Habari za Punde

DK. SHEIN AVITAKA VYOMBO VYA HABARI VYA SMZ KUJENGA USHIRKIANO KULETA UFANISI

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                               09Juni, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na kuzungumza na watumishi wa vyombo vya habari vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuhimiza
ushirikiano na mahusiano mazuri kazini ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Katika mkutano huo ulioshirikisha pia viongozi na 
watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Dk. Shein alisisitiza 
umuhimu wa vikao vya mara kwa mara katika sehemu za kazi ili kujenga mahusiano hayo ambayo ni muhimu katika kuleta ufanisi mahala pa kazi.

“katika mahala pa kazi utawala na uongozi unahitaji 

vikao kwani ni muhimu katika kujenga mahusiano 

kazini na hatimae kuweza kufikia malengo” Dk. Shein 

alisema.

Aliwaeleza watumishi hao kutoka Shirika la Magazeti 

la Serikali linalochapisha gazeti la Zanzibar Leo, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Redio na 

Televisheni pamoja na Idara ya Habari MAELEZO kuongeza juhudi na kufanyakazi kwa weledi kwa kuwa wananchi wana imani kubwa na vyombo hivyo vya serikali hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanakidhi matarajio ya wananchi.

Dk. Shein alivitaka vyombo hivyo vya habari vya serikali kwenda na kasi ya mabadiliko kwani wananchi wana hamu kuona vyombo hivyo vinafanya vizuri zaidi.

“Tunataka mabadiliko ya viongozi, watendaji na watumishi ili kujenga timu moja makini yenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza majukumu ya wizara na idara zake kikamilifu” Dk. Shein alisema na kudokeza kuwa mabadiliko aliyoyafanya katika uongozi wa wizara hiyo lengo lake ni kuleta ufanisi na 
kuhakikisha malengo yanafikiwa.

Kuhusu maslahi ya watumishi wa vyombo hivyo vya habari Dk. Shein alisisitiza kuwa serikali inayafanyia kazi kama ilivyo kwa watumishi wengine wa serikali lakini alikiri kuwa kumekuwepo na ucheleweshaji katika kutekeleza maagizo ya Serikali katika suala hilo kwa upande wa wizara hiyo.

Kwa hivyo aliiagiza wizara kutekeleza maagizo hayo mara moja ikiwemo suala la muundo wa utumishi (sheme of service) kwa ZBC na maslahi mengine ya watumishi wa taasisi hizo za serikali.

“Lazima muundo wa utumishi uwepo ili mtumishi ajue maslahi yake, wajibu wake na nafasi yake katika shirika na hapo ndio tutaweza kuwajibishana” Dk. Shein alieleza.

Alitumia fursa hiyo kuvipongeza vyombo hivyo vya habari kwa kazi nzuri inayofanya kwa jamii pamoja na kuwa vinazowakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Dk. Shein aliwawahakikishia watumishi hao kuwa serikali inatambua umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wake hivyo kila itakapowezekana watumishi watapewa fursa za mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi na mengine katika sehenu za kazi.

Katika mkutano huo Mheshimiwa Rais alirejea tena wito wake wa kuwataka viongozi wa serikali wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ili kutangaza shughuli za serikali.

Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi wa vyombo hivyo vya habari vya serikali kuimarisha nidhamu kazini ikiwemo kusoma na kuzifahamu vyema sheria na kanuni za kazi pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Habari, 

Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma lieleza kuwa uongozi mpya wa wizara tayari umeonana na kuzungumza na watumishi wa Idara na vitendo mbalimbali vya wizara ili kufahamu changamoto zinazowakabili.

Alibainisha kuwa mojawapo ya njia ya za kukabiliana 

changamoto hizo ni kutumia vizuri rasilimali zilizopo 

na kusimamia mapato. Katika mkutano huo 

watumishi walieleza changamoto mbalimbali 

zinazowakabili ikiwemo uchakavu wa vifaa, usafiri na 

maslahi duni.  


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

                                                

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.