Habari za Punde

Watendaji BLW waiomba Serikali kuiridhia na kuipitisha Sheria ya Utawala wa Baraza

Na, Himid Choko  BLW

WAFANYAKAZI  wa Afisi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wameiomba Serikali  pamoja na Wajumbe wa Baraza hilo, kuridhia na hatimae kuiipitisha Sheria ya Utawala wa Baraza  ili kuleta ufanisi wa utendaji ndani ya Afisi hiyo.

Wafanyakazi hao wametoa ombi hilo leo, wakati wa mkutano wa pamoja  wa kujadili Utendaji wa kazi , mkutano ambao pia umehudhuriwa na Spika wa Baraza hilo  Mhe  Zubeir  Ali Maulid na Naibu Spika  Mhe. Mgeni Hassan Juma.

Mmoja ya Wanyakazi  hao Makame Salim wa Sehemu ya Taarifa Rasmi za Baraza  amesema Sheria  ya Utawala wa Baraza  ambayo kwa sasa imeshapelekwa Serikalini , endapo itakubalika itasaidia kwa kiasi kikubwa  kulifanya Baraza kuepukana na changamoto mbali mbali za kiutendaji ndani ya muhimili huu wa Dola.

Amesema kuwa miongoni mwa faida zitakazopatikana baada ya kupitishwa sheria hii ni Uhuru wa  Baraza wa kujiendesha na kujiamulia  mambo yake wenyewe kama yalivyo Mabunge mengi ya nchi za Jumuiya ya Madola.

“Hata Baraza na Ofisi ya baraza la Wawakilishi kwa jumla, linakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini ikipatikana Sheria hii ya Utawala ya Baraza asilimia kubwa ya changamoto hizi zinaweza kutatuliwa, na jambo hili sio geni kwani  mabunge ya Jumuiya ya madola yamekuwa yakiendeshwa kwa mfumo kama huu” alimalizia ndugu Makame.

Wamesema  Sheria hiyo pia itasaidia kuiwezesha Ofisi ya Baraza kuwa na  uwezo wa kuwasimamia watumishi wake  katika njanja za maslahi, wajibu na adhabu pale wanapokwenda kinyume na utaratibu wa majukumu yao ya kazi.


Aidha Wafanyakazi hao wamesisitiza  kuangalia upya maslahi yao ukizingatia  mazingira nyeti ya kuwahudumia wanasiasa  na  kutunza siri za serikali.

‘Mhe Spika, kwa kweli tunafanya kazi katika mazingira magumu na nyeti, tunawahudumia viongozi na wanasiasa na tunatunza siri nyingi, kama maslahi yetu yataendelea kuwa kama haya nafasi kama hii inaweza kutumiwa na wafanyakazi wasiokuwa waaminifu kutumika vibaya na watu wengine wasiopendelea mafanikio ya nchi yetu” Alisisitiza Sulum Mkubwa wa Divisheni ya hansard ya Baraza la Wawakilishi. 

Mkuu wa divisheni ya Utafiti na maktaba ya baraza la wawakilishi, Othaman Ali Haji amemuomba Spika kupigania Upatikanaji wa Fursa hizo kama vile elimu na kozi za muda mfupi hasa nnje ya nchi kama vile zinavyopatokana katika taasisi nyengine serikalini.

Nae Spika Maulid ameahidi   kushirikiana na wafanyakazi hao na kusimamia maslahi yao na kuwaomba kuzidisha umoja na mashirikiano  katika utendaji wao wa  majukumu yao ya kazi.

Amesema  katika kuimarisha mahusiano mema  ya kikazi atajenga tabia ya kukutana na wafanyakazi hao mara kwa mara  ili kushauriana ,  kuelekezana na kukosoana kwa lengo kuhimiza wajibu na uwajibika kati ya Viongozi wa Baraza, Afisi ya Baraza na watumishi wa Afisi hiyo.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.