  ikiwemo  kipindupindu.


Amesema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea skuli mbalimbali kufuatia mripuko  wa maradhi ya kipindupindu unaoendelea Zanzibar na athari ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha.Waziri huyo amesema iko haja  kwa walimu kuchukua  tahadhari  zaidi ya kuhifadhi mazingira kutokana na  ongezeko la  kipindupindu  ili kuwakinga wanafunzi na dhidi ya maradhi hayo.Mwalimu Mkuu wa skuli ya Faraja iliyoko Kilimahewa mjini Unguja Ameir Khamis Bakari, alimueleza waziri huyo kwamba skuli yao inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji nguvu ya serikali kuzimaliza.Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uchimbaji mchanga katika eneo la skuli, hali aliyosema inasababisha mmong’onyoko wa ardhi unaohatarisha majengo ya skuli hiyo.Aidha alisema kero nyengine ni mtindo wa wananchi wanaoishi karibu na skuli hiyo kutupa taka katika maeneo ya skuli.Alieleza kuwa tayari uongozi wa skuli umetoa taarifa kwa viongozi wa shehia lakini hata hivyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.Akizungumzia changamoto hizo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amalio Riziki Juma Pembe, alisema vitendo hivyo  haviwezi  kuvumiliwa hata kidogo.Aliahidi kuwa uongozi wa wizara utakaa pamoja na viongozi wa shehia kuyatafutia ufumbuzi  matatizo hayo ili kuwanusuru wanafunzi wa skuli hiyo na maradhi, na kuwawezesha kusoma katika mazingira mazuri.Katika mfululizo wa ziara hiyo, waziri huyo alifika katika skuli ya sekondari Vikokotoni, na kumtaka mmiliki wa duka lililopo mkabala na skuli hiyo, kurekebisha mabomba ya maji machafu yanayoingiza maji ndani ya skuli hiyo na kuwapa usumbufu wanafunzi na walimu.Kwa upande wake, Naibu Waziri Wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri, amewahimiza walimu wakuu  kuweka vipindi vya masomo ya mazingira ili kuwajengea wanafunzi tabia ya kudumisha usafi.Halikadhalika, ametoa wito kwa walimu wakuu kusimamia usafi katika maeneo ya skuli zao, ili kuimarisha usalama wa wanafunzi ambao ndio viongozi wa baadae.Skuli nyengine zilizotembelewa na viongozi  wa wizara hiyo, ni Mwanakwerekwe C, Kwamtipura na Haile Sellassie.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.