Habari za Punde

Balozi Seif akabidhi gari kwa kamati ya jimbo la Kitope

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Jimbo hilo wakifurahia jambo mara baada ya kukabidhi Gari kwa ajili ya shughuli za kazi za Kamati hiyo ya siasa ya Jimbo.

Aliyemo ndani ya kiti cha dereva ni Kaimu Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mahonda Nd. Haji Salim akilijaribu gari hilo mara baada ya kukabidhiwa rasmi na Balozi Seif.

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif akimkabidhi Kadi ya uwanachama Mpya wa CCM Bibi Subira Kheir Faki mara baada ya kuizindua rasmi Maskani ya CCM ya Magumashi iliyopo Kitope B.

Kushoto ya Balozi Seif ni Kaimu Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mahonda Nd. Haji Salmin na mwenye kipaza sauti ni Katibu wa Jimbo hilo Bibi Hasina Juma.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewatanabahisha wanachama wa Chama hicho wenye tabia ya kuendekeza tamaa na ubinafsi wanapaswa kuelewa kwamba hulka hizo zinaweza kukiangamiza Chama chao kilichopewa mamlaka ya kuongoza Dola.

Alisema kazi iliyopo mbele ya wanachama hao wa CCM kwa sasa ni kuhakikisha wanajipanga kuimarisha jumuiya zao ili Chama chenyewe kipate nguvu zaidi za kuendelea kuongoza dola hata baada ya uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Balozi Seif Ali Iddi ambae ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na pia Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitoa nasaha hizo wakati akikabidhi Gari ya Usafiri kwa Kamati ya Siasa ya Jimbo hilo itakayosaidia utekelezaji wa majukumu yao hafla iliyofanyika hapo Tawi la CCM Kitope “B”.


Hafla hiyo fupi ilifanyika akiwa katika ziara maalum ya kuwashukuru Wanachama wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Wananchi wa Matawi na Shehia zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa marejeo wa Tarehe 20 Machi mwaka huu.

Balozi Seif alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM kwenda kinyume na maadili na kanuni za Chama chao kama walivyoahidi wakati wa kujiunga na uanachama kinaweza kusababisha hali tete ya amani ya nchi ambayo CCM ndio pekee inayoweza kuisimamia vyema.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliiagiza Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi ya Jimbo hilo iipangie majukumu gari hiyo ili iweze kutoa huduma ya usafiri kataka mpangilio utakaokubalika na wanachama wenyewe.

Balozi Seif alionya kwamba hatopendelea kusikia kwamba gari hiyo inaanza kuleta ugomvi baina ya Viongozi na Wanachama wao ndani ya jimbo hilo katika kipindi kifupi kijacho.

Katika ziara hiyo ya shukrani iliyohusisha Matawi ya Chama cha Mapinduzi ya Kitope “B” na Mahonda mapema Balozi Seif pia alipata fursa ya kuzindua  rasmi Maskani ya CCM ya Magumashi iliyopo Kitope “B”  na kutoa kadi kwa wanachama wapya wa CCM wa Maskani hiyo iliyojengwa katika hadhi inayokubalika na kulingana na chama chenyewe.

Akisoma Risala Mwenyekiti wa Maskani ya Magumashi Mzee Khamis Ndende Juma alisema juhudi za Balozi Seif  zinazopaswa kushukuriwa ndizo zilizopelekea Vijana wa eneo hilo kupata hifadhi ya Maskani  ambapo awali walikuwa wakifanya shughuli zao katika Vijiwe.

Ndugu Ndende kwa niaba ya Wanachama wenzake wamewapongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kwa kuetekelza majukumu yao mara tu baada ya kuchaguliwa  kuziongoza Serikali za Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwenyekiti huyo wa Maskani ya CCM Magumashi alisema kazi inayotekelezwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Magufuli inakubalika na Watanzania wanaosheshimu uadilifu.

Wanachama hao wa Maskani ya Magumashi wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwachukulia hatua kama inavyochukuliwa na Serikali ya Mauungano wa Tanzania wale wote wanaoendeleza vitendo vya ubadhirifu wa mali za Umma.

Alieleza kwamba Zanzibar kama Nchi na Kisiwa wapo baadhi ya watendaji hasa katika Taasisi za Umma wenye kuendeleza tabia ya udokozi wanaopaswa kuchukuliwa hatua za sheria mara moja ili kwenda sambamba na kasi ya upande wa Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.