Habari za Punde

Mwakilishi wa Jimbo la Mhaonda Balozi Seif Ali Iddi akisaini mkataba wa kupokea msaada wa shilingi zaidi ya Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na Ubalozi Mdogo wa China hapa Zanzibar kwa ajili ya uimarishaji wa Sekta ya Elimu Jimboni kwake.
Aliyesimama ni Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo  Zanzibar Bwana Xie Yunliang  anayemaliza muda wake wa kazi za Kidiplomasia hapa Zanzibar. 
Balozi Seif akipokea Hundi ya fedha ya zaidi ya shilingi milioni ishirini kutoka kwa Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo  Zanzibar Bwana Xie Yunliang kwa ajili ya uimarishaji wa Sekta ya Elimu katika Jimbo lake la Mahonda.(Picha na – OMPR)
Na. Othman Khamisd OMPR. 
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif ALI Iddi leo ametia saini Mkataba  wa kupokea msaada wa zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na Ubalozi Mdogo wa China hapa Zanzibar kwa ajili ya uimarishaji wa Sekta ya Elimu Jimboni kwake.

Hafla ya utiaji saini Mkataba huo wa kupokea hundi ya Fedha hizo imefanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar ambapo kwa upande wa Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar saini ilitiwa na Balozi Mdogo wake Bwana Xie Yunliang.

Akikabidhi Hundi hiyo Balozi Xie Yungliang alisema Ofisi yake imeamua kuchangia msaada huo kufuatia juhudi kubwa zinazoshuhudiwa kutekelezwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif katika kusimamia uimarishaji wa miradi ya Maendeleo hasa Sekta Mama ya Elimu.


Alisema Ofisi yake licha ya yeye kumaliza kazi yake ya Kibalozi hapa  Zanzibar lakini watendaji watakaoendelea kubakia watawajibika kusimamia vyema mahusiano yaliyopo kati ya Nchi yao na Zanzibar kwa maslahi ya Wananchi wa pande zote  mbili.

Akipokea Hundi hiyo Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alimshukuru Balozi Xie Yunliang kwa moyo wake wa upendo wa kusaidia kuimarisha sekta ya elimu yenye umuhimu katika kila kitu miongoni mwa Jamii.

Balozi Seif amekuwa na mpango maalum wa kuinua Kiwango cha Elimu ndani ya Jimbo analoliongoza kazi ambayo pia aliisimamia vyema wakati akiwa Mbunge wa lililokuwa Jimbo la Kitope akijizatiti pia kuiendeleza katika Jimbo Jipya la Mahonda akiwa katika nafasi ya Uwakilishi.

Zipo skuli za Sekondari ndani ya Jimbo la Mahonda ikiwemo ile ya Kitope, Mahonda yenyewe pamoja na Fujoni ambazo bado zinahitaji msukumo katika kuzijengea mazingira bora ya kufundishia hasa Maktaba, Maabara pamoja na mitandao ya mawasliliano ya Kompyuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.