Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk.Shein Awaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                   24 Mei, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao aliwateua hapo jana.

Walioapishwa ni Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mheshimiwa Vuai Mwinyi Mohamed ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kabla ya uteuzi huo Mheshimiwa Ayoub alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ na Mheshimiwa Vuai alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja.

Sherehe hiyo fupi iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.

Wakuu wa wilaya walioapishwa ni Hassan Ali Kombo ( Kaskazini ‘A’), Issa Juma Ali (Kaskazini ‘B’), Bi Marina Joel Thomas (wilaya ya Mjini) na Silima Haji Haji (Magharibi ‘B’).

Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja Bi Mashavu Sukwa Said, Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Kitwana Mustafa na Bi. Salama Mbarouk Khatib Wilaya ya Chake Chake Pemba.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa Said Hassan Said, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Kadhi Mkuu wa Zanzibar sheikh Khamis Haji.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mheshimiwa Khatib Abdulrahman Khatib.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.