Habari za Punde

Aina za watu kwenye mfungo wa Ramadhaan

Ndugu yangu katika imani. katika mwezi huu wa Ramadhaan tunatarajia kuwa na aina nne ya watu.

Aina ya kwanza

Wale ambao hawatotaka kufunga kabisa mwezi huu. Mwezi wa Ramadhaan na mwezi wa kawaida ni sawa huoni tofuati yoyote kwao. Bado tuna ndugu zetu Waislamu lakini kwao kufunga ni ibada nzito kwao.

Ndugu yangu katika Imani ninakunasihi usijaribu kuwa miongoni mwa watu wa aina hii hasa kama Allaah Azza wa Jall amekujaalia uwezo wa kufunga na si mgonjwa wala kuwa na udhuru unaotambulika kisheria.

Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amesema: Mtu yeyote atakaeacha kufunga Ramadhaan pasi na kuwa na udhuru au ugonjwa, hata akifunga dahari - siku zote katika maisha yake ( ili kuilipa ile siku aliyoacha kufunga) basi haitotosheleza. Bukhaari

Hatari zaidi inaweza kuja endapo huyu mtu ameacha kufunga kwa makusudi na kwa inda na inadi huku akila bila ya woga. Huyu ndugu yangu katika Imani ni Kaafir! Ametoka katika mila ya Uislamu kwa kuikana hadharani mojawapo ya nguzo katika nguzo tano za kiislam.


Ewe Mola! usitujaalie kuwa miongoni mwao

Aina ya pili

Ni wale watakaofunga Ramadhaan hii si kwa ajili ya Allaah, Azza wa Jall, bali ni kama utamaduni na mazoea kwamba mwezi huu waislamu huwa wanafunga na mimi nifunge. Aina hii ya watu mwezi wa Ramadhaan kwao si mwezi wa Ibaada na kukithirisha kumuabudu Allaah Azza wa Jall na hata wakitekeleza ibada hizi basi huwa ni kwa sababu ya kuona haya ili wasisemwe au kuonekana hawafanyi ibaada.

Hivyo hata wakisali huwasikii wakiomba maghfira wala toba na kundi hii hupenda kunun’gunika na kulalama mno wakati wa mfungo kwani wanayoyafanya si kwa jili ya kupata radhi zake Allaah Azza wa Jall.

Ewe Mola! usitujaalie kuwa miongoni mwao

Aina ya tatu


Ni wale watakaoufunga kama waislamu wengine ila hawakufahamu malengo halisi ya kufunga nayo ni kuipata Taqwa (kumuogopa Allaah Azza wa jall).

Kundi hili huwa halina mabadiliko yoyote katika maisha yao kabla na wakati wa kufunga isipokuwa tu wamekaa na njaa na kuwa na kiu.

Hawa amewataja Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam katika hadithi kwa kusema: Haingii akilini kwa mwenye kufunga (kisha) hadhi yake iwe ni kukaa na njaa au kiu tu. Na haingii akilini kwa mwenye kusimama usiku na kusali (kisha) iwe hadhi yake ni kukesha tu” Attabraani

Ewe Mola! usitujaalie kuwa miongoni mwao

Aina ya Nne

Ni aina ya ambao nnajiombea mimi, wewe unaesoma na kila Muislamu awe miongoni mwao ni ile ya wanaofunga kikweli na kutaraji kupata malipo kutoka kwa Allaah Azza wa Jall huku wakiikamilisha funga yao na kujiweka mbali na kila linaloweza kuharibu funga yao, wakiomba dua, wakisoma Qur’aan , wakifanya ibada za ziada, wakimkumbuka Allaah Azza wa Jall, wakihama nyumba zao kwa muda na kufanya Misikiti ndiyo nyumba zao wakikithirisha ibada. Hawa ndio Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amewaahidi kuwa furaha mara mbili. Mara ya kwanza wanapofungua na kufutari na furaha ya pili ambayo ni kubwa zaidi watakapokutana na Mola wao. Allaahu Akbar!

Ewe Mola tujaalie tuwe miongoni mwao Aamiyn.

Ramadhaan Mubaarak

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.