Habari za Punde

Fainali za Kombe la Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu Zanzibar

Na Othman Khamis OMPR.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Rashid Ali Juma alifikia hatua ya kuweweseka mchana kweupe kufuatia Timu aliyokuwa akishabikia kuchezea kipigo cha Paka mwinzi katika Finali ya Mashindano ya Tamasha la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taaluma ya Elimu ya Juu  Zanzibar { Zahilfe } zilizomalizika katika Uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar.

Waziri Rashid akiwa shabiki wa wanandinga wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka aliendelea kupata kigugumizi pale mpinzani wake Mtangazaji Mkongwe Suleiman Juma Kimea kuvimba kichwa wakati Timu aliyoshabikia ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu ikiibuka kwa ushindi wa Goli 4-2.

Mgeni rasmi wa hitimisho la Tamasha hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionyesha makeke yake kwa kushabikia Timu itakayoshinda kwenye mtanange huo wa Finali ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taaluma  ya Elimu ya Juu Zanzibar.

Mashabiki wa soka wa pande zote mbili walishindwa kukaa kwenye majukwaa mara tu baada ya Timu hizo kuingia kiwanjani kuanza kwa pambano hilo kubwa lililoacha simulizi katika viunga vya Mji wa Zanzibar huku Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pemba Juma akifuta machozi kuungana na Waziri Rashid baada ya Timu yao kufungwa.

Zanzibar Univesity ilianza kuonyesha umahiri wake wa kutandika kabumbu na katika Dakika ya 13 ikajipatia goli la kwanza lililowekwa kimiani na mchezaji machachari Awadhi Othman aliyeibuka kuwa mchezaji bora katika mashindano hayo.

Goli la Pili la Zanzibar Univesity lilifungwa na mchezaji Issa Ahmad katika Dakika ya 18 wakati mchezaji Said Bakari akaipatia goli la Tatu katika dakika ya 29 lililodumu hadi kuingia kipindi cha mapumziko.

Katika kipindi cha Pili cha mchezo huo wanachuo cha Uongozi wa Fedha walianza kujitutumua na kupata Goli la kwanza katika dakika ya sita ya kipindi hicho mfungaji akiwa Saleh Suleiman.

Goli hilo liliwaamsha wachezaji wa Zanzibar Univesity na kuhitimisha Goli lao la  Nne lililofungwa na mchezaji Hassan Hemed ambapo dakika ya 25 ya kipindi cha lala salama mchezaji Mussa Ali Omar akaipatia timu yake ya Chuo cha Uongozi wa Fedha Goli la pili.

Hadi kumalizika kwa pambano hilo la fainali ya Tamasha la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taluma ya Elimu ya Juu Zanziba,r  Zanzibar Univesiry ilishinda kwa goli Nne dhidi ya wapinzani wao Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka walioibuka na Goli Mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi zawadi ya Kikombe pamoja na fedha Taslimu shilingi Milioni Moja kwa Zanzibar University ambae ndie mshindi wa mashindano hayo wakati Chuo cha Uongozi wa Fedha wakaibuka washindi wa Pili.

Pia alikabidhi zawadi kwa  vyuo  vilivyoshinda katika michezo mbali mbali ya mashindano hayo pamoja na mchezaji bora ambae ni Awadh Othman wa Zanzibar Univesity, Kipa bora Saleh Burhan wa Zanzibar Univesity wakati muamuzi Bora alikuwa Abdulla Yussuf Abdulla.

Akiyafunga mashindano ya michezo hiyo ya Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimua ya Juu Zanzibar { ZAHILFE } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Wanamichezo na Vijana Nchini kuendelea kuwakataa Viongozi wote wenye tabia ya kutaka kuwatumia wajiingize katika vitendo viovu vinavyohatarisha  amani ya Nchi na hatimae  huviza maendeleo ya Taifa.

Alisema kazi kubwa inayowakabili mbele yao kwa sasa wanamichezo hao ni kuhakikisha wanadumisha Amani na kamwe wasikubali kugawanywa kwa misingi ya dini, kabila wala itikadi za kisiasa.

Alisema  kwa kuwa michezo huzalisha watu wasikivu wenye nidhamu na watiifu, Wanamichezo Vijana wanahitaji kujengwa kimaadili na nidhamu ili waweze kuendana na hali ya maisha ya ushindani yatakayokuwa yakiwakabili wakati watapokuwa viongozi wa baadae.

Alieleza kwamba nidhamu inamuwezesha mtu kufanya kazi zake kwa  mpangilio mzuri unaofuata taratibu zote za kazi kwa wakati ambazo ni njia ya uhakika ya kufikia malengo na kupata elimu bora.

Balozi Seif  alisema katika kutekeleza sera ya maendeleo ya michezo nchini, kupitia Tamasha hilo Taasisi za michezo zimeweza kubaini vipaji vipya vya michezo na hatimae kuwapata wachezaji bora sambamba na kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar za kuboresha michezo nchini.

Aliwataka wanamichezo wote kuwa na nidhamu na kuviendeleza vipaji vyao ili Taifa liweze kupata timu makini ambazo zitaweza kushiriki kwa kujiamini katika mashindano yoyote ya Kitaifa na Kimataifa.

Balozi Seif alifahamisha kwamba michezo hujenga ushirikiano, huleta furaha, burdani, afya, ajira sambamba na kuchangia pato la Taifa kutokana na baadhi yao waliobarikiwa kuwa na vipaji hununuliwa katika Timu za Kimataifa na kupatikana kwa fedha za kigeni.

Alisema michezo pia husaidia kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, ukahaba, wizi, ulevi na hivyo wanamichezo kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na Maambukizi ya virusi vya ukimwi yanayoimarisha maisha  mazuri na ya furaha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Uongozi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho hilo kwa jitihada zao za kuwaunganisha Wanafunzi pamoja kwenye michezo mbali mbali.

Balozi Seif alisema kwa kuwa michezo ina gharama  kubwa upo umuhimu wa kuwapongeza wadhamini na wahisani waliochangia na kufanikisha mashindano hayo muhimu kwa ustawi wa maandalizi ya kuibua vipaji vya wanamichezo  hapa nchini.

Katika kuunga mkono jitihada za Shirikisho hilo la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameahidi kusaidia Kompyuta moja na mashine ya Fotokopi ili kutanzua changamoto inayolikabili Shirikisho hilo.

Balozi Seif pia akaahidi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar kulipatia Ofisi ya kudumu Shirikisho hilo ili liondokane na Tabia ya Watendaji wake kuendesha Ofisi ndani ya mikoba.

Mapema akisoma risala ya wanamichezo hao mmoja wa Viongozi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya juu Zanzibar Abdulla Ramadhan alisema shirikisho hilo limeanzishwa mwaka 2009 kwa lengo la kuendeleza Sera ya Michezo kupitia Tamasha linaloendelea kila mwaka.

Abdulla Ramadhan alisema Wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na wale wa msingi na sekondari hapa n chini wamefarajika kuona sera ya michezo Nchini hivi sasa imeanza kutoa muelekeo na kuanza kusonga mbele kila mwaka.

Akitoa salamu kwa niaba ya wachangiaji na wafadhili wa mashindao hayo Mwakilishi kutoka Benki ya Afrika Juma Burhan Mohammed ambae ni Menaja wa Bednki hiyo Tawi la Zanzibar alisema michezo katika ulimwengu wa sasa sio burdani tuu lakini inasaidia afya njema za wanamichezo.

Burhan alisema ushirikiano wa pamoja kati ya wanamichezo, wazazi na washirika wa michezo ndio njia pekee inayoleta umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa Jamii katika maeneo yote iwe siasa, maendeleo na hata uchumi.

Meneja huyo wa Benki ya Afrika Tawi la Zanzibar alieleza kwamba Benki hiyo imejikita katika kuunga mkono harakati za Kijamii nchini ikiwemo michezo pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Alisema katika kuthibitisha hayo Benki ya Afrika imetoa upendeleo wa kumfungulia Akaunti Mchezaji bora kwa kumuwekea hakiba ya shilingi Laki Moja na Mfungaji Bora kumuwekea hakiba ya shilingi 50,000/-  kwenye mashindano hayo ya Tamasha la Mashindano ya michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Ewlimu ya Juu Zanzibar { ZAHILFE }.

Akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif kuifunga michezo hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma alisema hamasa ya vyuo vikuu katika kuimarisha sera ya Elimu kwa sasa inaanza kuelekezwa katika skuli za Msingi na Sekondari.

Waziri Rashid alisema hatua hii  itakayoratibiwa kwa pamoja na Wizara zinazosimamia Michezo na Elimu  itasaidia kuendeleza sera ya michezo katika dhana nzima ya kuinua sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Ujumbe wa Tamasha hilo la Mashindano ya Michezo ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar { ZAHILFE } unasema :- Elimu bora pamoja na mazingira safi na salama ndio njia kuu ya kupambana na Kipindupindu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.