Habari za Punde

UVCCM Zanzibar yawataka viongozi kutekeleza ahadi

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.


UMOJA wa vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar umewataka vijana wa umoja huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja  kuwakumbusha viongozi waliopo madarakani kwa sasa kutekeleza kwa haraka ahadi walizotoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika mwaka huu.

Umesema vijana wana haki ya kutumia vikao halali vinavyokubalika katika utaratibu wa kiuongozi ndani ya UVCCM kuwakumbusha viongozi wa chama hicho kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa kwa wananchi wa Zanzibar.

 Akizungumza katika ziara ya UVCCM katika Mkoa huo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrissa huko katika ofisi ya jimbo la Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Unguja.

Alifafanua kwamba CCM ni chama chenye viongozi makini wanaoahidi na wakatekeleza hivyo hakuna haja ya vijana kuendelea kulalamika badala yake wafuate utaratibu kuwakumbusha wahusika watekeleze majukumu yao kwa wananchi.

“ Vijana kumbukeni kuwa kwamba nyie ndiyo mliowaweka madarakani hao Marais, wabunge, wawakilishi na madiwani hivyo msiwaogope kuwakumbusha kwa kufuata taratibu wajibu wao wa kutekeleza ahadi zao kwenu na wakikataa basi rudini kwetu mtwambie na tutayafanyia kazi.”, alisema Idrissa.

Idrissa alisisitiza vijana hao  kuendelea kuwa wamoja ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali zilizopo katika chama na serikali iliyopo madakani.


Alisema umoja na mshikamano ndiyo njia pekee itakayowawezesha vijana kubuni fursa za maendeleo  kwa lengo la kujikwamua katika wimbi la umasikini nchini.

Alisema vijana ndiyo kundi kubwa katika jamii linalopambana na vikwazo tofauti katika kusimamia maslahi ya CCM lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa ajira,elimu,nyenzo na ukosefu wa kipato mambo yanayotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu na mamlaka husika ndani ya Chama na serikali.

“ Nakuombeni vijana wenzangu tuendelee kuwa wamoja katika kuimarisha na kusimamia maslahi ya CCM kwani Zanzibar bila ya kuwa na vijana imara na wazalendo nchi yetu itachelewa kupata maendeleo endelevu.

Pia vijana tunatakiwa kuwa wabunifu wa kuangalia na kuzitumia fursa zilizotuzunguka ili kupunguza umasikini unaotukabili katika maisha yetu ya kila siku.”, alisema Idrissa na kuongeza kwamba UVCCM itaendelea kuwa daraja la kuwavusha vijana kufikia katika kilele cha maendeleo.

Akizungumzia changamoto ya ajira, Idrissa alisema suala la ajira katika nchi zinazoendelea bado ni tatizo kwani hakuna serikali yenye uwezo wa kutoa ajira kwa wananchi wote bali kinachofanyika ni kufungua milango kwa Wawekezaji, sekta binafsi pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiria mali ili viweze kutoa ajira badala ya kutengemea serikali pekee.

 Kaimu Naibu Katibu Mkuu Idrisa, alilitaja lengo la ziara hiyo kuwa ni kuwashukru wananchi wa Zanzibar hasa makundi ya vijana walioshiriki katika mazingira tofauti kuiweka madarani serikali ya CCM inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.

Alisema kwamba ushindi wa CCM uliopatikana  katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliopatikana katika Machi 20, mwaka huu na kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 91 dhidi vya vyama vya upinzani vilivyoshiriki katika uchaguzi huo.

Alifafanua  ushindi wa chama hicho umetokana na ukongwe wa Demokrasia iliyoimarika ndani na nje ya chama hicho katika utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo kwa wananchi wote.

Alisema baada ya kumalizika uchaguzi mkuu kilichobaki ni kuimarisha chama hicho ili kiendelee kuwatumikia wananchi kwa vitendo.

Nao vijana wa umoja huo kwa nyakati tofauti wameahidi kuifanyia kazi miongozo waliyopewa katika hafla hiyo na kusema kwamba wataendelea kuwa waumini wa kweli wa CCM kwani ndiyo chama pekee kinachojali maslahi mapana ya vijana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.