Mheshimiwa Spika,
Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kwa mara nyengine tena kufika na
kuweza kukutana mbele ya Baraza lako Tukufu tukiwa wazima na wenye afya njema,
kwa lengo la kujadili mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo na ustawi wa nchi
yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika,
Aidha,
napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele
ya Baraza lako Tukufu ili niweze kuwasilisha kwa niaba ya Kamati ya Mawasiliano
na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Hotuba ya Maoni kuhusu Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Mheshimiwa Spika,
Pia, napenda kutoa shukrani zangu kwa Waziri
na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na
Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na Watendaji wote wa Wizara hii kwa
ushirikiano mkubwa walioutoa katika kufanikisha kumalizika kwa kazi hii ya
Kamati. Kwa kweli ushirikiano wao umetupa moya sana, na wameonyesha nia ya
kuendeleza yale mazuri waliyoyakuta hapo Wizarani na pia kuyaondoa yote
yanayorejesha nyuma maendeleo ya Wizara yao nasisi tunaahidi kufanyakazi nao
kwa pamoja ili malengo waliyojiwekea yaweze kufikiwa.
Mhesimiwa Spika,
Sasa naomba nichukue nafasi hii, kuwashukuru
kwa dhati Wajumbe wa Kamati yangu kwa michango yao muhimu waliyoitoa wakati
tulipokuwa tukijadili na kupitia Bajeti hii, ambapo mawazo na mapendekezo yao
yamewezesha leo hii kufika hapa na kuweza kuwasilishwa mbele ya Baraza lako
Tukufu na hatimae kujadiliwa na kupitishwa kwa
lengo la kuiwezesha Wizara kutekeleza malengo yake iliyojipangia kwa
mwaka huu. Naomba sasa kwa ruhusa yako niwataje Wajumbe pamoja na Makatibu wa
Kamati yetu ya Mawasiliano na Ujenzi kama ifuatavyo:-
1. Mhe.
Hamza Hassan Juma Mwenyekiti
2. Mhe.
Suleiman Sarahan Said M/
Mwenyekiti
3.
Mhe. Abdalla Ali Kombo. Mjumbe
4.Mhe.BahatiKhamis Kombo. Mjumbe
5.Mhe. Khadija Omar Kibano Mjumbe
6.Mhe.Mohammedraza Hassanaali Mjumbe
7.Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa Mjumbe
8.
Mhe. Nassor Salim Ali Mjumbe
9.
Mhe. Said Omar Said Mjumbe
10.Ndg. Fatma Omar Ali Katibu
11.Ndg.Himid Haji Choko Katibu
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya utangulizi huo sasa napenda nitoe Maoni ya Kamati kuhusiana na Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka
wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika,
Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na
Usafirishaji ni moja ya Wizara muhimu
katika nchi yetu kutokana na ukweli kwamba inasimamia sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, ambazo ni Sekta
ya Ujenzi, Sekta ya Usafiri wa Baharini, Sekta ya Usafiri wa Anga, Sekta ya Usafiri
wa Nchi Kavu pamoja na Sekta ya Mawasiliano. Aidha, baada ya maelezo hayo
naomba sasa niaze na uchambuzi wa Programu zinazosimamiwa na Wizara hii.
PROGRAMU
YA MIUNDOMBINU NA HUDUMA ZA USAFIRI WA BARABARA
Mheshimiwa Spika,Kamati
yangu imepata nafasi ya kufanya ziara ya siku mbili Unguja na Pemba kabla ya
kuipitia Bajet hii ya mwaka 2016/17, pamoja na ufinyu huo wa muda kamati
ilijifunza mambo mengi ambayo ni changamoto za Wizara na kwa kweli iko haja ya
kuweka mipango madhubuti ili kuhakikisha kazi za Wizara zinaenda kwa kasi kwa
mujibu walivyojipangia wao bila ya vikwazo vyovyote. Aidha, Kamati yangu
imejipanga kuisaidia sana Wizara katika kipindi chote ambacho Mhe Spika
umetutuma tuisimamie. Pamoja na hayo Kamati yangu imeipitia Bajeti hii katika
mazingira magumu haswa ukizingatia Wajumbe wangu wengi ni wageni hapa Barazani
lakini pia hawajawahi kuikagua Wizara nzima pamoja na kukutana na wafanyakazi
ili kujua changamoto zao ili kamati ikaweza kuisaida Wizara ipasavyo, lakini
pamoja na hayo nawashukuru Wajumbe wangu kwa umahiri wao jinsi walivyoweza
kutoa michango yao kwa Wizara kupitia uzoefu wao na msaada mkubwa wa watendaji
wao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hii, lakini naamini mwakani wataweza
kuisaidia sana Wizara ili kuona changamoto zao zinageuka kua chachu ya
maendeleo kwao.
Mheshimiwa Spika,Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kupitia
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kukamilisha Mradi wa Ujenzi
wa Barabara mbili kati ya tatu kwa upande wa Pemba zenye urefu wa kilomita
30.2. Barabara hizo ni barabara ya Wete - Konde na Wete - Gando. Na bado
barabara moja ya Wete -Chake Kwa kweli kukamilika kwa Mradi huu kunaondoa ile
adha ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaotumia barabara hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati
yangu imetembelea Mradi huo na kushuhudia wenyewe kazi kubwa iliyofanywa na
Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Co. Limited (MECCO), iliyopewa Kandarasi ya Kujenga barabara
hizo. Kwa kweli barabara hizo zimejengwa kwa kiwango kinachohitajika haswa kwa
wakati huu tulionao. Kamati inaamini kwamba Serikali haikufanya makosa kuiteuwa
Kampuni ya MECCO kuipa kazi hii, kwani kiwango cha ubora wa barabara hizo ni
kikubwa sana na cha kupigiwa mfano kwa hapa Zanzibar. Pamoja na mafanikio hayo
lakini bado kuna barabara hii ya Wete –Chake ambayo ni sehemu moja ya barabara
hizo haijaanza kujengwa hadi leo ili kukamilisha mradi huo wa barabara tatu za
Pemba kutokana na Serikali kuchelewa kutoa pesa za fidia wananchi ambazo
zinakadiriwa kufikia karibu Bilioni moja na milioni mia saba (1.7 Bil), ambazo zingelimuwezesha
mjenzi kuendelea na kazi hiyo iliyobakia, kwakweli suala hili limeisikitisha
sana Kamati yangu kwani kutokana kuchelewa kwa mradi huu kunaweza kuongeza
gharama za mradi huo kuliko bajeti iliyopangwa hasa kutokana na gharama za
vifaa kupanda bei siku hadi siku ,lakini baada ya kuangalia bajeti kuu ya
Serikali ya mwaka huu wa 2016/17 tumeziona pesa hizo 1.7 Bilioni zimetengwa kwenye bajeti ili kumalizia malipo hayo ya
fidia kwa wananchi ili mjenzi aendelee na kazi iliyobaki ya kukamilisha bara
bara hiyo ya Wete Chake,
Mheshimiwa Spika, Kamati
yangu inaitaka Wizara ya fedha kuipatia Wizara pesa hizo mara tu baada ya
kuipitisha Bajeti hii kwani sio kwamba ikishalipwa fidia kua kazi hiyo itaanza
hapohapo, kwani hapo kutakua na kazi za kuanza kuondoa baadhi ya nyumba na
vipando mbali mbali vilivyomo katika eneo la mradi kazi ambayo pia itachukua
muda, kwa hiyo kutolewa mapema kwa pesa hizo kutaharakisha ukamilishaji wa
ujenzi huo ambao umeshakua wa muda mrefu ambao uliasisiwa tangu mwaka
2009.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo,
Kamati yangu kwa masikitiko kabisa, inakujuiilisha kwamba bado Kampuni hiyo ya
MECCO licha ya kuing’arisha Pemba kwa Ujenzi wa barabara hizo, bado haijakamilishiwa
malipo ya kazi hiyo ya Kujenga barabara hizo. Ambapo kampuni hiyo inadai karibu
3 mil usd na Tshs 1.7 wakati kazi wameshamaliza zaidi ya miaka mitatu nyuma,
jambo ambalo linaisababishia Serikali kujiongezea mzigo wa madeni pamoja na
riba ya ucheleweshaji wa malipo ya mradi (Interest). Ambapo mzigo huo
huwabebesha wananchi bila sababu yoyote.
Mheshimiwa Spika, Lakini
pamoja na hayo tunamshukuru Mhe Waziri kwa kuiahidi Kamati kua suala hilo
limeshafika ofisini kwake na ameshalitolea maelekezo ufanyike uhakiki wa madai
hayo na mwenye haki yake apewe, hii Imetupa moyo Kamati kwani jambo ambalo
limekwama kwa muda zaidi ya miaka mitatu Waziri ameahidi kulitatua kwa wakati
muafaka ili kazi zisikwame kwa sababu zisizo za msingi.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na kadhia hii ya ucheleweshaji wa malipo hasa kwa pesa zinazotoka kwa Wafadhili
Kamati yangu tunamshauri Waziri wa Fedha kuwateua maafisa katika kila mradi ili
kuwepo Wizarani kwa muda wote wa mradi ili kuona na kujua changamoto
zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwasilisha Wizara ya
fedha ili kuondoa usumbufu wakati wa malipo, kwani imeonyesha wakati mwingine
kunatokea kutokuaminiana kwa baadhi ya watendaji baina Wizara ya Fedha yaani
mlipaji (PAYEE) na Wizara yaani
mwenye mali (CLIENT), jambo hili
tunaona sio sahihi kwani hao wote ni
watendaji wa Serikali na wanafanyakazi ya wananchi kwa maendeleo yetu sote sio
ya mtu Fulani. Aidha, tatizo hili sio kwa Wizara hii tu bali ni kwa miradi yote
inayopatiwa pesa kutoka kwa wahisani au mikopo ya nje. Kwani Wizara inapojipangia
malengo ya mwaka mmoja basi huhitaji watekeleze kama walivyopanga na kusiwe na
vikwazo, hasa kwa utaratibu wa sasa wa Bajeti
inayozingatia Program (PBB) maana
yake mipango iende kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Aidha, juhudi za Serikali za kuwasogezea
maendeleo wananchi wake, ilijenga Barabara tano za ndani za Mkoa wa Kaskazini
Pemba chini ya Ufadhili wa Millenium Challenge Accout (MCC-T) na kazi hii ilipewa
Kampuni ya H. Young ya Kenya. Ujenzi
wa Barabara hizo zilizojengwa kwa
kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 35 ambao ulijumuisha barabara za Kipangani
- Kangagani, Chwale – Kojani, Mzambarau Takao - Pandani hadi Finya, Mzambarau
Karim – Mapofu, Bahanasa – Daya na Makoongeni – Mtambwe.
Mheshimiwa Spika, Kamati
yangu ilibahatika kuzitembelea barabara hizo na kugundua changamoto kadhaa ikiwemo
dosari zilizojitokeza muda mfupi tu, baada ya kukamilika ujenzi wa barabara
hizo mara tu baada ya kukabidhiwa kwa Serikali. Dosari hizo ni pamoja na nyufa
na mmong’onyoko wa udongo katika sehemu mbali mbali za barabara hizo. Aidha
Kamati yangu imegundua kwamba baada ya kusikiliza ushauri wa jopo la wataalamu
, Mwajiri (MCA-T) pamoja na Wizara
kwa ujumla waliamua kufanyika kwa matengenezo kadhaa ili kuzihami barabara hizo na kazi hii ilikabidhiwa tena kwa Kampuni ya
MECCO kwa gharama ya Dola za Kimarekani
Milioni 1.68.
Mheshimiwa Spika, Kamati
yangu baada ya kuona changamoto
kwenye barabara hizo tunaishauri
Serikali kabla ya hizi kampuni hasa za ujenzi wa Barabara kuzipa kazi za ujenzi (TENDER) basi ni vyema zile (tender board) kuangalia vizuri vigezo (B.O.Q) pia na uzoefu wa kazi na
kujiridhisha kwa kuona kazi zilizofanywa
na kampuni hizo na sio kuja kujifundishia kazi hapa kwetu Mheshimiwa Spika, kwani
pesa zinazotumika, ni pesa za wananchi kwa hiyo zinapaswa kutumika vizuri.
Mheshimiwa Spika, Hili nnalisema kwani kwa uzoefu Mhe. Rais wetu wa sasa wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. (JOHN POMBE
MAGUFULI) wakati akiwa Waziri wa Miundombinu wa Jamhuri ya Muungano aliwahi
kuwafukuza kazi wakandarasi wasiokua na viwango na pia kukataa kuzipokea
barabara ambazo zilizokua zimejengwa chini ya kiwango, hii ilimjengea sana sifa
wakati huo na ndio maana wananchi wanamkubali kwa umakini wake na umahiri wake
wa kutokua na muhali wakati anapokua kazini na hadi hii leo amekua Raisi bora
Duniani na kila pahala amekua akisifika. Kwahiyo, Mhe. Waziri wetu tunakuomba
uige mfano wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli usikubaki kuipokea kazi ambayo
itakayokua chini ya kiwango na pia usiikubali Kampuni yoyote ambayo haina
uzoefu wa kufanya kazi na kuja kujifundishia kwenye Wizara yako, kwani ndani ya
Wizara yako huko nyuma zipo Kampuni zilipewa kazi zikashindwa njiani na
nyingine zimekimbia na hadi leo kazi zimelala na kurejesha nyuma maendeleo ya
nchi yetu na ukiangalia historia za kampuni hizo ni zile zilizoletwa na wajanja
kwa tama zao na kuitia hasara Serikali.
Vile vile, Kamati yangu itakusaidia kukupa
nguvu pale utakapoamua kuifukuza
kazi kampuni yeyote ya mkobani.
Mheshimiwa Spika, chi
nyingi za kiafrika zinakabiliwa sana na changamoto hii ya kujengewa barabara
zilizo chini ya kiwango na kuzibebesha mzigo Serikali zao, kwa hili sisi
hatutolikubali.
heshimiwa Spika, Pia, Kamati yangu ilistushwa sana na kiwango
cha pesa nyingi sana zilizolipwa kwa fidia kwenye ujenzi wa barabara hizi za
Pemba karibu Tshs. ( 6.Bil ) Kiwango
hiki ni kikubwa sana ambapo Kamati
ilipoiuliza Wizara wakasema haikuhusishwa na ulipaji wa fidia hizo, suala hili
kwa kua Kamati haijakusudia kuundwa kwa kamati teule kulifuatilia suala hili
tunaitaka Wizara ilifanyie kazi na ituletee ripoti kamili ya uhakika na uhalali
wa malipo hayo kwani ukiangalia katika maeneo hayo hakuna majumba mengi kiasi
hicho ambapo gharama ingekua kubwa kiasi hicho. Kwani kama hatukua makini hasa
kwenye masuala ya fidia basi miradi itakua na gharama mara mbili ya bajeti
halisi kutokana na ukubwa wa fidia hizo zinazotolewa nasema haya kwani hadi hii
leo bado kuna malalamiko ya wananchi kuhusu fidia hizo.
Mheshimiwa Spika, Hadi
Kamati yangu inapitia Bajeti ya Wizara hii, kazi hii ya marekebisho ya barabara
hizo ilikua inaendelea ingawa kulikua na madai ya kujitokeza vipingamizi kadhaa
kama vile idara zenye dhamana ya rasilimali zisizohamishika kutoa pingamizi ya
kuchimba na kusafirisha kifusi na mawe kwenda eneo la kazi. Kutokana na suala
hili tunaziomba taasisi zote za Serikali kutoa mashirikano wakati wa kutekeleza
miradi bila ya kujali mradi unatekelezwa Wizara gani kwani zote ni taasisi za
Serikali hiyo, tofauti ni mgawanyo wa majukumu tu.
Mheshimiwa Spika, Kutokana
na kadhia hii na nyenginezo zinazofanana na hii, Kamati inaishauri Serikali kwamba,
wakati wa utekelezaji wa Miradi Mikubwa
kama hii, kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha mapema kabisa wataalamu wa
ndani pamoja na watunzaji na waendeshaji
wa Miradi hiyo itakapomalizika ili kujikinga na hasara na usumbufu unaoweza
kujitokeza baada ya kukamilika kwa Miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Vile
vile, Kamati yangu inazidi kuipongeza Serikali, kupitia Wizara hii kwa kuendelea na juhudi zake za kutatua kero za
wananchi katika sekta hii ya usafiri wa nchi kavu, hususan kuanza kwa Ujenzi wa
Barabara ya Mwanakwerekwe – Fuoni pamoja
na sehemu mbali mbali kwa Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri iliyomalizika hivi
punde inaonyesha kwamba ujenzi wa Barabara ya Mwanakwerekwe - Fuoni umefikia
hatua ya uwekaji wa kifusi kwa hatua mbali mbali pamoja na Ujenzi wa Culvert.
Mheshimiwa Spika, Kamati
yako ya Mawasiliano na Ujenzi ninayoiongoza, imepata bahati ya kukagua mradi
huu na hadi tunaondoka katika sehemu hiyo barabara ilikua inasubiri utiwaji wa
lami ili mradi uweze kukamilika kabisa. Hata hivyo, shughuli ya uwekaji wa lami
bado ilikua ni kitendawili kisichokuwa na jawabu kutokana na kukosekana na
ruhusa kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Spika, Kamati
imegundua kwamba barabara hii inajengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Barabara, ambapo
kwa mujibu wa Mkataba wa Ujenzi wa Mradi huu Kampuni ya MECCO ilitakiwa
kuifanya kazi hadi hatua hii ya Kifusi tu, na baadae kazi ya utiaji wa lami
ifanywe na Idara ya Utengenezaji na Utunzaji wa Barabara Serikalini, lakini
kutokana na uhalisia uliopo na kwa kuaangalia uwezo wa Kampuni hii ya Kizalendo
ya MECCO, kumekuwa na mazungumzo na mwelekeo wa kuitumia tena Kampuni hii kwa
kazi za utiaji wa lami. Pia, Kamati iliarifiwa kwamba bado taasisi zinazohusika
hazijatoa baraka za kukabidhiwa na kuanza shughuli hiyo kwa Kampuni ya MECCO.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa
kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa Barabara hii, Kamati ya Mawasiliano na
Ujenzi inaiomba Serikali kufanya maamuzi ya haraka “ikibidi kukata pua kujenga
Wajihi” ili kazi za utiaji wa lami katika barabara hii iweze kukamilika na kuanza
kwani imeshapitwa na muda. Hata hiyo, (PBB)
kuendelea kubaki kama ilivyo hivi sasa kazi iliyokwisha kufanyika inaweza
kuharibika kwa kuchimbika kwa kifusi kilichowekwa. Vile vile, kuendelea kuchelewesha
utiaji wa lami katika barabara hii, kunaendelea kuleta adha na athari kubwa kwa
wananchi waishio pembezoni mwa barabara hiyo kutokana na mavumbi jambo ambalo
licha kuharibu afya zao inasumbua hadi kwenye mapishi yao wanakula vumbi usiku
na mchana ,adha kwa watumiaji pamoja na wananchi wanaishi pembezoni mwake kuendelea
kuteseka kiafya na kimazingira.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
yangu imegundua changamoto kubwa mbili katika mradi huu, moja na hatua ya
utiaji wa lami, ni nani atakaetia lami na nyingine ni miundombinu ya mabomba
makubwa ya maji yuliyoko kwenye barabara hiyo ambapo kamati yangu ilijitahidi
kusaidiana na wizara hii ya Miundombinu kuwakutanisha na Wizara ya Ardhi ,Maji,
Nishati na Mazingira tunawashukuru Mawaziri wa Wizara hizi mbili pamoja na
manaibu wao pamoja na Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara kwa mashirikiano
waliyoyatoa kwa Kamati ili kukwamua tatizo hilo na walituahidi katika kikao
hicho kulitatua suala hilo kwa haraka ili kazi iweze kuendelea, tunaitaka Bodi
ya Mfuko wa Barabara kutoa fedha kwa haraka ili mradi ukamilike, mara nyingi
tumekua tukilalamika kuchelewa kwa miradi kutokana na kuchelewa pesa kutoka kwa
wahisani lakini leo cha kushangaza huu mfuko wa Barabara ni pesa ya Serikali
yenyewe pia inakosekana kupatikana kwa wakati na kusababisha mradi kukwama bila
ya sababu za msingi, nadhani Mhe Waziri akija atatusaidia wajumbe ni hatua gani
imeshafikiwa katika kuondoa changamoto hizo ili mradi ukamilike.
Mheshimiwa
Spika,
Namuomba
sana Mhe.Waziri ajitahidi kuwasimamia watendaji wake ili kuikamilisha Barabara
hiyo ya fuoni kwasababu Serikali imekua ikisemwa sana na wananchi kwa kadhia ya
barabara hiyo badala ya kusifiwa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa barabara hizo
jambo ambalo halipendezi kwa Kamati yetu na naamini hata kwa Waziri mwenyewe,
na kwa moyo aliotuonyesha kwa muda mfupi tulipoanza kufanya kazi nae tumemuona
ni kiongozi makini na ana nia ya kuondoa changamoto za Wizara kwa muda mfupi
sana.
PROGRAMU YA MIPANGO NA UTAWALA KATIKA SEKTA YA
UJENZI, MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Pamoja
na nia njema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwaendeleza wananchi wake
na pamoja na jitihada zake za kuimarisha huduma mbali mbali za Kijamii, Kitaifa
na Kimataifa. Bado, kuna haja ya kujitathmini, kujiridhisha na kuwa makini
kabisa wakati wa kuingia Mikataba ya Miradi mikubwa ya kimaendeleo. Kwa kweli,
utafiti na upembuzi yakinifu pamoja na ushirikishwaji wa wadau ni vitu vya
msingi ambavyo vinaweza kusaidia wakati wa uwanzishwaji wa Miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
yangu imekagua Ujenzi wa Jengo jipya la Abiria (Terminal 2) katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar. Kwa kweli
malalamiko na manung’niko mengi kuhusiana na kutoridhishwa na mwenendo na
utekelezaji wa Mradi huu. Ujenzi wa Mradi huu umekuwa ukizungumzwa kwa muda
mrefu sasa, sio tu na Wajumbe wa Baraza
lako tukufu, bali pia na watalamu mbali
mbali wa majego pamoja na wadau wa masuala ya usafiri wa Anga.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
yangu imegundua kwamba, kulikua na mapungufu kadhaa katika mchoro wa awali
ikiwemo maegesho ya ndege kuwa karibu mno na jengo la abiria pamoja na njia ya
kurukia ndege (Run way) kuwa juu kuliko jengo lenyewe, jambo ambalo linaweza
kuleta usumbufu na uharibifu mkubwa wa mali na vifaa hapo baadae wakati wa mvua
kubwa kama hazijachukuliwa hatua za dharura ikiwemo kujenga mtaro wa kutolea
maji ya mvua ili kuondoa tatizo hilo, pamoja na Kamati yangu kuambiwa kuwa
mtaro utajengwa na kuyapeleka maji kwenye bwawa la kuhifadhia maji ya mvua
lakini kamati yangu haijaridhika na hatua hiyo kwani inaonyesha itakua ni hatua
ya dharura bali tunashauri uwepo mradi mwingine maalum kwa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege wa kuyatoa maji ya mvua uwanjani kuyapeleka hadi pwani ( Baharini).
Hiyo ndio itakua ufumbuzi wa kudumu kwa kuyaondoa maji ya mvua hapo uwanjani.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na chanagamoto hizo, Kamati haikuridhika na mwenendo mzima wa Mradi huu, Mradi
ambao awali ulianza kwa dola za
Kimarekani 70,400,000 (2009) na kufanyiwa
marekebisho (June 2012) kwa kuongezwa
Dola 11,828,674.71 na hatimae Aprili, 2014 ulifanyiwa marekebisho mengine na kuongezwa tena Dola 46,518,414.80 na kufanya
jumla kuu kufikia Dola za Kimarenani 128,747,089.51.
Hiki ni kiwango kikubwa sana cha
fedha kwa mradi mmoja jambo ambalo sisi wajumbe tangu ulipoanza mradi huu
tulianza kutilia mashaka jinsi ya ushirikishwaji wa wadau mbali mbali jambo
ambalo lilitawaliwa na manung’uniko miongoni mwa watendaji wa Serikali na hata
Wajumbe kuzuia Bajeti kutokana na kizungumkuti cha mwenendo wa mradi huu,
pamoja na hayo lakini Kamati yangu inamtaka Mhe. Waziri kuwa jasiri na makini
zaidi na kuangalia changamoto hizo
lakini cha msingi sasa tunataka mradi ukamilike na tuanze kuutumia kwa maslahi
ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
Tunamuomba sana Mhe.Waziri, kuisimamia miradi
ya Wizara kwa karibu zaidi kwani tumeona karibu miradi yote ya Wizara hii
imekua ikiongezeka gharama zake kila siku ukiangalia hili sio jambo la kudharau
hata kidogo.
Mheshimiwa Spika,
Jambo jingine katika Mradi huu wa (Terminal 2) ni changamoto ya
kutokushirikishwa kwa wadau mbali mbali ambao watakaoutumia Uwanja huo tokea
mwanzo, lakini pamoja na hayo Kamati yangu inaitaka Wizara kuhakikisha
inaitisha vikao mbali mbali vitakavyowashirikisha wadau wote ikiwemo Mamlaka
yenyewe ambayo ndio watakaokuja kukabidhiwa jengo hilo ili kuanza kupanga ni
namna gani wataweza kuja kuutumia na kuudhibiti uwanja huo, changamoto nyingine
kamati yangu iliyoiona ni kiwango kikubwa cha Umeme kitakachokuja kutumika
katika kuendeshea kiwanja hicho na utaratibu wa mapato na matumizi ya Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege baina yao na Wizara ya fedha, na hili ni vyema katika
hivyo vikao vyao tunavyowashauri Wizara basi
na hili muanze kulizingatia mapema ili kuepuka usumbufu hapo baadae. Pia Kamati
yangu inaishauri Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuliekea kinga ya
Bima ya ajali ya moto jengo hilo kwani ni jengo la gharama kubwa kwa hiyo ni vyema
kuliekea tahadhari mapema, kwani mfano mzuri hivi karibuni katika nchi jiraji
ya Kenya kiwanja cha JomoKenyatta Airport kiliungua moto lakini kwa kua kiwanja
kimekatiwa Bima basi kiliweza kukarabatiwa kwa muda mfupi na kuendelea na kazi
kama kawaida, lakini pia kwakua kiwanja kitatumika na wageni mbali mbali pamoja
ndege kubwa za kimataifa basi ni lazima kiwanja kiwahahakikishie wadau wote
wataokitumia kuwa kiko katika hali ya usalama mkubwa wakati wote.
Mheshimiwa Spika,
Kitabu
cha Mheshimiwa Waziri pia kinaonyesha kupungua
kwa Tani za Mizigo iliyohudumiwa kwa mwaka huu, ambapo walihudumia Tani 1,397 ikilinganishwa na Tani 1,439 mwaka jana kwa madai
ya kupungua kwa idadi ya ndege maalum za Mizigo. Kamati inaomba kupatiwa
maelezo ya kina juu ya mapungufu haya na namna ya Mamlaka ilivyojipanga kukabiliana
na tatizo hilo kwani tunategemea kila kiwanja kinavyoboreka basi iendane na
makusanyo yatakavyoongezeka.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu
Uwanja wa Ndege wa Pemba, Kamati inaipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege,
Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kukamilisha Mradi wa Utiaji wa Taa za Kuongozea Ndege wakati wa kutua na kuruka katika kiwanja hicho. Hata hivyo, Kamati haijaridhika
na matumizi ya kiwanja hicho kwani hadi hivi sasa hakuna ndege yoyote inayotua ama
kuruka baada ya jua kuzama. Uchunguzi wa Kamati umebaini kwamba, hali hii
inakuja kutokana na kwamba Makapuni yanayotoa Huduma za Usafiri wa ndege kuleta
ndege zenye Injini na propela moja tu, ambazo haziruhusiwi
kuruka baada ya jua kuzama. Kutokana na kadhia hii, Kamati inachukuwa fursa hii
kuiomba Serikali kuwashajihisha watu wa Kampuni za ndege kuleta ndege ambazo
zinaweza kutoa huduma hata baada ya jua kuzama. Aidha, Kamati pia inasisitiza
juu ya uimarishwaji wa usafi pamoja na vitendea kazi katika Uwanja wa ndege wa
Pemba kwani hali ilivyo hivi sasa bado haiiridhishi. Pia Kamati yangu imepata
taarifa tangu taa hizo kutiwa hapo kiwanjani basi hakuna ndege iliyowahi kwenda
huko usiku, kwa hiyo bado tunashauri Wizara kuhakikisha kila inapokusudia
kufanya maboresho katika maeneo yake basi ni vyema kuwashirikisha wadau ili
kuweza kupata ushauri wa uwekaji wa miundombinu na kupata matokeo mazuri wakati
wa matumizi ya miradi yao. Ndio maana tukasema hata huo uwanja Mkubwa basi washirikishwe
wadau wote ikiwemo Mamlaka yenyewe na taasisi binafsi zitakazokuja kuutumia
uwanja huo, kwani hata sekta binafsi zinamawazo mazuri ya kuboresha huduma za Viwanja
vya Ndege na maeneo mengine. Lakini pia kamati yangu inaishauri Serikali isione
taabu kuingia mikataba ya (PPP) katika
kuundesha uwanja wa Ndege Terminal 2 kwani utahitaji uangalizi
wa hali ya juu na maarifa makubwa ya kuuendesha
uwanja huo, lakini pia kwa kuzingatia matumizi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa
kupewa heshima zao maalum kwenye mikataba hiyo. Kwani Uwanja huo ni mali ya
Umma.
PROGRAMU NDOGO YA MIPANGO NA SERA KATIKA SEKTA YA
UJENZI, USAFIRI MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Kamati
yangu inalipongeza sana Shirika la Bandari kwa kazi nzuri za kutoa huduma za
kuzihudumia Bandari zetu za Unguja na Pemba, pamoja na changamoto za ubaba wa
fedha za kununulia vifaa vya kisasa katika kuendeshea kazi zao, Kamati ilipokea
maelezo kua wakati mwingine inapohitaji mkopo kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar
inabidi kutumia pesa zao za ndani jambo ambalo linarejesha nyuma Shirika letu.
Kutokana na taarifa hiyo, Kamati yangu inamuomba Waziri kupitia Katibu wake
Mkuu ambae ni mzoefu wa masuala ya Bandari kulisaidia Shirika kupata fedha hizo
na ikiwa kuna ugumu kwa PBZ Basi wasiogope kwenda kwenye mabenki mengine kukopa
ili kujiimarisha kihuduma na kibiashara, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Shirika
wanayohaki ya kukopa, kushtaki na kushtakiwa, kwa hiyo suala la fedha kisiwe
kikwazo cha kukwamisha shughuli zao.
Mheshimiwa Spika,
Shirika
la Bandari ni lango kuu la kuingilia mizigo yote hapa Zanzibar kutoka nchi za
nje, lakini bado Bandari zetu zina mapungufu makubwa sana katika vitandea kazi
hasa Crine za kisasa ambazo zingeliweza kupakua mizigo kwa haraka, lakini pia
Shirika lina changamoto kubwa ya mahala pa kuhifadhia Makontena. Jambo ambalo
pia husababisha usumbufu mkubwa wa msongamano hapo Bandarini, kwani pale kwenye
uwanja wa Hoteli ya Bwawani yalipokua yakihifadhiwa hivi sasa eneo hilo
haliwezi kutumika tena, kwa hiyo tunalitaka Shirika kutafuta eneo jingine
mbadala la kuhifadhia makontena ili kuondoa usumbufu kwa wafanya biashara wenye
makontena.
Mheshimiwa Spika,
Lakini
pia namuomba Mhe.Waziri akija aje kutusaidia ufafanuzi hivi karibuni kampuni
moja ya meli CMC inayoleta Makontena
hapa Zanzibar walitoa circular kwa wateja wao kua kunaongezeko la karibu USD 200 kwa Kontena kutokana na conjestion ya Makontena hapo
Bandarini, je suala hili ni kweli? Na kama ni kweli je Shirika limechukua hatua
gani kuihami hali hiyo.Kwani ongezeko ya bei ya usafirishaji pia huathiri bei
za bidhaaa hapa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Pia,
Kamati yangu inaipongeza Serikali kupitia Shirika la Bandari kwa ujenzi wa Gati
ya Tumbatu lakini inaiomba Serikali kwenye Bandari ya mkokotoni kuweka
utaratibu mzuri wa kudhibiti mizigo na abiria wanaoingia pale kwani kuna mapato
mengi ya kodi ya Serikali hayakusanywi na pia kuna watu huingia kiholela
kupitia Bandari hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja
na kuwa Kamati yangu haijapata nafasi ya kuitembelea Bandari ya Pemba lakini
tunaishauri Wizara kupitia Shirika kutafuta Crine kubwa katika Bandari ya Pemba
kwani inaleta usumbufu mkubwa hasa kunapotokea mizigo mikubwa pale Bandarini. Pia,
Kamati yangu inalitaka Shirika kuangalia uharibifu wa mazingira unaofanywa na
baadhi ya wavuvi huko kwenye mnara wa matumbini ili usije kuleta athari kwa
mnara ule.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
inachukua fursa hii tena kuipongeza Serikali kwa kwa kusikia kilio cha Wajumbe
wa Baraza lako tukufu liliopita kwa kuitaka Serikali kununua Meli yake ya
kubeba abiria na mizigo hasa baada ya kuona ajali za baharini zimekua nyingi na
za kutisha kutokana na upungufu wa vyombo vya usafiri wa Baharini jambo ambalo
lilipoteza maisha ya wananchi wengi pamoja na mali zao kwa mashirikiano na
kuliomba Baraza kuruhusu kukata matumizi ya viburudishaji na vinywaji kwenye
bajeti za Wizara na tukaweza kufunga mikanda na leo tunajivunia kua tumeweza
kununua meli ya MV. Mapinduzi II. Ambayo
hivi sasa inaendelea na safari zake kama kawaida. Hata hivyo, kumekuwa na
taarifa tofauti kuhusiana na upakiaji wa Mizigo ndani ya meli hiyo, inasemekana
hivi sasa meli hiyo inashindwa kupakia baadhi ya mizigo ikiwemo magari.
Kutokana na taarifa hizo, Kamati inahitaji Maelezo ya kina juu ya kadhia hiyo.
Vile vile, Kamati inashauri kuangaliwa upya kwa utaratibu wa ukusanyaji wa mapato
ya meli hii kwani kunataarifa kwamba wanaosimamia meli hii sio wanaokusanya
mapato hayo, jambo ambalo Kamati yangu haijafurahishwa nalo kwani inaweza
kuleta usumbufu mkubwa hasa katika kuihudumia Meli hiyo. Kamati yangu inaitaka
Wizara kuwaekea misingi watendaji wa Shirika, ili kuweza kudhibiti mapato yake
na pia kutumia kufuatana na taratibu za Shirika zinavyosema ili kuhakikisha
Meli hiyo inakua safi, na kutoa huduma bora kwa wananchi kama inavyotarajiwa.
PROGRAMU YA UHIFADHI WA MJI MKONGWE NA
UIMARISHAJI WA MAJENGO YA SERIKALI NA BINAFSI
Mheshimiwa Spika,
Shirika
la Nyumba imepandisha kodi ya nyumba kutoka shilingi 25,000/= kwa mwezi hadi
shilingi 75,000/=. Kiwango hiki ni kikubwa ukizingati kwamba wengi wa wapangaji
hao ni wa kipato cha chini. Kamati inaitaka Wizara kukaa pamoja na watendaji wa
Shirika hilo ili kufikiria upya mabadiliko hayo kulingana na vipato vya
wananchi wetu, pamoja tunajua kua Shirika linahitaji kujitegemea lakini pia
tufikirie na wengi ya wanaoishi ni wananchi wenye kipato cha chini ,tunashauri
kupandisha kodi kwa ghafla kwa asilimia 150 sio jambo sahihi kuzingatia hali ya
watu wetu, isipokua kwa zile nyumba zinazotumika kibiashara kama maduka,
mikahawa na biashara nyengine hizo
wangeliweza kuwapandishia kodi kiasi hicho au hata zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
yangu inaelewa mzigo mkubwa uliokabidhiwa Shirika la nyumba kuanzishwa likiwa
na nyumba karibu zote zimesha chakaa na zinahitaji mtaji mkubwa ili kuzirejesha
katika ubora wake wa asili na ukarabati huo unahitaji pesa nyingi
tungeliishauri Serikali kulipatia mtaji Shirika hilo ili kutafuta nguvu za
kujitegemea kibiashara na kutoa huduma za makaazi, vinginevyo kuwabebesha mzigo
huo kwa ghafla wananchi wetu kwakweli sio sahihi na huo ni mtihani wetu sote. Pia
tunalishauri Shirika hilo kubuni miradi kwa kushirikiana na taasisi za fedha za
ndani na nje ili kujenga majengo kwa ubia na wateja mbali mbali ili kuweza
kujenga majumba ya kisasa na kuweka miji yetu katika sura nzuri kama
inavyotakiwa, kamati yangu pia inalitaka Shirika kuzifanyia ukarabati nyumba za
maendeleo zilizojengwa na uongozi wa awamu ya kwanza kwani baadhi yao hivi sasa
zimeanza kuhatarisha maisha yao, vilevile kamati yangu inataka Shirika lipige
marifuku wale wapangaji wote kwenye nyumba za maendeleo kuacha mara moja
kuzivunja nyumba hizo na kutia milango ya nyuma na milango ya biashara bila
kushirikisha Shirika lenyewe kwani hupelekea kusababisha kupunguza uimara wa
majengo hayo, kwani wengine hufanya Saloon, milango ya nyuma n.k.
Mheshimiwa
Spika,
Mji Mkongwe ni moja ya miji ya urithi wa kimataifa, na ni
hazina kubwa Mwenyeenzi Mungu aliyotujaalia, mji huu umekua ni sehemu moja ya
vivutio vya wageni kuja kutembelea Zanzibar, mji huu umekua ukiipatia nchi yetu
mapato mengi ya pesa za kigeni, lakini pia wasomi wengi wa Historia wamekua
wakija kuutembelea na kufanya research zao kupitia Mji Mkongwe wa Zanzibar, mji
huu umehifadhi majengo makongwe ya kihistoria ambapo yalijengwa karne nyingi
zilizopita, kwa hiyo ni mji ambao unaopaswa kuhifadhiwa, kulindwa na kudumishwa
na wazanzibari sote ili kulinda hazina hiyo, kwa nchi za wenzetu kama vile Misri imekua ni moja ya kiingizio kikubwa cha mapato kwa
nchi zao kutokana na kuvitangaza vivutio vyao vya kihistoria ikiwemo majengo na
rasilimali zilizomo kama kumbukumbu za matukio ya Nchi zao.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaitaka Mamlaka kupitia Mhe. Waziiri
wamejipanga vipi kuuhifadhi mji huo hasa kutokana na ujenzi wa majumba mengi ya
kisasa yanayojengwa katika mji huo ambayo hayaendani na uasilia wa majengo
hayo, lakini isitoshe Kamati yangu inaendelea kusikitishwa sana na kuona kua
jengo la Mji Mkongwe limefikia hali ya kuanguka sehemu ya jengo hilo na hadi
leo limeshindwa kukarabatiwa, na pia Kamati yangu inataka majibu kutoka kwa
Waziri, je? Fedha zinazopatikana kutokana na jengo hilo zinadhibitiwa na taasisi
gani? Na kama kuna taasisi inayokusanya mapato ya hapo ilikuaje hadi jengo
kufika kubomoka bila kufanyiwa ukarabati kwa wakati. Pia, Kamati yangu inaitaka
Wizara kuhakikisha jengo hili linakarabatiwa na kulirudisha katika hali yake ya
kawaida.
Mheshimiwa
Spika,
Pia, Kamati yangu
inataka kujua katika Mji Mkongwe, kuna majumba mangapi yanayohifadhiwa, pia je
yako majengo katika Mji Mkongwe hayamo katika uhifadhi, je kwa kua kuna idadi
kubwa ya nyumba za Mji Mkongwe ambazo zimechakaa na hazifai kuishi binaadam kwa
usalama wao lakini vado nyumba hizo zinaendelea kuishi watu je ni hatua gani za
kisheria zinachukuliwa ili kunusuru maisha yao, na kama ikitokezea jumba
limeanguka na kuathiri maisha yao je Mamlaka ya Mji Mkongwe inawajibika vipi?
Mheshimiwa
Spika,
Kabla sijamalizia hotuba yangu, napenda sasa kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote kwa kunisikiliza kwa makini na
utulivu, pia napenda kukushukuru kwa mara nyengine tena wewe binafsi kwa
kuniruhusu kutoa maoni ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi
kuhusiana na Bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya maelezo hayo, napenda kutamka kwa niaba ya
Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi na kwa
niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Shaurimoyo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji. Aidha nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wote wachangie
na wakosoe na kushauri pale penye kasoro ili ikipita iwe Bajeti yetu sote na
tumpe nguvu Waziri wetu msikivu kwenda kuyatekeleza yale tuliyomuelekeza na
yale aliyotuomba tumkubalie akayatekeleze kwa maslahi ya wananchi wetu na Taifa
letu kwa ujumla. Na hatimae nakuombeni Waheshimiwa Wajumbe wenzangu wote wa Baraza
hili tukufu kuunga mkono Makadirio ya Bajeti ya Wizara hii kwa ajili ya
utekelezaji bora wa majukumu na malengo waliyojipangia.
Mheshimiwa Spika,
Naomba
kuwasilisha.
Ahsante,
Hamza Hassan Juma,
Mwenyekiti
Kamati ya
Mawasiliano na Ujenzi,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
.
Je si uzembe na ubadhirifu huu ? Mradi unaongozeka gharama na Hamna aliefikishwa mahakamani kujibu, au kuwajibishwa ni Sawa na ule mradi wa e-government wa smz ambapo ulikamilika na ukagundulika na kasoro tele ila wasimamizi wakasema " mara hii hatutafanya makosa ". Je wanajua kwamba watu hata mlo mmoja unawashinda ? Je hizo fedha za wananchi wanazitumia kama si za mtu ? Au ndo Ukiwa mkuu katika smz ufanye utakavyo kwenye fedha za maskini?
ReplyDelete