Habari za Punde

Tamko la THBUB Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2016

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Salma Ali Hassan akisoma tamko la Tume mbele ya vyombo vya habari, ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16, 2016. Wengine ni Kamishna wa Tume, Mhe. Dkt. Kelvin Mandopi (mwenye suti) na Bwana Francis Nzuki, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Tume.


TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
                                                                                                 
Juni 16, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2016

Tunapoadhimisha kumbukumbu ya siku ya mtoto wa Afrika hii leo Juni 16, 2016 ikiwa ni mara ya 26 tangu uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uizindue siku hiyo mwaka 1991, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), inatoa wito kwa umma, Serikali na wadau mbalimbali wa haki za watoto kuunganisha nguvu kupinga vitendo vyote vya ukatili wanavyofanyiwa watoto mahali popote Tanzania.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inasikitishwa na kukerwa na matukio ya ukatili wa aina mbalimbali wanayofanyiwa watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari. Matukio hayo yanajumuisha: kutupwa kwa watoto wachanga, ubakaji, ulawiti, ukeketaji, mauaji, na watoto wa kike kuozwa katika umri mdogo, hivyo kuwanyima haki zao, hususan haki ya kupata elimu. Matendo haya yenye kuvunja haki za watoto yanafanywa na watu wazima wenye akili timamu.

Tume inalaani kwa nguvu zake zote ukatili wa aina yoyote wanaofanyiwa watoto. Hivyo inawataka wananchi kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapewa malezi na makuzi stahiki katika familia na jamii. Pia wanalindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na wanapata fursa katika maendeleo ya ustawi wao.

Hatua hii ni muhimu kwani maendeleo ya Taifa lolote duniani yanawategemea watoto. Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa  idadi ya watoto nchini Tanzania ni zaidi ya asilimia 50 ya watu wote. Kwa hiyo, jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili na kuwapa fursa ya maendeleo ya ustawi wao halina mjadala. Jukumu hili ni la kila mmoja wetu ikiwemo familia, jamii na Serikali.

Tume inasisitiza kwamba binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Haki hii ya usawa inatambuliwa katika ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na mikataba ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika (AU) na kimataifa.

Nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba hii ya kimataifa na kikanda na kutunga sheria mbalimbali za kuharamisha makosa ya ukatili dhidi ya binadamu. Miongoni mwa sheria hizi ni Sheria ya Mtoto, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sheria  ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.

Hivyo, vitendo vya ukatili vikiwemo vitendo vya ubakaji, ulawiti, na ndoa za utotoni, haviwezi kuendelea kutendeka huku Serikali, wananchi na wadau wa haki za binadamu wakitazama bila kuchukua hatua.

Ni wajibu wetu sote, kuchukua hatua stahiki kuwalinda watoto; na Serikali kupitia vyombo vyake iendelee kushughulikia kesi za watoto kwa haraka zaidi.

Katika kuyapa kipaumbele masuala ya watoto mwaka 2007 Tume ilianzisha dawati maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya watoto nchini, yakiwemo malalamiko mbalimbali ya uvunjwaji wa haki za watoto.

Katika kufuatilia malalamiko ya watoto hasa yanayohusu ulawiti na ubakaji, Tume imebaini  changamoto mbalimbali, zikiwemo: upelelezi wa kesi hizi kuchukuwa muda mrefu, jamii kutokuwa na hamasa ya kupinga vitendo vya ubakaji na ulawiti, na kutowapeleka watoto hospitali mara inapogundulika wametendewa unyama huo, jambo ambalo hupoteza ushahidi.

Aidha, wahusika huwatishia maisha watoa taarifa, na wakati mwingine kwa kuwa matukio mengi yanawahusisha wanafamilia au watu wa karibu, hivyo ndugu hao hukaa na kusuluhishana nje ya mahakama.

Changamoto nyingine ni baadhi ya madaktari kutotoa ushirikiano wa kutosha katika mashauri haya, na ucheleweshwaji katika kusikiliza kesi hizi.

Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatoa mapendekezo yafuatayo:
1.        Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu ubakaji na ulawiti wa Watoto, kufanya upelelezi thabiti na kuwakamata wahusika, na kuwafikisha mahakamani kujibu mashtaka.

2.        Madaktari katika hospitali mbalimbali kuyapa kipaumbele matukio ya ulawiti na ubakaji na kuwasaidia wahanga wa vitendo hivyo, hasa katika kutoa ushahidi mahakamani.

3.        Mahakama ziharakishe usikilizaji wa kesi za ubakaji na ulawiti na kutoa hukumu kwa wakati.

4.        Wananchi, jamii, kamati za ulinzi na usalama kwa ujumla watoe ushirikiano kwenye vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa watoto kama vile ndoa za utotoni, ubakaji na ulawiti wa watoto.

5.        Wazazi na walezi waache kuharibu mwenendo wa mashauri ya ubakaji na ulawiti kwa kukubaliana na wabakaji nje ya vyombo vya sheria hivyo kupoteza ushahidi.

6.        Wazazi watakaobainika kulinda uhalifu kwa kutotoa taarifa wachukuliwe hatua za kisheria.

7.        Wazazi na walezi wawe makini na mienendo ya watoto ili kubaini mabadiliko ya kitabia.

8.        Wazazi/walezi wawe karibu na watoto na kujenga urafiki nao ili kuwafanya waweze kutoa taarifa zozote zisizo za kawaida kwa urahisi.

9.        Wazazi/walezi wachunguze mahusiano ya mtoto na jamii ya nyumbani na nje ili kubaini viashiria vya udhalilishaji wa watoto au vitendo vya ukatili na kuvizuia kabla havijatokea.

UBAKAJI NA ULAWITI KWA WATOTO VINAEPUKIKA:
Chukua hatua kumlinda mtoto!

Imetolewa na:
(SIGNED)

Salma Ali Hassan (Kamishna)

Kny. Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Juni 16, 2016

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.