Habari za Punde

Majimbo yanayoongozwa na wanawake Pemba yawe mfano kimaendeleo

 Wanaweza, wathubutu, wahangaikaji na wajasiri
Na Haji Nassor, Pemba
WANAWAKE na uongozi, wanawake wanaweza bila ya kuwezeshwa, wanawake ni wajasiri, wanawake ndio wenye uchungu wa maendeleo.
Kauli hizi na nyengine zimekuwa maarufu sio Zanzibar pekee, lakini kila kona kama sio pembe ya ulimwengu huu wa karne ya 21.
Kila mmoja ni shahidi kuwa, kundi hili la wanawake liliachwa nyuma kwa karne takiriba 20, za ulimwenguni likionekana kama vile halipaswi kufikia malengo yake.
Kwa Zanzibar wenye kukumbuka historia ya miaka kadhaa hadi mwaka 1964 pamoja na Zanzibar kutawaliwa na wakoloni, na kuwepo kwa udhalilishaji, lakini wanawake walikuwa zaidi.
Inasemekana walikuwa wakifanyishwa kazi kubwa yenye ujira mdogo, hawakuwa na nafasi ya kuuliza, kusikilizwa, kushiriki wala kushirikishwa tena hata kwenye mambo yanayowahusu.
Lakini baada ya mwaka 1964 kwa Zanzibra kufanyika Mapinduzi ambayo yalikuja kumuondoa mkoloni, sasa alau wanawake kwa lugha za vijana, wakaaza kupumua.
Ingawa ilichukua muda sana kwa kundi hili la wazazi wetu kuonekana kama wananchango ndani ya familia na taifa kwa ujumla, lakini walishasema wahenga kuwa papo kwa papo kamba hukata jiwe.

Ndani ya karne hii ya 21, baada ya wanawake kujikusanya kule Beinjin nchini China na wakaibuka maazimio kadhaa, sasa hapo utetezi, ulianza wa kupewa haki zao uliibuka.
Zamana na kauli mbiu zilianza kuwa, wanawake wapewe haki zao, kisha wawezeshwe, wanawake wanahaki ya uongozi, wengine wakaibuka na wanawake na umiliki wa rasilimali.
Yote kwa yote hayo, ni ishara kwamba sasa kundi la wanawake ambalo kwa karne 20, lilikuwa limebanwa na makundi ya wanaume.
Lakini wapo viongozi kama vile rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, wakati anaingia Ikulu ya Zanzibar mwaka 2010 alianza kwa kuwapa nafasi za uwaziri.
Maana wengi walishaota mizizi kwenye akili zao kwamba, wanawake hawapaswi kuonekana kwenye meza refu wakiwa mawiziri.
Kauli mbiu ya wanawake na uongozi wakati huo na sasa imeshikiwa bango na wanaharakati kama vile TAMWA, ZAFELA, ZSLC, TGNP, ZAWCO, na mradi wa WEZA na ndio maana idadi ya wanaoibukia majimboni inaongezeka.
Kwa kisiwani Pemba kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 na baadhi ya vyama kuususia, kama vile ilikuwa faraja kwa wanawake waliogembea kutimiza ndoto zao.
Sasa majimbo ya Chambani, Gando, Wete na Mtambwe yanashikwa na wanawake, na Inshallah hadi hapo mwaka 2020 utakapoitishwa uchaguzi mwengine mkuu.
Tulishaambiwa na watetezi wa haki za wanawake hata wanawake wenyewe kwamba, mwanamke akikabidhiwa uongozi maendeleo ya kweli hupatikana.
Kwa hili Juma Hassan Juma wa Jimbo la Chambani yeye anasubiri kuona ahadi za mwakalishi wake Mhe: Bahati Khamis Kombo.
“Mimi nilikuwa natamani sana kuona uongozi wa mwanamke hasa ngazi ya Jimbo, maana huwa twaelezwa kwamba wanawake wanaweza’’, alisema.
Rahika Juma Haji anasema pamoja na hilo lazima mwanamke kama kiongozi, apewe ushirikiano na sio kuachiwa mizigo, ili atimize ndoto zake.
Mwanajuma Hija Hamad wa Mtambwe, yeye anasema hana shaka kama wananchi wa jimbo hilo wanahitaji maendeleo, sasa wajipange.
“Unajua sisi wanawake tukishapewa madaraka hasa yenye uamuzi kama ya uwaziri, uwakilishi na ubunge, basi mafanikio ya kweli yataibuka’’, alifafanua.
Khamis Omar Kibano ndugu wa mwakilishi huyo wa Jimbo la Mtambwe, Mhe: Khadija Omar Kibano, hana shaka na utendaji wa kazi wa mwakilishi huyo, na miaka hii mitano maendeleo yatapatikana.
Mwenyewe mwakilishi huyo wa Jimbo la Mtambwe, anasema wananchi wa Jimbo hilo, watarajie makubwa ya kimaendeleo atakayoyafanya.
“Mimi kweli nilikuwa mwanaharakati mkubwa wa kuhamasisha wanawake na uongozi, na sasa nimefanikiwa wananchi wakae mkao wa kula’’, alifafanua.
Wanaharakati kama vile TAMWA wanajivunia kupatikana kwa wawakilishi hao wanne wa majimbo ya Pemba, wakiamini sasa pumu imepata mkohozi.
TAMWA kupitia Mratibu wake Zanzibar Mzuri Issa Ali, anasema mchakato wa kuwahamasisha wanawake kuingia kwenye safu ya uongozi ni jambo endelevu.
Muhusin Kombo Makame anasema wanawake hao wanaweza kudumu ndani ya majimbo hayo hata kwa miaka mengine mitano ijayo, ikiwa wananchi wanahitajia maendeleo.
“Unajua tatizo letu la Pemba tulio wengi tunahitajia zaidi chama fulani kishinde, na sio mtu wa chama chengine kutuletea maendeleo’’, alifafanua.
Bahati Khamis Kombo mwakilishi wa Jimbo la Chambani, wakati akinadi sera zake, yeye aliwaambia wapiga kura kuwa, kama akifanikiwa nafasi hiyo wajenge matarajio makubwa.
“Unajua wanawake wanapopata nafasi na kisha jamii ikakubali kushirikiana nao, basi wananchi wanaweza kufikia malengo yao, maana mwanamke ndio mjenzi wa familia’’, aliafafnua.
Wanawake ambao hawajaingia kwenye uongozi wamekuwa   zaidi wakiwalalamikia, baadhi ya viongozi wanaume kwamba wamekuwa wakifanya pasi na uoni wa mbali.
Mwanaharakati Asha Abdi kutoka TAMWA, anasema sio busara kuona kila nafasi za uteuzi zinashikwa kwa wingi na wanaume huku wanawake wakikosa uwakilishi.
Wasiwasi wake ni kuona sauti za wanawake zikikosa mwakilishi hasa kwenye mambo yanayowahusu, jambo ambalo ni aina nyengine ya udhalilishaji.
“Unajua kila kiongozi anaeingia kwenye madaraka husahau kuwa kunakundi kubwa la wanawake, ambalo ndio walezi na familia na jamii yote’’, alibainisha.
Ndio maana sasa macho na masikio ya wananchi wengine wa kisiwani Pemba, wanayamulika majimbo manne ya Mtambwe, Gando, Wete na Chambani yanayoongozwa na wanawake.
Wapo wanaohoji kuwa, majimbo hayo yataendelea kushikiliwa tena na wanawake hao hata kwa uchaguzi wa mwaka 2020, maana wananukuu kauli kuwa wanawake wanauthubutu.
Nilipomtaka aelezee hilo hivi karibuni Mkoani Mtwara mwanaharakati na Mkurugenzi mstaafu wa TAMWA, Valerie Msoka anasema kwanza ni kuhakikisha wanapewa ushirkiano.
“Haina maana kuwa kila jimbo au nafasi aliopewa mwanamke kwamba ndio ataleta mafanikio, kama atatengwa, jambo la kwanza ni kuona wanashauriwa’’, alisema.
Msoka anasema hata wanaume kama hawakupewa ushirikiano kama anavyopewa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: John Magufuli hivi sasa, kamwe hawezi kufikia malengo yake.
Yeye anashauri wanawake walioibuka na ushindi kwenye majimbo na nafasi nyengine kufanya kazi kwa moyo wa juhudi akiamini matunda yataonekana.
Sasa kama wapo wanawake walioubika na ushindi na kuteuliwa kwenye nafasi mbali mbali za uamuzi, ni wakati wa viongozi hao kuonyesha utendaji wao wa kazi.
Yeye mwakilishi wa Jimbo la Gando Maryam Thani Juma, anasema hakuna atakaloliweza peke yake, pasi na wananchi wake kukaa chini na kushirikiana.
“Unajua mwanamke pamoja na umahiri wake, lakini anahitaji kupewa ushirikiano, ili yale aliojipangia aweze kuyafikia maana sio mashine kama ukishaiwasha inafanya kazi’’, alifafanua.
Tena inawezekana zipo nafasi kwa muda mrefu zinashikiliwa na wanaume, mfano kama majimbo kadhaa ya Pemba ambayo wanaume walikuwa kama walioyarithi.
Leo kama tunayo majimbo manne yanashikwa na wanawake Pemba, lazima zile kelele, kauli mbiu, maadhimio ya utetezi kwa wanawake na uongozi tuone yakizaa matunda.
Maana kila mmoja anaamini kuwa, mwanamke ndio mjenzi wa familia, jamii, tarafa, shehia, halimashauri, wilaya, Mkoa na taifa sasa haya lazima yajitokeze.
Kijana Fatma Himid Mashaka wa Kojani, yeye anasema wanawake sio mashine, bali jambo la mwanzo wanapopewa uongozi isiwe kama wanajaribiwa.
“Inawezekana wengi wanafikiria kuwa, wanawake wanapopewa nafasi za uongozi kama vile wako majaribioni, lakini ni haki yao kama lilivyokundi jengine’’, anabainisha.
Yeye anasema iwe Mtwara, Kilimanjaro, Wete au Makunduchi kama kuna mwanamke amepata nafasi ya uongozi, suala la kupewa nguvu linahitajika.
Aliekuwa Afisa Mdhamini wizara inayoshughulikia wanawake na watoto kwa sasa, Naibu Katibu mkuu wizara hiyo Mauwa Makame Rajab, anasema mafikio ya mwanamme yanatokana na mwanamke.
“Unajua wanaume wengi wanadhani wanapofanya vyema kwenye uongozi hawajui kuwa, nyuma yao yupo mwanamke na mwanamke ili afanikiwe awepo mwanamme’’, alifafanua.

Yote kwa yote…… majimbo manne ya Pemba ambayo wajumbe wake wa baraza la wawakilishi ni wanawake, tunatarajia yawe mfano kwenye utekelezaji wa ahadi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.