Habari za Punde

HOTUBA YA KAMATI YA MAWASILIANO NA UJENZI YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA UJENZI, MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

Mheshimiwa Spika,                                                     
Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kwa mara nyengine tena kufika na kuweza kukutana mbele ya Baraza lako Tukufu tukiwa wazima na wenye afya njema, kwa lengo la kujadili mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo na ustawi wa nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako Tukufu ili niweze kuwasilisha kwa niaba ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Hotuba ya Maoni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika,
 Pia, napenda kutoa shukrani zangu kwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na Watendaji wote wa Wizara hii kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kufanikisha kumalizika kwa kazi hii ya Kamati. Kwa kweli ushirikiano wao umetupa moya sana, na wameonyesha nia ya kuendeleza yale mazuri waliyoyakuta hapo Wizarani na pia kuyaondoa yote yanayorejesha nyuma maendeleo ya Wizara yao nasisi tunaahidi kufanyakazi nao kwa pamoja ili malengo waliyojiwekea yaweze kufikiwa.
Mhesimiwa Spika,
 Sasa naomba nichukue nafasi hii, kuwashukuru kwa dhati Wajumbe wa Kamati yangu kwa michango yao muhimu waliyoitoa wakati tulipokuwa tukijadili na kupitia Bajeti hii, ambapo mawazo na mapendekezo yao yamewezesha leo hii kufika hapa na kuweza kuwasilishwa mbele ya Baraza lako Tukufu na hatimae kujadiliwa na  kupitishwa kwa  lengo la kuiwezesha Wizara kutekeleza malengo yake iliyojipangia kwa mwaka huu. Naomba sasa kwa ruhusa yako niwataje Wajumbe pamoja na Makatibu wa Kamati yetu ya Mawasiliano na Ujenzi kama ifuatavyo:-
1.    Mhe. Hamza Hassan Juma                                 Mwenyekiti
2.   Mhe. Suleiman Sarahan Said                             M/ Mwenyekiti
3.   Mhe. Abdalla Ali Kombo.                             Mjumbe
4.Mhe.BahatiKhamis Kombo.                             Mjumbe
5.Mhe. Khadija Omar Kibano                               Mjumbe 
6.Mhe.Mohammedraza Hassanaali                         Mjumbe
7.Mhe.Mwanaidi  Kassim Mussa                              Mjumbe
8.   Mhe. Nassor Salim Ali                                 Mjumbe
9.   Mhe. Said Omar Said                              Mjumbe
10.Ndg. Fatma Omar  Ali                                  Katibu
11.Ndg.Himid Haji Choko                                 Katibu
 Mheshimiwa Spika,
Baada ya utangulizi huo sasa napenda nitoe Maoni ya Kamati kuhusiana na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika,
Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji   ni moja ya Wizara muhimu katika nchi yetu kutokana na ukweli kwamba inasimamia sekta muhimu  kwa maendeleo ya nchi yetu, ambazo ni Sekta ya Ujenzi, Sekta ya Usafiri wa Baharini, Sekta ya Usafiri wa Anga, Sekta ya Usafiri wa Nchi Kavu pamoja na Sekta ya Mawasiliano. Aidha, baada ya maelezo hayo naomba sasa niaze na uchambuzi wa Programu zinazosimamiwa na Wizara hii.
PROGRAMU YA MIUNDOMBINU NA HUDUMA ZA USAFIRI WA BARABARA
Mheshimiwa Spika,Kamati yangu imepata nafasi ya kufanya ziara ya siku mbili Unguja na Pemba kabla ya kuipitia Bajet hii ya mwaka 2016/17, pamoja na ufinyu huo wa muda kamati ilijifunza mambo mengi ambayo ni changamoto za Wizara na kwa kweli iko haja ya kuweka mipango madhubuti ili kuhakikisha kazi za Wizara zinaenda kwa kasi kwa mujibu walivyojipangia wao bila ya vikwazo vyovyote. Aidha, Kamati yangu imejipanga kuisaidia sana Wizara katika kipindi chote ambacho Mhe Spika umetutuma tuisimamie. Pamoja na hayo Kamati yangu imeipitia Bajeti hii katika mazingira magumu haswa ukizingatia Wajumbe wangu wengi ni wageni hapa Barazani lakini pia hawajawahi kuikagua Wizara nzima pamoja na kukutana na wafanyakazi ili kujua changamoto zao ili kamati ikaweza kuisaida Wizara ipasavyo, lakini pamoja na hayo nawashukuru Wajumbe wangu kwa umahiri wao jinsi walivyoweza kutoa michango yao kwa Wizara kupitia uzoefu wao na msaada mkubwa wa watendaji wao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hii, lakini naamini mwakani wataweza kuisaidia sana Wizara ili kuona changamoto zao zinageuka kua chachu ya maendeleo kwao.
Mheshimiwa Spika,Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kukamilisha Mradi wa Ujenzi wa Barabara mbili kati ya tatu kwa upande wa Pemba zenye urefu wa kilomita 30.2. Barabara hizo ni barabara ya Wete - Konde na Wete - Gando. Na bado barabara moja ya Wete -Chake Kwa kweli kukamilika kwa Mradi huu kunaondoa ile adha ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaotumia barabara hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu imetembelea Mradi huo na kushuhudia wenyewe kazi kubwa iliyofanywa na Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Co. Limited (MECCO), iliyopewa Kandarasi ya Kujenga barabara hizo. Kwa kweli barabara hizo zimejengwa kwa kiwango kinachohitajika haswa kwa wakati huu tulionao. Kamati inaamini kwamba Serikali haikufanya makosa kuiteuwa Kampuni ya MECCO kuipa kazi hii, kwani kiwango cha ubora wa barabara hizo ni kikubwa sana na cha kupigiwa mfano kwa hapa Zanzibar. Pamoja na mafanikio hayo lakini bado kuna barabara hii ya Wete –Chake ambayo ni sehemu moja ya barabara hizo haijaanza kujengwa hadi leo ili kukamilisha mradi huo wa barabara tatu za Pemba kutokana na Serikali kuchelewa kutoa pesa za fidia wananchi ambazo zinakadiriwa kufikia karibu Bilioni moja na milioni mia saba (1.7 Bil), ambazo zingelimuwezesha mjenzi kuendelea na kazi hiyo iliyobakia, kwakweli suala hili limeisikitisha sana Kamati yangu kwani kutokana kuchelewa kwa mradi huu kunaweza kuongeza gharama za mradi huo kuliko bajeti iliyopangwa hasa kutokana na gharama za vifaa kupanda bei siku hadi siku ,lakini baada ya kuangalia bajeti kuu ya Serikali ya mwaka huu wa 2016/17 tumeziona pesa hizo 1.7 Bilioni zimetengwa kwenye bajeti ili kumalizia malipo hayo ya fidia kwa wananchi ili mjenzi aendelee na kazi iliyobaki ya kukamilisha bara bara hiyo ya Wete Chake,
Mheshimiwa SpikaKamati yangu inaitaka Wizara ya fedha kuipatia Wizara pesa hizo mara tu baada ya kuipitisha Bajeti hii kwani sio kwamba ikishalipwa fidia kua kazi hiyo itaanza hapohapo, kwani hapo kutakua na kazi za kuanza kuondoa baadhi ya nyumba na vipando mbali mbali vilivyomo katika eneo la mradi kazi ambayo pia itachukua muda, kwa hiyo kutolewa mapema kwa pesa hizo kutaharakisha ukamilishaji wa ujenzi huo ambao umeshakua wa muda mrefu ambao uliasisiwa tangu mwaka 2009. 
Mheshimiwa SpikaHata hivyo, Kamati yangu kwa masikitiko kabisa, inakujuiilisha kwamba bado Kampuni hiyo ya MECCO licha ya kuing’arisha Pemba kwa Ujenzi wa barabara hizo, bado haijakamilishiwa malipo ya kazi hiyo ya Kujenga barabara hizo. Ambapo kampuni hiyo inadai karibu 3 mil usd na Tshs 1.7 wakati kazi wameshamaliza zaidi ya miaka mitatu nyuma, jambo ambalo linaisababishia Serikali kujiongezea mzigo wa madeni pamoja na riba ya ucheleweshaji wa malipo ya mradi (Interest). Ambapo mzigo huo huwabebesha wananchi bila sababu yoyote.

Mheshimiwa Spika, Lakini pamoja na hayo tunamshukuru Mhe Waziri kwa kuiahidi Kamati kua suala hilo limeshafika ofisini kwake na ameshalitolea maelekezo ufanyike uhakiki wa madai hayo na mwenye haki yake apewe, hii Imetupa moyo Kamati kwani jambo ambalo limekwama kwa muda zaidi ya miaka mitatu Waziri ameahidi kulitatua kwa wakati muafaka ili kazi zisikwame kwa sababu zisizo za msingi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kadhia hii ya ucheleweshaji wa malipo hasa kwa pesa zinazotoka kwa Wafadhili Kamati yangu tunamshauri Waziri wa Fedha kuwateua maafisa katika kila mradi ili kuwepo Wizarani kwa muda wote wa mradi ili kuona na kujua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwasilisha Wizara ya fedha ili kuondoa usumbufu wakati wa malipo, kwani imeonyesha wakati mwingine kunatokea kutokuaminiana kwa baadhi ya watendaji baina Wizara ya Fedha yaani mlipaji (PAYEE) na Wizara yaani mwenye mali (CLIENT), jambo hili tunaona sio sahihi kwani hao wote ni watendaji wa Serikali na wanafanyakazi ya wananchi kwa maendeleo yetu sote sio ya mtu Fulani. Aidha, tatizo hili sio kwa Wizara hii tu bali ni kwa miradi yote inayopatiwa pesa kutoka kwa wahisani au mikopo ya nje. Kwani Wizara inapojipangia malengo ya mwaka mmoja basi huhitaji watekeleze kama walivyopanga na kusiwe na vikwazo, hasa kwa utaratibu wa sasa wa Bajeti inayozingatia Program (PBB) maana yake mipango iende kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Aidha, juhudi za Serikali za kuwasogezea maendeleo wananchi wake, ilijenga Barabara tano za ndani za Mkoa wa Kaskazini Pemba chini ya Ufadhili wa Millenium Challenge Accout (MCC-T) na kazi hii ilipewa Kampuni ya H. Young ya Kenya. Ujenzi wa  Barabara hizo zilizojengwa kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 35 ambao ulijumuisha barabara za Kipangani - Kangagani, Chwale – Kojani, Mzambarau Takao - Pandani hadi Finya, Mzambarau Karim – Mapofu, Bahanasa – Daya na Makoongeni – Mtambwe.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu ilibahatika kuzitembelea barabara hizo na kugundua changamoto kadhaa ikiwemo dosari zilizojitokeza muda mfupi tu, baada ya kukamilika ujenzi wa barabara hizo mara tu baada ya kukabidhiwa kwa Serikali. Dosari hizo ni pamoja na nyufa na mmong’onyoko wa udongo katika sehemu mbali mbali za barabara hizo. Aidha Kamati yangu imegundua kwamba baada ya kusikiliza ushauri wa jopo la wataalamu , Mwajiri (MCA-T) pamoja na Wizara kwa ujumla waliamua kufanyika kwa matengenezo kadhaa ili kuzihami barabara hizo  na kazi hii ilikabidhiwa tena kwa Kampuni ya MECCO kwa gharama ya  Dola za Kimarekani Milioni 1.68.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu baada ya kuona changamoto kwenye barabara hizo tunaishauri Serikali kabla ya hizi kampuni hasa za ujenzi wa Barabara kuzipa kazi za ujenzi (TENDER) basi ni vyema zile (tender board) kuangalia vizuri vigezo (B.O.Q) pia na uzoefu wa kazi na kujiridhisha kwa kuona kazi zilizofanywa na kampuni hizo na sio kuja kujifundishia kazi hapa kwetu Mheshimiwa Spika, kwani pesa zinazotumika, ni pesa za wananchi kwa hiyo zinapaswa kutumika vizuri.
Mheshimiwa Spika, Hili nnalisema kwani kwa uzoefu Mhe. Rais wetu wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. (JOHN POMBE MAGUFULI) wakati akiwa Waziri wa Miundombinu wa Jamhuri ya Muungano aliwahi kuwafukuza kazi wakandarasi wasiokua na viwango na pia kukataa kuzipokea barabara ambazo zilizokua zimejengwa chini ya kiwango, hii ilimjengea sana sifa wakati huo na ndio maana wananchi wanamkubali kwa umakini wake na umahiri wake wa kutokua na muhali wakati anapokua kazini na hadi hii leo amekua Raisi bora Duniani na kila pahala amekua akisifika. Kwahiyo, Mhe. Waziri wetu tunakuomba uige mfano wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli usikubaki kuipokea kazi ambayo itakayokua chini ya kiwango na pia usiikubali Kampuni yoyote ambayo haina uzoefu wa kufanya kazi na kuja kujifundishia kwenye Wizara yako, kwani ndani ya Wizara yako huko nyuma zipo Kampuni zilipewa kazi zikashindwa njiani na nyingine zimekimbia na hadi leo kazi zimelala na kurejesha nyuma maendeleo ya nchi yetu na ukiangalia historia za kampuni hizo ni zile zilizoletwa na wajanja kwa tama zao na kuitia hasara Serikali. Vile vile, Kamati yangu itakusaidia kukupa nguvu pale utakapoamua kuifukuza kazi kampuni yeyote ya mkobani.
Mheshimiwa Spika, chi nyingi za kiafrika zinakabiliwa sana na changamoto hii ya kujengewa barabara zilizo chini ya kiwango na kuzibebesha mzigo Serikali zao, kwa hili sisi hatutolikubali.
heshimiwa Spika, Pia, Kamati yangu ilistushwa sana na kiwango cha pesa nyingi sana zilizolipwa kwa fidia kwenye ujenzi wa barabara hizi za Pemba karibu Tshs. ( 6.Bil ) Kiwango hiki ni kikubwa sana ambapo Kamati ilipoiuliza Wizara wakasema haikuhusishwa na ulipaji wa fidia hizo, suala hili kwa kua Kamati haijakusudia kuundwa kwa kamati teule kulifuatilia suala hili tunaitaka Wizara ilifanyie kazi na ituletee ripoti kamili ya uhakika na uhalali wa malipo hayo kwani ukiangalia katika maeneo hayo hakuna majumba mengi kiasi hicho ambapo gharama ingekua kubwa kiasi hicho. Kwani kama hatukua makini hasa kwenye masuala ya fidia basi miradi itakua na gharama mara mbili ya bajeti halisi kutokana na ukubwa wa fidia hizo zinazotolewa nasema haya kwani hadi hii leo bado kuna malalamiko ya wananchi kuhusu fidia hizo.
Mheshimiwa Spika, Hadi Kamati yangu inapitia Bajeti ya Wizara hii, kazi hii ya marekebisho ya barabara hizo ilikua inaendelea ingawa kulikua na madai ya kujitokeza vipingamizi kadhaa kama vile idara zenye dhamana ya rasilimali zisizohamishika kutoa pingamizi ya kuchimba na kusafirisha kifusi na mawe kwenda eneo la kazi. Kutokana na suala hili tunaziomba taasisi zote za Serikali kutoa mashirikano wakati wa kutekeleza miradi bila ya kujali mradi unatekelezwa Wizara gani kwani zote ni taasisi za Serikali hiyo, tofauti ni mgawanyo wa majukumu tu.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kadhia hii na nyenginezo zinazofanana na hii, Kamati inaishauri Serikali kwamba, wakati wa utekelezaji  wa Miradi Mikubwa kama hii, kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha mapema kabisa wataalamu wa ndani pamoja na watunzaji  na waendeshaji wa Miradi hiyo itakapomalizika ili kujikinga na hasara na usumbufu unaoweza kujitokeza  baada ya kukamilika kwa  Miradi hiyo.
Mheshimiwa SpikaVile vile, Kamati yangu inazidi kuipongeza Serikali, kupitia Wizara hii kwa  kuendelea na juhudi zake za kutatua kero za wananchi katika sekta hii ya usafiri wa nchi kavu, hususan kuanza kwa Ujenzi wa Barabara ya Mwanakwerekwe – Fuoni  pamoja na sehemu mbali mbali  kwa Unguja na Pemba.  
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri iliyomalizika hivi punde inaonyesha kwamba ujenzi wa Barabara ya Mwanakwerekwe - Fuoni umefikia hatua ya uwekaji wa kifusi kwa hatua mbali mbali pamoja na Ujenzi wa Culvert.
Mheshimiwa Spika, Kamati yako ya Mawasiliano na Ujenzi ninayoiongoza, imepata bahati ya kukagua mradi huu na hadi tunaondoka katika sehemu hiyo barabara ilikua inasubiri utiwaji wa lami ili mradi uweze kukamilika kabisa. Hata hivyo, shughuli ya uwekaji wa lami bado ilikua ni kitendawili kisichokuwa na jawabu kutokana na kukosekana na ruhusa kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa SpikaKamati imegundua kwamba barabara hii inajengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Barabara, ambapo kwa mujibu wa Mkataba wa Ujenzi wa Mradi huu Kampuni ya MECCO ilitakiwa kuifanya kazi hadi hatua hii ya Kifusi tu, na baadae kazi ya utiaji wa lami ifanywe na Idara ya Utengenezaji na Utunzaji wa Barabara Serikalini,   lakini kutokana na uhalisia uliopo na kwa kuaangalia uwezo wa Kampuni hii ya Kizalendo ya MECCO, kumekuwa na mazungumzo na mwelekeo wa kuitumia tena Kampuni hii kwa kazi za utiaji wa lami. Pia, Kamati iliarifiwa kwamba bado taasisi zinazohusika hazijatoa baraka za kukabidhiwa na kuanza shughuli hiyo kwa Kampuni ya MECCO.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa Barabara hii, Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi inaiomba Serikali kufanya maamuzi ya haraka “ikibidi kukata pua kujenga Wajihi” ili kazi za utiaji wa lami katika barabara hii iweze kukamilika na kuanza kwani imeshapitwa na muda. Hata hiyo, (PBB) kuendelea kubaki kama ilivyo hivi sasa kazi iliyokwisha kufanyika inaweza kuharibika kwa kuchimbika kwa kifusi kilichowekwa. Vile vile, kuendelea kuchelewesha utiaji wa lami katika barabara hii, kunaendelea kuleta adha na athari kubwa kwa wananchi waishio pembezoni mwa barabara hiyo kutokana na mavumbi jambo ambalo licha kuharibu afya zao inasumbua hadi kwenye mapishi yao wanakula vumbi usiku na mchana ,adha kwa watumiaji pamoja na wananchi wanaishi pembezoni mwake kuendelea kuteseka kiafya na kimazingira.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imegundua changamoto kubwa mbili katika mradi huu, moja na hatua ya utiaji wa lami, ni nani atakaetia lami na nyingine ni miundombinu ya mabomba makubwa ya maji yuliyoko kwenye barabara hiyo ambapo kamati yangu ilijitahidi kusaidiana na wizara hii ya Miundombinu kuwakutanisha na Wizara ya Ardhi ,Maji, Nishati na Mazingira tunawashukuru Mawaziri wa Wizara hizi mbili pamoja na manaibu wao pamoja na Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara kwa mashirikiano waliyoyatoa kwa Kamati ili kukwamua tatizo hilo na walituahidi katika kikao hicho kulitatua suala hilo kwa haraka ili kazi iweze kuendelea, tunaitaka Bodi ya Mfuko wa Barabara kutoa fedha kwa haraka ili mradi ukamilike, mara nyingi tumekua tukilalamika kuchelewa kwa miradi kutokana na kuchelewa pesa kutoka kwa wahisani lakini leo cha kushangaza huu mfuko wa Barabara ni pesa ya Serikali yenyewe pia inakosekana kupatikana kwa wakati na kusababisha mradi kukwama bila ya sababu za msingi, nadhani Mhe Waziri akija atatusaidia wajumbe ni hatua gani imeshafikiwa katika kuondoa changamoto hizo ili mradi ukamilike.
 Mheshimiwa Spika,
Namuomba sana Mhe.Waziri ajitahidi kuwasimamia watendaji wake ili kuikamilisha Barabara hiyo ya fuoni kwasababu Serikali imekua ikisemwa sana na wananchi kwa kadhia ya barabara hiyo badala ya kusifiwa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa barabara hizo jambo ambalo halipendezi kwa Kamati yetu na naamini hata kwa Waziri mwenyewe, na kwa moyo aliotuonyesha kwa muda mfupi tulipoanza kufanya kazi nae tumemuona ni kiongozi makini na ana nia ya kuondoa changamoto za Wizara kwa muda mfupi sana.
PROGRAMU YA MIPANGO NA UTAWALA KATIKA SEKTA YA UJENZI, MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na nia njema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwaendeleza wananchi wake na pamoja na jitihada zake za kuimarisha huduma mbali mbali za Kijamii, Kitaifa na Kimataifa. Bado, kuna haja ya kujitathmini, kujiridhisha na kuwa makini kabisa wakati wa kuingia Mikataba ya Miradi mikubwa ya kimaendeleo. Kwa kweli, utafiti na upembuzi yakinifu pamoja na ushirikishwaji wa wadau ni vitu vya msingi ambavyo vinaweza kusaidia wakati wa uwanzishwaji wa Miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imekagua Ujenzi wa Jengo jipya la Abiria (Terminal 2) katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar. Kwa kweli malalamiko na manung’niko mengi kuhusiana na kutoridhishwa na mwenendo na utekelezaji wa Mradi huu. Ujenzi wa Mradi huu umekuwa ukizungumzwa kwa muda mrefu sasa,  sio tu na Wajumbe wa Baraza lako tukufu, bali pia  na watalamu mbali mbali wa majego pamoja na wadau wa masuala ya usafiri wa Anga.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imegundua kwamba, kulikua na mapungufu kadhaa katika mchoro wa awali ikiwemo maegesho ya ndege kuwa karibu mno na jengo la abiria pamoja na njia ya kurukia ndege (Run way) kuwa juu kuliko jengo lenyewe, jambo ambalo linaweza kuleta usumbufu na uharibifu mkubwa wa mali na vifaa hapo baadae wakati wa mvua kubwa kama hazijachukuliwa hatua za dharura ikiwemo kujenga mtaro wa kutolea maji ya mvua ili kuondoa tatizo hilo, pamoja na Kamati yangu kuambiwa kuwa mtaro utajengwa na kuyapeleka maji kwenye bwawa la kuhifadhia maji ya mvua lakini kamati yangu haijaridhika na hatua hiyo kwani inaonyesha itakua ni hatua ya dharura bali tunashauri uwepo mradi mwingine maalum kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wa kuyatoa maji ya mvua uwanjani kuyapeleka hadi pwani ( Baharini). Hiyo ndio itakua ufumbuzi wa kudumu kwa kuyaondoa maji ya mvua hapo uwanjani.
Mheshimiwa Spika,  
Kutokana na chanagamoto hizo, Kamati haikuridhika na mwenendo mzima wa Mradi huu, Mradi ambao awali  ulianza kwa dola za Kimarekani 70,400,000 (2009) na kufanyiwa marekebisho (June 2012)  kwa kuongezwa Dola 11,828,674.71 na hatimae  Aprili, 2014 ulifanyiwa  marekebisho mengine  na kuongezwa tena Dola 46,518,414.80  na kufanya jumla kuu kufikia Dola za Kimarenani 128,747,089.51. Hiki ni kiwango kikubwa sana cha fedha kwa mradi mmoja jambo ambalo sisi wajumbe tangu ulipoanza mradi huu tulianza kutilia mashaka jinsi ya ushirikishwaji wa wadau mbali mbali jambo ambalo lilitawaliwa na manung’uniko miongoni mwa watendaji wa Serikali na hata Wajumbe kuzuia Bajeti kutokana na kizungumkuti cha mwenendo wa mradi huu, pamoja na hayo lakini Kamati yangu inamtaka Mhe. Waziri kuwa jasiri na makini zaidi  na kuangalia changamoto hizo lakini cha msingi sasa tunataka mradi ukamilike na tuanze kuutumia kwa maslahi ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
 Tunamuomba sana Mhe.Waziri, kuisimamia miradi ya Wizara kwa karibu zaidi kwani tumeona karibu miradi yote ya Wizara hii imekua ikiongezeka gharama zake kila siku ukiangalia hili sio jambo la kudharau hata kidogo.
Mheshimiwa Spika,
 Jambo jingine katika Mradi huu wa (Terminal 2) ni changamoto ya kutokushirikishwa kwa wadau mbali mbali ambao watakaoutumia Uwanja huo tokea mwanzo, lakini pamoja na hayo Kamati yangu inaitaka Wizara kuhakikisha inaitisha vikao mbali mbali vitakavyowashirikisha wadau wote ikiwemo Mamlaka yenyewe ambayo ndio watakaokuja kukabidhiwa jengo hilo ili kuanza kupanga ni namna gani wataweza kuja kuutumia na kuudhibiti uwanja huo, changamoto nyingine kamati yangu iliyoiona ni kiwango kikubwa cha Umeme kitakachokuja kutumika katika kuendeshea kiwanja hicho na utaratibu wa mapato na matumizi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege baina yao na Wizara ya fedha, na hili ni vyema katika hivyo vikao vyao tunavyowashauri  Wizara basi na hili muanze kulizingatia mapema ili kuepuka usumbufu hapo baadae. Pia Kamati yangu inaishauri Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuliekea kinga ya Bima ya ajali ya moto jengo hilo kwani ni jengo la gharama kubwa kwa hiyo ni vyema kuliekea tahadhari mapema, kwani mfano mzuri hivi karibuni katika nchi jiraji ya Kenya kiwanja cha JomoKenyatta Airport kiliungua moto lakini kwa kua kiwanja kimekatiwa Bima basi kiliweza kukarabatiwa kwa muda mfupi na kuendelea na kazi kama kawaida, lakini pia kwakua kiwanja kitatumika na wageni mbali mbali pamoja ndege kubwa za kimataifa basi ni lazima kiwanja kiwahahakikishie wadau wote wataokitumia kuwa kiko katika hali ya usalama mkubwa wakati wote.
Mheshimiwa Spika,
Kitabu cha Mheshimiwa Waziri  pia kinaonyesha kupungua kwa Tani za Mizigo iliyohudumiwa kwa mwaka huu, ambapo walihudumia  Tani 1,397  ikilinganishwa na Tani 1,439 mwaka jana  kwa madai ya kupungua kwa idadi ya ndege maalum za Mizigo. Kamati inaomba kupatiwa maelezo ya kina juu ya mapungufu haya na namna ya Mamlaka ilivyojipanga kukabiliana na tatizo hilo kwani tunategemea kila kiwanja kinavyoboreka basi iendane na makusanyo yatakavyoongezeka.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu Uwanja wa Ndege wa Pemba, Kamati  inaipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kukamilisha Mradi wa Utiaji wa Taa za Kuongozea Ndege  wakati wa kutua na kuruka  katika kiwanja hicho. Hata hivyo, Kamati haijaridhika na matumizi ya kiwanja hicho kwani hadi hivi sasa hakuna ndege yoyote inayotua ama kuruka baada ya jua kuzama. Uchunguzi wa Kamati umebaini kwamba, hali hii inakuja kutokana na kwamba Makapuni yanayotoa Huduma za Usafiri wa ndege kuleta ndege zenye Injini na propela moja tu, ambazo haziruhusiwi kuruka baada ya jua kuzama. Kutokana na kadhia hii, Kamati inachukuwa fursa hii kuiomba Serikali kuwashajihisha watu wa Kampuni za ndege kuleta ndege ambazo zinaweza kutoa huduma hata baada ya jua kuzama. Aidha, Kamati pia inasisitiza juu ya uimarishwaji wa usafi pamoja na vitendea kazi katika Uwanja wa ndege wa Pemba kwani hali ilivyo hivi sasa bado haiiridhishi. Pia Kamati yangu imepata taarifa tangu taa hizo kutiwa hapo kiwanjani basi hakuna ndege iliyowahi kwenda huko usiku, kwa hiyo bado tunashauri Wizara kuhakikisha kila inapokusudia kufanya maboresho katika maeneo yake basi ni vyema kuwashirikisha wadau ili kuweza kupata ushauri wa uwekaji wa miundombinu na kupata matokeo mazuri wakati wa matumizi ya miradi yao. Ndio maana tukasema hata huo uwanja Mkubwa basi washirikishwe wadau wote ikiwemo Mamlaka yenyewe na taasisi binafsi zitakazokuja kuutumia uwanja huo, kwani hata sekta binafsi zinamawazo mazuri ya kuboresha huduma za Viwanja vya Ndege na maeneo mengine. Lakini pia kamati yangu inaishauri Serikali isione taabu kuingia mikataba ya (PPP) katika kuundesha uwanja wa Ndege Terminal 2 kwani utahitaji uangalizi wa hali ya juu na maarifa makubwa ya kuuendesha uwanja huo, lakini pia kwa kuzingatia matumizi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa kupewa heshima zao maalum kwenye mikataba hiyo. Kwani Uwanja huo ni mali ya Umma.
PROGRAMU NDOGO YA MIPANGO NA SERA KATIKA SEKTA YA UJENZI, USAFIRI MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inalipongeza sana Shirika la Bandari kwa kazi nzuri za kutoa huduma za kuzihudumia Bandari zetu za Unguja na Pemba, pamoja na changamoto za ubaba wa fedha za kununulia vifaa vya kisasa katika kuendeshea kazi zao, Kamati ilipokea maelezo kua wakati mwingine inapohitaji mkopo kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar inabidi kutumia pesa zao za ndani jambo ambalo linarejesha nyuma Shirika letu. Kutokana na taarifa hiyo, Kamati yangu inamuomba Waziri kupitia Katibu wake Mkuu ambae ni mzoefu wa masuala ya Bandari kulisaidia Shirika kupata fedha hizo na ikiwa kuna ugumu kwa PBZ Basi wasiogope kwenda kwenye mabenki mengine kukopa ili kujiimarisha kihuduma na kibiashara, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Shirika wanayohaki ya kukopa, kushtaki na kushtakiwa, kwa hiyo suala la fedha kisiwe kikwazo cha kukwamisha shughuli zao.
Mheshimiwa Spika,
Shirika la Bandari ni lango kuu la kuingilia mizigo yote hapa Zanzibar kutoka nchi za nje, lakini bado Bandari zetu zina mapungufu makubwa sana katika vitandea kazi hasa Crine za kisasa ambazo zingeliweza kupakua mizigo kwa haraka, lakini pia Shirika lina changamoto kubwa ya mahala pa kuhifadhia Makontena. Jambo ambalo pia husababisha usumbufu mkubwa wa msongamano hapo Bandarini, kwani pale kwenye uwanja wa Hoteli ya Bwawani yalipokua yakihifadhiwa hivi sasa eneo hilo haliwezi kutumika tena, kwa hiyo tunalitaka Shirika kutafuta eneo jingine mbadala la kuhifadhia makontena ili kuondoa usumbufu kwa wafanya biashara wenye makontena.
Mheshimiwa Spika,
Lakini pia namuomba Mhe.Waziri akija aje kutusaidia ufafanuzi hivi karibuni kampuni moja ya meli CMC inayoleta Makontena hapa Zanzibar walitoa circular kwa wateja wao kua kunaongezeko la karibu USD 200 kwa Kontena kutokana na conjestion ya Makontena hapo Bandarini, je suala hili ni kweli? Na kama ni kweli je Shirika limechukua hatua gani kuihami hali hiyo.Kwani ongezeko ya bei ya usafirishaji pia huathiri bei za bidhaaa hapa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Pia, Kamati yangu inaipongeza Serikali kupitia Shirika la Bandari kwa ujenzi wa Gati ya Tumbatu lakini inaiomba Serikali kwenye Bandari ya mkokotoni kuweka utaratibu mzuri wa kudhibiti mizigo na abiria wanaoingia pale kwani kuna mapato mengi ya kodi ya Serikali hayakusanywi na pia kuna watu huingia kiholela kupitia Bandari hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kuwa Kamati yangu haijapata nafasi ya kuitembelea Bandari ya Pemba lakini tunaishauri Wizara kupitia Shirika kutafuta Crine kubwa katika Bandari ya Pemba kwani inaleta usumbufu mkubwa hasa kunapotokea mizigo mikubwa pale Bandarini. Pia, Kamati yangu inalitaka Shirika kuangalia uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wavuvi huko kwenye mnara wa matumbini ili usije kuleta athari kwa mnara ule.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inachukua fursa hii tena kuipongeza Serikali kwa kwa kusikia kilio cha Wajumbe wa Baraza lako tukufu liliopita kwa kuitaka Serikali kununua Meli yake ya kubeba abiria na mizigo hasa baada ya kuona ajali za baharini zimekua nyingi na za kutisha kutokana na upungufu wa vyombo vya usafiri wa Baharini jambo ambalo lilipoteza maisha ya wananchi wengi pamoja na mali zao kwa mashirikiano na kuliomba Baraza kuruhusu kukata matumizi ya viburudishaji na vinywaji kwenye bajeti za Wizara na tukaweza kufunga mikanda na leo tunajivunia kua tumeweza kununua meli ya MV. Mapinduzi II. Ambayo hivi sasa inaendelea na safari zake kama kawaida. Hata hivyo, kumekuwa na taarifa tofauti kuhusiana na upakiaji wa Mizigo ndani ya meli hiyo, inasemekana hivi sasa meli hiyo inashindwa kupakia baadhi ya mizigo ikiwemo magari. Kutokana na taarifa hizo, Kamati inahitaji Maelezo ya kina juu ya kadhia hiyo. Vile vile, Kamati inashauri kuangaliwa upya kwa utaratibu wa ukusanyaji wa mapato ya meli hii kwani kunataarifa kwamba wanaosimamia meli hii sio wanaokusanya mapato hayo, jambo ambalo Kamati yangu haijafurahishwa nalo kwani inaweza kuleta usumbufu mkubwa hasa katika kuihudumia Meli hiyo. Kamati yangu inaitaka Wizara kuwaekea misingi watendaji wa Shirika, ili kuweza kudhibiti mapato yake na pia kutumia kufuatana na taratibu za Shirika zinavyosema ili kuhakikisha Meli hiyo inakua safi, na kutoa huduma bora kwa wananchi kama inavyotarajiwa.
PROGRAMU YA UHIFADHI WA MJI MKONGWE NA UIMARISHAJI WA MAJENGO YA SERIKALI NA BINAFSI
Mheshimiwa Spika,
Shirika la Nyumba imepandisha kodi ya nyumba kutoka shilingi 25,000/= kwa mwezi hadi shilingi 75,000/=. Kiwango hiki ni kikubwa ukizingati kwamba wengi wa wapangaji hao ni wa kipato cha chini. Kamati inaitaka Wizara kukaa pamoja na watendaji wa Shirika hilo ili kufikiria upya mabadiliko hayo kulingana na vipato vya wananchi wetu, pamoja tunajua kua Shirika linahitaji kujitegemea lakini pia tufikirie na wengi ya wanaoishi ni wananchi wenye kipato cha chini ,tunashauri kupandisha kodi kwa ghafla kwa asilimia 150 sio jambo sahihi kuzingatia hali ya watu wetu, isipokua kwa zile nyumba zinazotumika kibiashara kama maduka, mikahawa  na biashara nyengine hizo wangeliweza kuwapandishia kodi kiasi hicho au hata zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaelewa mzigo mkubwa uliokabidhiwa Shirika la nyumba kuanzishwa likiwa na nyumba karibu zote zimesha chakaa na zinahitaji mtaji mkubwa ili kuzirejesha katika ubora wake wa asili na ukarabati huo unahitaji pesa nyingi tungeliishauri Serikali kulipatia mtaji Shirika hilo ili kutafuta nguvu za kujitegemea kibiashara na kutoa huduma za makaazi, vinginevyo kuwabebesha mzigo huo kwa ghafla wananchi wetu kwakweli sio sahihi na huo ni mtihani wetu sote. Pia tunalishauri Shirika hilo kubuni miradi kwa kushirikiana na taasisi za fedha za ndani na nje ili kujenga majengo kwa ubia na wateja mbali mbali ili kuweza kujenga majumba ya kisasa na kuweka miji yetu katika sura nzuri kama inavyotakiwa, kamati yangu pia inalitaka Shirika kuzifanyia ukarabati nyumba za maendeleo zilizojengwa na uongozi wa awamu ya kwanza kwani baadhi yao hivi sasa zimeanza kuhatarisha maisha yao, vilevile kamati yangu inataka Shirika lipige marifuku wale wapangaji wote kwenye nyumba za maendeleo kuacha mara moja kuzivunja nyumba hizo na kutia milango ya nyuma na milango ya biashara bila kushirikisha Shirika lenyewe kwani hupelekea kusababisha kupunguza uimara wa majengo hayo, kwani wengine hufanya Saloon, milango ya nyuma n.k.
Mheshimiwa Spika,
Mji Mkongwe ni moja ya miji ya urithi wa kimataifa, na ni hazina kubwa Mwenyeenzi Mungu aliyotujaalia, mji huu umekua ni sehemu moja ya vivutio vya wageni kuja kutembelea Zanzibar, mji huu umekua ukiipatia nchi yetu mapato mengi ya pesa za kigeni, lakini pia wasomi wengi wa Historia wamekua wakija kuutembelea na kufanya research zao kupitia Mji Mkongwe wa Zanzibar, mji huu umehifadhi majengo makongwe ya kihistoria ambapo yalijengwa karne nyingi zilizopita, kwa hiyo ni mji ambao unaopaswa kuhifadhiwa, kulindwa na kudumishwa na wazanzibari sote ili kulinda hazina hiyo, kwa nchi za wenzetu kama vile Misri imekua  ni moja ya kiingizio kikubwa cha mapato kwa nchi zao kutokana na kuvitangaza vivutio vyao vya kihistoria ikiwemo majengo na rasilimali zilizomo kama kumbukumbu za matukio ya Nchi zao.
 Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaitaka Mamlaka kupitia Mhe. Waziiri wamejipanga vipi kuuhifadhi mji huo hasa kutokana na ujenzi wa majumba mengi ya kisasa yanayojengwa katika mji huo ambayo hayaendani na uasilia wa majengo hayo, lakini isitoshe Kamati yangu inaendelea kusikitishwa sana na kuona kua jengo la Mji Mkongwe limefikia hali ya kuanguka sehemu ya jengo hilo na hadi leo limeshindwa kukarabatiwa, na pia Kamati yangu inataka majibu kutoka kwa Waziri, je? Fedha zinazopatikana kutokana na jengo hilo zinadhibitiwa na taasisi gani? Na kama kuna taasisi inayokusanya mapato ya hapo ilikuaje hadi jengo kufika kubomoka bila kufanyiwa ukarabati kwa wakati. Pia, Kamati yangu inaitaka Wizara kuhakikisha jengo hili linakarabatiwa na kulirudisha katika hali yake ya kawaida.
Mheshimiwa Spika,
 Pia, Kamati yangu inataka kujua katika Mji Mkongwe, kuna majumba mangapi yanayohifadhiwa, pia je yako majengo katika Mji Mkongwe hayamo katika uhifadhi, je kwa kua kuna idadi kubwa ya nyumba za Mji Mkongwe ambazo zimechakaa na hazifai kuishi binaadam kwa usalama wao lakini vado nyumba hizo zinaendelea kuishi watu je ni hatua gani za kisheria zinachukuliwa ili kunusuru maisha yao, na kama ikitokezea jumba limeanguka na kuathiri maisha yao je Mamlaka ya Mji Mkongwe inawajibika vipi?
Mheshimiwa Spika,
Kabla sijamalizia hotuba yangu, napenda sasa kuwashukuru Waheshimiwa  Wajumbe wote kwa kunisikiliza kwa makini na utulivu, pia napenda kukushukuru kwa mara nyengine tena wewe binafsi kwa kuniruhusu kutoa maoni ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi kuhusiana na Bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo, napenda kutamka kwa niaba ya Kamati ya Mawasiliano na  Ujenzi na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Shaurimoyo, naunga  mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji. Aidha nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wote wachangie na wakosoe na kushauri pale penye kasoro ili ikipita iwe Bajeti yetu sote na tumpe nguvu Waziri wetu msikivu kwenda kuyatekeleza yale tuliyomuelekeza na yale aliyotuomba tumkubalie akayatekeleze kwa maslahi ya wananchi wetu na Taifa letu kwa ujumla. Na hatimae nakuombeni  Waheshimiwa Wajumbe wenzangu wote wa Baraza hili tukufu kuunga mkono Makadirio ya Bajeti ya Wizara hii kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu na malengo waliyojipangia.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha.
Ahsante,

Hamza Hassan Juma,
Mwenyekiti
Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

.

1 comment:

  1. Je si uzembe na ubadhirifu huu ? Mradi unaongozeka gharama na Hamna aliefikishwa mahakamani kujibu, au kuwajibishwa ni Sawa na ule mradi wa e-government wa smz ambapo ulikamilika na ukagundulika na kasoro tele ila wasimamizi wakasema " mara hii hatutafanya makosa ". Je wanajua kwamba watu hata mlo mmoja unawashinda ? Je hizo fedha za wananchi wanazitumia kama si za mtu ? Au ndo Ukiwa mkuu katika smz ufanye utakavyo kwenye fedha za maskini?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.