Habari za Punde

Kamati tendaji ZFA Wilaya ya Magharibi 'A' kukutana na vilabu

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar

Kamati Tendaji ya chama cha soka wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja Jumapili hii (Mei 15, 2016) inatarajia kukutana na vilabu wanachama wa chama hicho katika ofisi za chama hicho iliyopo Bububu Meli 7 njia ya Jeshini wilayani humo.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa chama hicho Zainab Omar Mussa imesema kuwa mkutano huo utakuwa ni malum kwa wadau hao kutambulishana mambo mbali mbali yanayokihusu chama hicho kilichoasisiwa Disemba 27, 2015 baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa wilaya ya Magharibi Unguja mwanzoni mwa mwaka jana.


Zainab amesema toka muda huo Kamati hiyo ilikuwa ikitekeleza majukumu yake hivyo baada ya kukamilisha mambo ya msingi yakiwemo ya kupata ofisi ya muda na kukabidhiwa mkabrasha ya vilabu wanachama wa wilaya hiyo, wameona umuhimu wa kukutana na vilabu hivyo ili kujadiliana mambo mbali mbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi wilayani humo.

Ameongeza kuwa pamoja na kukutana na baadhi ya vilabu Jumamosi ya wiki iliyopita, Kamati hiyo imeona umuhimu wa kukutana nao tena ili kuwapa taarifa mbali mbali na kupata maoni yao juu ya namna bora ya uendeshaji wa chama hicho na kuwataka viongozi wa vilabu hivyo kufika kwa wingi katika mkutano huo utakaoanza saa 3:00 asubuhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.