Monday, June 20, 2016

Zantel yanogesha tamasha la ‘Full Moon Party’ visiwani Zanzibar

Zantel yanogesha tamasha la ‘Full Moon Party’ visiwani Zanzibar
Kampuni ya simu inayoongoza visiwani Zanzibar,Zantel,mwishoni mwa wikii hii imefanikiwa kulinogesha tamasha la ‘Full Moon Party’ linalofanyika kila mwezi visiwani Zanzibar na kufanikiwa kuvuta mamia ya mashabiki.
Tamasha hilo maarufu linalojumuisha burudani ya muziki na sarakasi, lilifanyika katika ufukwe wa Kendwa Rocks mkoa wa Kaskizini Unguja likijumuisha burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Kikundi cha Sarakasi cha Zanzibar ndicho kilichoanza kutoa burudani kikifuatiwa na bendi ya FM Academia kutoka Dar es Salaam, wakiongozwa na Nyoshi El Saadat, ambao waliacha gumzo kwa burudani kali waliyoitoa.
Akizungumzia kuhusiana na tamasha hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, bwana Benoit Janin alisema lengo la Zantel kudhamini tamasha hilo ni kukuza utalii wa ndani hapa nchini.
‘Tamasha hili linalenga kufungua milango ya utalii nchini kwa kuonyesha vivutio vya kiburudani tulivyonavyo, na hivyo kuiongezea mapato nchi yetu’ alisema bwana Janin.
Katika kunogesha zaidi tamasha hilo Zantel ilimualika mtangazaji wa kipindi cha 5 Select cha East Africa TV, Tbway kuwa mshereheshaji shughuli hiyo.