Habari za Punde

GEWE mradi uliopunguza vitendo vya udhalilishaji


Na Zuhura Juma, PEMBA

“GEWE imetuwezesha kuibua matendo ya udhalilishaji yaliyokuwa yamejificha katika jamii”

 “Ama kweli! kikulacho, kinguoni mwako”, wahenga hawakukosea walipoutoa msemo huu, kwani wakati wote huo tumekuwa tukiliwa na matendo ya udhalilishaji bila kujijua wenyewe.

“Tulikuwa kimyaa… mda wote huo kama tuliozindikwa, jinsi matendo ya udhalilishaji yalivyokuwa yakitokea bila wenyewe kushughulika na kuliona ni jambo la kawaida"

… hivyo ndivyo yalivyokuwa yakiwatoka maneno waratibu wa shehia, jinsi walivyoweza kuyaibua matendo yaliyokuwa yakitendeka katika jamii…

Kwa kweli ni jinamizi kubwa lililokuwa likiinamia jamii siku za nyuma, ingawa bado lipo lakini limebakia ncha tu liweze kuondoka.

Na hili linawezekana kuliondosha kabisa, kwani tumeweza kula samaki mzima… hivi tushindwe na mkia?

“Mhuuu… lililopo lipoo, maana tumejua mengi zaidi na zaidi katika jamii yaliyokuwa yamefunikwa nyungu na baadhi ya wanajamii”, waliongeza kusema.

Kwa kweli jamii ilidhalilika kwa watoto kubakwa, kulawitiwa na hata kutelekezwa na wazazi wao.

Jambo ambalo lilipelekea watoto wengi kukosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kukosa elimu.


Vitendo hivyo vilionekana kushamiri siku hadi siku katikia jamii, lakini mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake ‘GEWE’, uliweza kuvipunguza kwa kiasi kikubwa.

Hii ni katika jitihada yake ya kutoa elimu katika nyanja tofauti, ilimuradi yaweze kupotea kabisa katika jamii.

Na hili limefanikiwa ingawa havijaondoka vyote lakini vimepungua.

Mradi huo ulitoa fursa ya kuibua maovu yaliyojificha, kutoa elimu kwa jamii ambapo iliweza kuelimika, kuibua kesi za udhalilishaji.

Pia kutatua kero ikiwa ni pamoja mabomba ya maji machafu ambayo yanaweza kusababisha maradhi.

Tokea kutolewa elimu kwa waratibu wa shehia zilizopitiwa na mradi huo, imesaidia sana kuibua matatizo yaliyojificha katika siku za nyuma kwenye jamii.

Labda niseme GEWE inahitaji pongezi kubwa kwa jitihada zake zilizotumika katika kuvipiga vita vitendo vya udhalilishaji katika jamii.

Elimu ya taarifa na maarifa ni miongoni mwa elimu waliyoipata waratibu hao, ambayo walitakiwa kuweka kituo kitakachoweza kuleta mabadiliko zaidi.

Kituo cha taarifa na maarifa ni kituo cha wanaharakati ngazi ya jamii ambayo itasaidia jamii kupata uelewa na uchambuzi na kuona wanajenga nguvu za pamoja, ili kuleta mabadiliko.

Kituo hicho kinatakiwa kianze ngazi ya shehia, ili kuzikusanya kesi na kuzipeleka katika kituo na kuweza kuzifuatilia kwa pamoja.

Kufanya hivyo kutapelekea kujenga nguvu za pamoja katika kuzishughulikia kesi kwa pamoja na kwa kina, ili kuweza kuzipatia ufumbuzi unaofaa.

Mafunzo hayo, ymewafanya waratibu hao kuungana kwa pamoja na kushirikiana katika kuyafichua matatizo yaliyojificha na kuweza kuyakusanya pamoja na kuyafuatilia.

Kituo cha taarifa na maarifa kimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuyakusanya matukio ya udhalilishaji yanayotokea katika  kila shehia.

Siti Khatib Ali mratibu wa shehia ya Mchangamdogo akisifu kituo cha taarifa na maarifa kimeweza kuwasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kuleta mabadiliko.

“Kituo kimetusaidia sana, kwani tumeweza kukutana na kubadilishana mawazo na kutafuta njia ya ziada ya kuweza kuvitokomeza vitendo hivi”, alizidi kusifu.

Kama wahenga walivyosema ‘Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu’, hivyo msemo huu umewasaidia sana waratibu pale ambapo wameweka kituo kwa ajili ya kukutana na kupanga mikakati yao.

Mratibu wa shehia ya Mjiniole, Khadija Henoik Maziku anafahamisha tokea kuweka kituo hicho wameweza kuzikusanya kesi katika kila shehia na kuzikusanya pamoja katika kituo.

Jambo ambalo limewarahisishia katika shughuli zao za ufuatiliaji, kwani wengi sio mmoja hivyo hushirikiana katika kulitatua tatizo.

“Kituo chetu cha taarifa na maarifa kimetujengea ushirikiano mkubwa na tumepata ule mwamko wa kuzikusanya kesi katika shehia zetu na kuzifikisha katika kituo kwa ajili ya kuzifuatilia”, alisema huku uso wake ukionesha furaha.

Ni kesi 47 zilizoripotiwa katika kituo cha taarifa na maarifa, ambazo zimetoka katika shehia zilizopitiwa na mradi wa GEWE.

Kesi hizo zipo katika mchakato wa kuzifuatilia, ambapo hushirikiana kwa pamoja jambo ambalo limekuwa ni faraja kwao kwa kuwepo kwa kituo hicho.


Salma Abdallah Hamad mratibu kutoka shehia ya Shengejuu hakukaa kimya jinsi alivyofaidika na elimu hiyo ya kuweka kituo cha maarifa na taarifa kwa kupiga hatua kubwa ya kupambana na kesi za udhalilishaji.

“Tumeweza kuzikusanya kesi kwa pamoja katika kituo chetu cha taarifa na maarifa, ambapo kesi za utelekezwaji zimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na nyuma”, alieleza.

“Kwa sasa kesi za utelekezwaji kwa wanawake na watoto zimeonesha sura nzuri, kwani akina baba walio wengi wamekuwa karibu na familia zao.

Jamii imebadilika kutoka hali moja kwenda nyengine, ambapo kesi zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Kupungua kwa kesi hizo, ni faraja kubwa kwa waratibu hao, jambo ambalo ndio lengo kubwa la mradi wa GEWE katika kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji.

Waratibu hao pia waliweza kupatiwa elimu ya urakidishi, ambayo imewawezesha kupita katika jamii na kujua changamoto zinazowakabili wananchi.

Walitakiwa kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi ambazo ni huduma za jamii na kuziwasilisha katika vyombo vya habari, ili kuweza kupata ufumbuzi.

Tokea kuweka kituo hicho tayari wamefanya mambo mbali mbali kutokana na ushirikiano mkubwa waliouonesha waratibu hao.

Mratibu kutoka katika mradi wa GEWE Asha Abdi Makame, anaeleza waratibu hao walitakiwa waanzishe kituo cha taarifa na maarifa ili wakusanye matukio yote ya Wilaya na wapate kuzitoa katika vyombo vya habari.

“Muvitumie vyombo vya habari, ili kuona matendo haya yanaondoka kabisa na sasa tunataka tutanue wigo, tuzishirikishe na shehia nyengine na tayari tumepata mwakilishi kutoka Mkoani”, alisema Mratibu.

Mratibu aliwahamasisha kuyafanyiakazi mafunzo na kuweza kukidumisha kituo cha taarifa na maarifa, kwani kinajenga ushirikiano mkubwa.

Na walitakiwa elimu hizo kuwafikishia shehia nyengine ambazo hazikuingia katika mradi, ili kuweza kuvitokomeza vitendo.

….. Grace kutoka GEWE hakukaa kimya na kusema ili kuweza kuvitokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, hawana budi kuzidisha ushirikianobega katika kituo chao cha taarifa na maarifa.

“Ili vitendo hivi viweze kuondoka kabisa, munatakiwa mufuatilie kwa kina na mufanyekazi kwa pamoja”, alishauru.

Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete Pemba, alisema ili kuweza kupata taifa bora la baadae hapana budi kushirikiana katika kuviondosha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

“Mradi wa GEWE umewezesha kuvipunguza vitendo vya udhalilishaji, hivyo tusichoke kufuatilia kwa umakini na kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya vitendo hivi”, alifahamisha.

Afisa huyo aliwataka waratibu hao kukitunza na kukiimarisha kituo cha taarifa na maarifa na kuwaarifu wao wakati wakiweka mikutano yao, ili kuweza kushirikiana katika kuzitatua changamoto hizo.

Kuwepo kwa kituo cha taarifa na maarifa ni muhimu kwa waratibu wa shehia, ambazo zinaweza kujenga nguvu ya pamoja katika kukusanya matukio na kuyafuatilia.

Mradi wa kukuza Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake GEWE, uliweza kupiga vita vitendo hivyo kwa kutoa elimu katika jamii, ulioanza mwaka 2012 hadi kumalizika mwaka 2014, ambapo umeengezewa muda wa mwaka mmoja ulioanza Disemba 2015 hadi Disemba mwaka huu.
                              

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.