Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Moh’d Dahoma akifungua mafunzo ya siku moja kwa wandishi wa Habari kuhusu maradhi ya kipindupindu katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo ya siku moja juu ya maradhi ya kipindupindu wakifuatilia mafunzo hayo katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar Nd. Kheri Makame Kheri akitoa ufafanuzi kuhusiana na maradhi hayo na kuwataka waandishi kujikita zaidi kuelimsha jamii.
Ofisa Afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Ofisi ya Dar es salaam Dkt. Neema Kileo akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) waliohudhuria mafunzo ya siku moja juu ya mripuko wa maradhi hatari ya kipindupindu Zanzibar.
Mwandishi wa habari kutoka Zenj F M Radio Mustafa akichangia mada zilizowasilishwa katika mafunzo ya siku moaja ya waandishi wa habari iliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar Mnazimmoja.
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia katika afya na mawasiliano kutoka Wizara ya Afya Salum Aboubakar akitoa tathmini ya maradhi ya kipindupindu tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana mpaka hivi sasa.
Na Ramadhani Ali/MAELEZO ZANZIBAR
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Muh’d Dahoma amesema ili ugonjwa wa Kipindupindu umalizike inategemea zaidi maamuzi ya familia na jamii kwa jumla kukubali kubadilika.
Amesema desturi potofu na tabia za wananchi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizi ya kipindupindu nchini.
Akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa kipindupindu yaliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja, Dkt. Dahoma amewataka waandishi wa habari kutoa elimu zaidi kwa jamii ili wajue sababu zinazopelekea kuongezeka ugonjwa huo na njia za kujikinga.
Amesema bado wananchi wanakuwa wagumu kubadili mfumo wao wa maisha licha ya juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya za kimataifa, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na vyombo vya habari.
‘’Bado watu wanaishi katika mazingira machafu, wengine hawana vyoo na wapo hawataki kuyatibu maji ya kunywa, mambo yanayochangia mambukizi ya kipindupindu,’’ alisisitiza Dkt. Dahoma.
Ameishauri jamii kuwa tayari kubadilika baada ya kupata elimu ya maradhi ya kipindupindu ili kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Akitoa takwimu ya maradhi ya kipindupindu tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana, amesema wananchi 3,700 wameugua maradhi hayo na 46 kati yao wamefariki na Wilaya ya Magharibi inaongoza kwa kutoa wagonjwa wengi zaidi.
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia katika afya na mawasiliano kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Nd. Salum Aboubakar amewashauri wahariri wa habari kuvipa kipaumbele vipindi na habari zinazohusu Kipindupindu katika vyombo vyao ili wananchi waweze kuzinduka.
Nae Ofisa Afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Ofisi ya Dar es salaam Dkt. Neema Kileo ameshauri vipindi vinavyozungumzia kipindupindu vipangwe katika muda ambao wananchi wengi wanaweza kuvisikiliza.
Washiriki wa mafunzo hayo wamekubali kutoa muda zaidi katika vyombo vyao vya habari kwa maafisa wa Kinga na Elimu ya Afya ili kutoa elimu zaidi katika kukabiliana na maradhi hayo.
No comments:
Post a Comment