Habari za Punde

Balozi Seif akabidhi msaada wa kompyuta 20 Skuli ya Serkondari Mahonda

 wa kwanza kutoka kushoto ni Mwanafunzi Mahija Said  Ramadhan wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda akiendelea na mafunzo ya somo la Kompyuta na Mwanafunzi mwenzake Pili Moh’d Daudi wakiwa na mwalimu wao wa somo hilo Mwalimu Kassim Hamid Mansour.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif alitoa msaada wa Kompyuta 20 kwa skuli hiyo alishuhudia zoezi hilo lilompa faraja kwa wanafunzi hao kuanza kuajiandaa na mabadiliko ya taaluma ya kisasa ya teknolojia ya mawasiliano.
 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda  Balozi Seif akimuahidi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda mwalimu Rashid Abdulla wa kwanza kutoka kulia kusaidia uimarishaji wa darasa la maabara la Skuli hiyo wakati alipoitembelea akiwa kwenye ziara ya kushukuru wananachi baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu.
  Baadhi ya Wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Mahonda wakiendelea na mazoezi ya somo la kompyuta baada ya kupatiwa msaada na mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi.

Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/- Kiongozi wa Timu ya Soka ya African Boys hapo Magumashi Maskani ili ziwasaidie katika kujiandaa na laigi Daraja la Kwanza.

Timu hiyo ya Kitope iliyomo ndani ya jimbo la Mahonda imekuwa bingwa wa Wilaya na kupanda daraja katika msimu uliomalizika hivi karibuni.


Picha na – OMPR – ZNZ.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba wakati umefika kwa wanafunzi wa skuli za Sekondari nchini kujifunza kutumia vyema taaluma ya Mitandao ya Teknolojia ya Kisasa ya Mawasliano ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Dunia yaliyopo hivi sasa katika matumizi ya fani hiyo.

Balozi Seif alisema hayo wakati akikagua madarasa ya Kompyuta ya Skuli za Sekondari za Kitope na Mahonda ndani ya Jimbo la Mahonda  baada ya kuzipatia msaada wa vifaa hivyo na kuzindua rasmi madarasa yake.


Msaada huo umezinufaisha Skuli hizo ambapo ile ya Kitope ilikabidhiwa Kompyuta 25 wakati ile sekondari ya Mahonda ilikabidhiwa na kuanza na Kompyuta kumi.

Alisema mtandao wa Teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano umemsaidia sana mwanaadamu kurahisisha maisha yake ya kawaida kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba taaluma hiyo pia imetoa fursa za ajira kwa vijana wengi kwenye maeneo mbali mbali duniani.

Balozi Seif alieleza kwamba wimbo wa sayansi na teknojia ulioanikiza kila pembe ya dunia hii lazima kwa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla uelekee katika kusaidia kufanikisha changamoto zinazoikabili jamii na hasa watumishi wa taasisi za Umma.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliupongeza Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope kwa uamuzi wake wa kuanzisha darasa la Kompyuta litakalotoa fursa kwa wanafunzi wake kuingia vyema ndani ya dunia ya utandawazi kwa kujiamini.

Akiguzisa changamoto nyingi zinazoikabili skuli ya Msingi na Sekondari ya Mahonda Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliahidi kushirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na Kamati ya Skuli katika kuona changamoto hizo zinapungua kadri ya hali ya uwezeshaji itakavyoruhusu.

Aliiomba Kamati ya Skuli hiyo msingi na sekondari  kuanza kushirikiana na wazazi wa wanafunzi katika kutafuta mbinu na kuweka mikakati itakayosaidia kupunguza zile changamoto zilizomo ndani ya uwezo wao.

Balozi Seif aliwapa matumaini Walimu na wanafunzi hao hasa wale wa skuli ya msingi kwa kuwaahidi kutafuta wahisani watakaounga mkono nguvu za kusaidia vikalio vya madarasa ya skuli hiyo.

Alisema hatua ya kwanza itahusisha vikalio 100 kati ya mahitaji halisi ya vikalio 300 tatizo ambalo limekuwa alikiziathiri skuli nyingi za hapa Zanzibar na hata zilizopo Tanzania Bara.

Alifahamisha kwamba kutokana na upungufu wa vikalio baadhi ya viongozi wamebuni mbinu za kuanzisha michango ya hiari { Harambee } kwa kuzishirikisha taasisi na  mashirika ya maendeleo kuchangia nguvu zao.

Wakisoma risala za skuli zote mbili Mwalimu Dadi Salum Rashid wa Sekondari na Mwalimu Hiba Mmanga kwa pamoja wamemshukuru Mwakilishi huyo kwa jitihada zake za kusaidia kambi kwa wanafunzi wa skuli hiyo na hatimae kufanya vyema katika mitihani yao.

Walisema kiwango cha ufaulu katika skuli hiyo kimepanda na kufikia asilimia 86.3% kwa wanafunzi wa darasa la kumi na mbili { Form 1V } na asilimia 85.5% kwa wanafunzi wa darasa la 14{ Form VI } kwa mwaka 2015.

Hata hivyo Mwalimu Dadi Salum na Mwalimu Hiba Mmanga walieleza kwamba licha ya mafanikio makubwa ya ufaulu kwa wanafunzi hao lakini bado zipo changamoto nyingi zinazochangia kuviza kwa maendeleo na ufaulu zaidi ya wanafunzi hao.

Walizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa madarasa na yale yaliyopo baadhi yameshachakaa sana, ukosefu wa vikalio kwa wanafunzi wa madarasa ya skuli ya msingi, uchelewaji wa kukamilika kwa jengo la maabara pamoja na ukumbi wa mitihani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.