Habari za Punde

DK.Shein Aongoza Mazishi ya Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kusini Pemba.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                  26 Aprili, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  leo amewaongoza viongozi na maelfu ya wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Abdalla Mohamed Mshindo yaliyofanyika Kihinani, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Maghribi Unguja.

Mazishi ya marehemu Mshindo aliyefariki jana jioni huko nyumbani kwake Kihinani yalihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Akisoma wasifu wa marehemu Katibu Msaidizi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Chake Chake Ndugu Omar Abdalla Omar alieleza kuwa Chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa marehemu Abdalla Mohamed Mshindo ambaye alikuwa kiongozi shupavu aliyekitumikia chama hicho kwa uaminifu mkubwa.

Kwa hivyo chama hicho kinaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa na kuwaomba wote walioguswa na msiba huo kuwa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Kwa mujibu wa wasifu huo, marehemu alizaliwa katika kijiji cha Chambani Wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba terehe 2 Mei 1959.

Alipata elimu ya msingi mwaka 1972 hadi 1979 katika skuli ya Makoongwe wilaya ya Mkoani na alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1982 katika skuli ya sekondari ya Fidel Castro iliyopo wilaya ya Chake Chake.

Katika uhai wake marehemu Mshindo alishika nyadhifa mbalimbali katika Chama cha Mapinduzi zikiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Tawi la Makoongwe mwaka 1986 hadi 1992 na baadae kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Mkoani mwaka 1992 hadi mwaka 2000.

Mwaka 2000 marehemu Mshindo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba wadhifa alioutumika hadi mauti yalipomfikia hiyo jana.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Peponi-Amin 


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.