Habari za Punde

RISALA YA WAUGUZI KUADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI 12 MEI 2016

Mheshimiwa  Mgeni Rasmi, Mama Mwanamwema Shein mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi

Mheshimiwa Waziri ya Afya
Mhe. Naibu Waziri wa Afya
Mheshimiwa Katibu mkuu Wizara ya Afya
Mhe.Naibu Katibu Mkuu
Waheshimiwa viongozi mbali mbali wa Wizara ya afya
Wageni waalikwa,
Ndugu Wauguzi wezangu,

Mabibi na Mabwana,
Itifaki imezingatiwa

Assalaam Alaykum,

Awali ya yote hatuna budi kumshukuru M/Mungu kwa kutujaalia kukutana leo hii tukiwa na furaha na afya njema.
Pia kwa niaba ya Wauguzi wenzangu, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mgeni Rasmi kwa kuvunja majukumu yako muhimu na kukubali ombi letu la kujumika na sisi katika hafla hii.

Mhe. Mgeni Rasmi,

Madhumuni makubwa ya kukutana kwetu ni kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani, Siku ambayo amezaliwa muanzilishi wa huduma za Uuguzi duniani Bibi Florence Nightingale ambae alizaliwa kwenye mji wa Florence kule Italy 1820. Mama huyu raia ya Uingereza alileta mageuzi makubwa kwenye kada ya Uuguzi, alitumia muda wake mwingi kuhudumia wagonjwa kwa moyo wa huruma, upendo, imani na ushirikiani mkubwa sana.

Mheshimiwa Mgeni rasmi

Siku hii huadhimishwa kwa kufanya shughuli mbali mbali ili kuimarisha afya ya jamii. Wadau mbali mbali dunia nzima na wanachama wa Baraza la Kimataifa la Wauguzi husherehekea siku hii kwa kufanya shughuli katika jamii kwa kipindi cha wiki nzima. Maudhui ya mwaka huu ni “MUUGUZI NI CHACHU YA MABADILIKO: UIMARISHAJI WA UTHABITI WA MIFUMO WA AFYA”
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kuadhimisha siku hii hapa Zanzibar, Wauguzi wamefanya shughuli mbali mbali katika jamii kwa kutoa huduma za uchunguzi macho, ugonjwa wa kisukari na sindikizo la damu, kufanya usafi wa mazingira na utoaji wa zawadi katika kituo cha Wazee Sebleni na kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini.
Mheshimiwa Mgeni rasmi
Ili kuleta mabadiliko chanya katika afya ya jamii, Siku ya Wauguzi duniani imeanzishwa kuongeza uelewa wa wajibu na majukumu ya Wauguzi pamoja na kuona umuhimu wa kutimiza mahitaji ya Wauguzi duniani kote. Wauguzi duniani kote wametoa mchango mkubwa katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga, kupunguza malaria, kifua kikuu, polio, na kupunguza maambukizo mapya ya VVU. Hivyo wauguzi wakitumiwa ipasavyo wana mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya jamii.
Mheshimiwa mgeni rasmi
Kuongezeka migogoro na wahamiaji duniani, kuongezeka kwa maradhi yasiyo ya kuambukiza (saratani, kisukari, shindikizo la damu), kuongezeka kwa maradhi ya mripuko (kipindupindu, ebola), maafa ya kimaumbile (mafuriko, kimbunga na vita), ongezeko la watu duniani kunaweza kukapelekea kutofikiwa kwa maudhui ya siku ya wauguzi duniani. Hivyo tunaomba Serekali kuimarisha mifumo thabiti ya afya ili kukabiliana na changamoto hizi.
Mheshimiwa mgeni rasmi
Ili kupambana na changamoto nilizozitaja hapo juu, mambo yafuatayo yanahitajika;
·        Kuwepo uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya
·        Kuwepo mfumo madhubuti ya taarifa za maradhi na ufuatiliaji.
·        Kuwepo mfumo bora wa matayarisho na kukabiliana na majanga mbali mbali
·        Kuwepo kwa miundombinu bora ya afya
·        Upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba
·        Kuajiri watendaji kazi waliopatiwa mafunzo katika fani uuguzi na ukunga
·        Uwepo vituo na hospitali zilizowezeshwa kwa vifaa na madawa na kutoa huduma bora
·        Kuwepo bajeti ya kutosha katika huduma za afya
Kuwatumia wauguzi katika kutoa huduma kutapelekea kufikiwa kwa malengo ya afya ya ulimwengu (Universal Health Coverage)

 Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Tunatowa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wadau mbali mbali wa Maendeleo kwa juhudi mbali mbali inazofanya katika kuhakikisha kada ya Uuguzi inaimarika, hii ni pamoja na kupatiwa ufadhili kwa Wauguzi kwenda kujiendeleza kielemu. Kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, jumla wauguzi 198 wamepatiwa fursa ya  kujiendeleza katika mafunzo ya Uuguzi kwa kiwango cha stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu, haya ni mafanikio makubwa katika fani ya Uuguzi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Pamoja na jitihada zote za Serikali na wadau mbali mbali katika kudumisha huduma za afya, fani ya Uuguzi inakabiliwa na changamoto zifuatavyo:
·        Uhaba wa Wauguzi bingwa wa maradhi ya kinamama, maradhi ya watoto wachanga, huduma za dharura na ajali, mifumo ya fahamu na ubongo hali inayopelekea usumbufu mkubwa katika utoaji huduma za kila siku
·        Upungufu wa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wauguzi wanapokuwa katika hospitali za kujifunzia
·        Kupunguwa kwa moyo wa kufanya kazi kwa Wauguzi kulikosababishwa na upungufu wa vitendea kazi za Uuguzi
·        Kazi nyingi wanazofanya Wauguzi kulingana na idadi ya wagonjwa wanaowahudumia ambapo hakuna wiano sawa na viwango vya kimataifa vya utowaji wa huduma za kiuguzi, hii inapelekea huduma zinazotolewa zisiwe na kiwango bora
·        Kukosekana kwa ufadhili kwa Wauguzi wanotaka kujiendeleza ndani na nje ya nchi
·        Mazingira magumu ya kazi yanayochangiwa na ukosefu wa posho mbali mbali na vifaa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Tunaomba  utufikishie kilio chetu kwa wahusika ili utekelezaji wake usiendelee kuchukuwa muda mrefu zaidi. Sisi wauguzi tunaahidi kwamba tutatekeleza wajibu wetu kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni zilizopo ili kimarisha huduma kwa wagonjwa. Aidha tunalaani vikali tabia za Wauguzi wachache wasiofuata maadili na miongozo ya Uuguzi na kuharibu taswira ya Uuguzi kwa jamii.

Mwisho kabisa tunapenda kukushukuru tena kwa kukubali kwako kuwa Mgeni Rasmi wa siku hii adhimu, kwa kweli Wauguzi  sote tumefarijika sana kuwa nasi katika siku hii.
Aidha tunashukuru wadau mbali mbali na wageni waalikwa waliojiunga na sisi na kufanikisha maadhimisho haya.

Ahsanteni.
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.