Habari za Punde

Utafiti: Vikwazo vinavyowakabili wanawake kufikia malengo ya uongozi wa kisiasa

1.0.UTANGULIZI

MIONGOZO ya Dunia katika kupigania haki na Ujenzi wa Demokrasia ya kweli kupitia taratibu na mifumo mbali mbali ikiwemo ya Uchaguzi inazingatia na kuhimiza sana usawa na uwiano wa kijinsia.

Mifumo hii inataka kuwepo nguvu zinazolingana ama kuwiana katika vyombo vya maamuzi kati ya wanawake na wanaume wanaomba na kupewa madaraka ya uongozi wa kiasiasa na hata katika ngazi za uteuzi.

Lakini licha ya kuwepo mazingatio hayo kwa mitazamo na maudhui ya kimataifa ni dhahiri kwamba bado wanawake wanakumbana na changamoto za vipingamizi kadhaa wa kadhaa katika kufikia matarajio ya kushika madaraka na uongozi wa kisisasa.

Hali hiyo imekuwa ikichangiwa na sababu tofauti likiwemo mifumo  inayotokana na tamaduni kandamizi kwa baadhi ya jamii zinazowapunguzia uwezo na kuwapa ukomo wa madaraka wanawake na hivyo kuonekana kwamba bado wanawake hawajaweza kuwa na nguvu sawa  na wanaume katika kushika madara na dhamana za uongozi katika sura ya kitaifa hata kimataifa.

 Mawazo hayo kwa sasa yanakinzana  sana na  fikrana na mawazo mbadala waliyonayo wanaharakati na taasisi na Jumuiya tofauti Duniani zinazosimamia masuala ya usawa wa jinsia kwa kuhimiza michakato ya kutafuta na kupewa wananchi dhamana na madaraka ya kisasa kwamba ni lazima izingatie tangu hatua ya kisera, kitaratibu na kisheria kuwepo uwiano katika ya mwanamke na mwaname.

Kufanikiwa kwa Kampeni za namna hii kitaifa na kimataifa kunategemea sana upeo wa uelewa na fikra za kimabadiliko kwa wanajamii, lakini  inabidi tuelewe kwamba  kwa kiasi kikubwa mchango wa vyombo vya habari makini unahitajika kufanikisha hilo.


Vyombo hivi hubeba jukumu la ziada katika kuisaidia jamii kuchambua na kuelewa kwamba ili kuchagua kiongozi anayefaa ni kwa kuzingatia uwezo wa kumudu  majukumu na kuchapuza kasi ya maendeleo yao na kamwe kusijali kuwa mwanamke ama mwanamme lakini zaidi  kuzingatia uwezo, ari , kipaji , maadili na moyo wa uzalendo katika harakati za ujenzi wa nchi.Ni kwa msingi huo, vyombo vya habari hivi sasa vinabeba dhana pana zaidi duniani ya kuwa na , sio tu wa kuelimisha na kuburudisha, lakini vinabeba dhamana ya kuwa muhimili wa nne wa dola licha kwamba mihimili mingine ya dola inauona kama sio  na kulibakisha Bunge, Serikali na mahakama kuwa ndio mihimili rasmi pekee ya Dola.

2.0.WAJIBU NA JUKUMU LA VYOMBO VYA HABARI  KATIKA KUSAIDIA  WANAWAKE KUFIKIA MALENGO YA UONGOZI WA KISIASA

Ø  Uandishi wa Habari ni taaluma muhimu iliyobeba jukumu zito la kuihudumia jamii, kwa kuongeza upeo wao wa uelewa, upeo wa kufikiri, utembuzi na pia uwezo  kutambua na kuchambua masuala tofauti yanayohusu jamii yenyewe yakiwemo , maendeleo yao , changamoto zao na hata matatizo  waliyonayo. Na kwamba taarifa zao lazima zilenge kuibua mijadala ya wazi inayowashirikisha makundi yote, lakini mijadala hiyo ni vyema ilenge kuleta suluhisho kwa changamoto na matatizo yaliyopo ndani ya jamii hiyo.

Ø  Matatizo hayo yanaweza yakawa ya kiuchumi, kisiasa ama kijamii na kiutamaduni ambapo katika kikwazo kimoja wapo cha wanawake kutofikia malengo ya uongozi wa kisiasa hutokana na hayo.
Ø  Hivyo basi, taaluma hii inahitaji waandishi mahiri sana wanaofahamu vyema  mila na desturi za jamii zao na mambo yanayoleta vikwazo kwa jamii hiyo, lakini pia lazima waandishi watambue vyema wajibu wao wa kuwajibika kuisaidia jamii na pia kutambua vilivyo misingi na mipaka ya majukumu yao ya kuitendaji na kitaaluma.

Ø  Kwa ujumla, vyombo vya habari vina wajibu wa kuwapasha habari na kuelimisha jamii juu ya masuala mbali mbali yanayotokea ndani na nje ya nchi katika mtazamo wa kuelimisha, kukosoa na kushajiisha utendaji bora, lakini lazima waelekeze juhudi zao katika kuamsha ari na kuibua mijadala yenye tija kwa jamii katika kufikia malengo yakiwemo yale ya wanawake katika kushika madaraka  na uongozi wa kisiasa .

Ø  Pia vijawajibika kuikosoa jamii na viongozi moja kwa moja  na pia kuelekeza jamii pale  haja ya kufanya hivyo inapotokea ili jamii  na viongozi wenyewe waweze kuwa na mabadiliko sahihi yanayohitajika, ambayo sio tu yanajikita katika mitazamo ya ndani, lakini lazima mabadiliko hayo yakidhi haja ya kitaifa na kimataifa kwenye maeneo yote ya siasa , uchumi na utamaduni.

Ø  Aidha katika kufikia malengo ya wanawake ya kushika uongozi wakisiasa na hata nafasi nyengine, waandishi  wa habari wanahitajika kubeba dhamana ya uwajibikaji bora uliotukuka kwa kutenda haki na kuwa wawazi sana katika shughuli zao za kila siku za kuipasha habari jamii kwenye mambo yanayohusu vikwanzo vinavyowakwaza wanawake katika jitihada zao  za kusaka uongozi wa kisiasa na kutimiza kiu na malengo yanayofanana na hayo.

Ø  Kwa ujumla, katika harakati za wanawake kutafuta na kufanikiwa kushika madaraka ya uongozi wa kisiasa, vinapaswas kuwa na kazi zifuatazo za  kuwasaidia wanawake:.

Ø  Kuandika habari zinazohusu  masuala  ya  wanawake katika harakati na mbio za kusaka madaraka ya uongozi wa kisiasa kwa uwazi na zilizotafitiwa kwa kina zitakazoshajiisha kuwajengea ujasiri, ari na uwezo wa kufikia malengo.

Ø  Waandishi lazima kujitahidi kuandika habari za ukweli na zenye uhalisia na zinazoakisi matukio yenye kupiga vita vipingamizi  dhidi ya wanawake katika kila hatua ya michakato ya chaguzi ikiwa ni pamoja na kushajiisha vyema kwa kuchambua sifa na uwezo halisi ili wakubalike, sio tu kwenye jamii ya wanawake, lakini pia kwa jamii kwa jumla.

Ø  Kuhakikisha kwamba wanafuatilia taarifa zinazokwaza jitihada za maendeleo ya wanawake  zinazotolewa  mara kwa mara hasa wakati wa harakati za uchaguzi na hatimaye kuwapa nafasi wanawake kuzungunza mbele ya jamii  kujenga jina na taswira zao kisiasa.

Ø  Ni vyema kwa waandishi wa habari kuaandika sifa halisi za wanawake wanaoweza kupata nafasi za uongozi, sio tu ule wa kisiasa, lakini hata kwa wale wanaoteulewa na mamlaka za uteuzi.

Ø  Ni kazi pia ya waandishi wa habari kufanya kazi kwa  moyo wa kujitolea sana kwa kuwa na agenda makhususi inayolenga maslahi ya wanawake kushika madaraka ya uongzi  wa umma katika ngazi mbali mbali.

Ø  Waandishi ni vyema kutumia vyanzo vya  uhakika vya habari na kutoegemea upande wowote na zaidi waepuke masuala yote yanayoweza kuwa  vyanzo vya ukandamizaji wa wanawake na kuwakosesha haki zao na matumaini ya kushika uongozi.

Ø  Wanahabari wanawajibika pia kuzifahamu kwa kina sheria na taratibu zote zinazoweza kuwa  vipingamizi kwa wanawake sio tu wakati wa uchaguzi ama michakazo ya kusaka madaraka na uongozi wa kisiasa lakini pia  vinavyokandamiza jitihada za kuwajengea uwezo na ujasiri wanawake.

3.0. KAZI ZA VYOMBO VYA HABARI KATIKA  HARAKATI ZA KUWASAIDIA WANAWAKE KUSHIKA UONGOZI WA KISIASA

Kabla kuzungumzia vyombo vya habari kama nguzo ama kiungo muhimu cha kuhimiza na kuchapuza kasi ya harakati za wanawake katika kutafuta na kufikia malengo ya uongozi wa kisiasa , ni vyema kugusia kidogo dhana ya  vyombo vya habari katika kuangalia kazi za vyombo hivyo kwamba ni kuelimisha , kushajiisha na kuburudisha na kukosoa kama majukumu ya msingi.
Lakini, katika kazi ya kukuza harakati za wanawake kidemokrasia vyombo hivi vinapaswa kwenda mbali zaidi katika hatua za kuhakikisha vinatimiza wajibu wa msingi wa  kuchangia kuimarisha, kulinda, kukuza na kuhifadhi pia kuitetea haki za wanawake kidemokrasia wakati wote.

Kwa upande mwengne, kama tujuavyo vyombo vya habari ni daraja ama kiungo muhimu kwa jamii kupata habari na taarifa mbali mbali kutoka kwa watawala na jamii yenyewe. Hivi pia vinajukumu kubwa la kuisaidia jamii katika kuleta mabadiko ya fikra na kufikia maamuzi sahihi yanayohitajika ndani ya jamii kimaendeleo. Mabadiliko hayo huletwa kwa njia mbali mbali kama vile kuelimisha, kushajiisha, kukosoa, kuelekeza na kujenga ushawishi wa kuibua mijadala katika mambo mbali mbali ambayo kimsingi yanapotekelezwa jamii hufahamu na kujirekebisha.  Utaratibu huu ndio unaotambulika kama uandishi wa kuwajibika kwa jamii (social responsible journalism).  Hii ni kutokana na ukweli kwamba jamii bora haiwezi kujengeka  bila ya vyombo vya habari makini na pia inavyoviaminwai sana na jamii  kiasi kwamba wakati mwengine hata viongozi na wanasiasa hukosa imani hiyo ya wananchi.

Katika kusaidia na kuimarisha  uwezo wa wanawake kutimiza kiu ya uongozi wa demokrasia na pia kuwa watekelezaji wazuri wa majukumu ya serikali na uongozi, harakati za wawanawake hapa Zanzibar na kwengineko duniani, vyombo vya habari  ni lazima vikubali kuwajibika ipasavyo katika mambo yafuatayo:.

Ø  Kushajiisha uwajibikaji bora kwa wanawake viongozi

Wanawake viongozi na pia raia  ambao huwa wafuasi wao na wanapaswa kuwajibika vyema tena kwa pamoja ambapo hali hiyo husaidia sana taifa kupiga hatua kwa vile wote kwa pamoja wagubikwa na hisia za uzalendo wa nchi yao kuchapuza  maendeleo bila kujali anayewaongoza ni mwanamke .
Hapa inasisitizwa uwajibikaji bora utaongeza ufanisi, kuzuia rushwa, ubaguzi na  aina zote za udhalilishaji wa kijinsia  na hivyo kukuza ufanisi na maendeleo huku ikizingatiwa sana kutobezwa haki za watu kwa namna yeyote  sambamba na  viongozi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi. Hivi leo mataifa yote ambayo vyombo vya habari vinafanya kazi ya namna hiyo wameweza kupigiwa mfano kutokana na ufanisi unaoweza kupatikana tena kwa kasi kubwa kuliko inavyokisiwa.

Ø  Kupima na kuchambua utekelezaji wa sera za wanawake kiuchumi na Kisiasa

 Kwa kuzingatia ukuaji wa haki za kijinsia katika kusaidia harakati za wanawake viongozi, Vyombo vya Habari vina wajibu wa kuzifahamu sera zote zinazosimamia maendeleo sio tu ya wananwake, lakini pia  kiuchumi na kisiasa . Pia lazima wawe na kipaji cha kuzichambua iwapo sera hizo zina tija, kwanza kwa wanawake na umma kwa jumla. Kufanya hivyo ndio kusaidia upatikanaji wa maslahi  bora kwa watu ili  kazi ya kustawisha na kukuza uwajibikaji na utekelezaji wake kupitia viongozi wanawake uwe na dhamira ya kukuza ufanisi na demokrasia.

Ingawa  ni vyema  kufahamu kuwa wakati mwengine sera za mataifa maskini ikiwemo Tanzania, sera za kisiasa na kiuchumi hugubikwa na msukumo wa mitazamo ya mataifa ya nje na taasisi nyenginezo huku uwezo wa kuzitafsiri sera hizo kiuhalisia na kwa mitazamo ya ndani ukashindikana kwa kuwa hukosekana dira madhubuti ya utekelezaji sera hizo iliyobuniwa na wazalendo wenyewe.  Iwapo vyombo vya habari vitatimiza ipasavyo wajibu huo hapana shaka vitachangia sana kukuza uwezo wa harakati za wanawake sio tu katika Nyanja za uongozi wa kisiasa, lakini pia katika maeneo mengine ya nchi kimaendeleo.
Ø  Waandishi kuisaidia kuinganisha nguvu za wanawake na jamii
Ujenzi wa uwezo wa wanawake bila shaka mtakubaliana name kwamba sio jambo jepesi na ni gharama na mara nyengine inaweza hata kuchangia kuzalisha mifarakano na misuguano isiyo ya lazima miongoni mwa wanawake wenyewe kwa wenyewe, wanasiasa , viongozi wa serikali na hata wananchi hata jamii.
Aidha vyombo  vya habari,  lazima vifanye kazi ya kuhakikisha kwamba wanawasaidia wanawake kwa kuwajenga imani wananchi kutambua mchango wa wanawake na hivyo kuendelea kuwa kitu kimoja kwa moyo safi wakiamini kwamba wanawake wanaweza kulisaidia taifa.
Ø   Vyombo kuwa kiungo madhubuti kati ya viongozi, wanawake na wananchi
Vyombo kufanya kazi hii ni jambo muhimu sana ambapo vyombo vya habari  vikiwajibika kwa umakini  juu ya suala hilo ni dhahiri kwamba nguvu za pamoja katika utekelezaji wa mambo mbali mbali yataweza kufanikiwa. Haitarajiwi vyombo hivi  vikasadia kujenga fitna na uchonganishi  miongoni mwa wanawake na  watawala na watawaliwa na badala yake ni kuhakikisha kwamba vinawajibika kwa kujenga taswira njema miongoni mwa jamii , viongozi  na wanawake wanaotafuta nafasi za uongozi wa kisiasa.
Ø  Kujenga ari kwa jamii kuleta mijadala ya maana kwa  wanawake
Kila mmoja anakiri kwamba mijadala ya wazi inayofanywa na vyombo vya habari kuwahusisha wananchi wa ngazi mbali mbali ni moja ya msingi muhimu wa kukua na kuanuka demokrasia  katika kuwajengea ari wanawake ambapo wananchi hupata nafasi ya kupaza sauti zao na kutoa mawazo , michango na maelekezo yao ambapo huwa  aina moja ya ushiriki na ushirikishwaji na kwamba serikali  sikivu inahitaji sana wananchi kujadili kwa uwazi masuala mbali  yanayowahusu wanawake  binafsi, viongozi wao waliowachagua na hata wale walioteuliwa ili kuona kwamba ni kweli wanawajibika ipasavyo kwa kuzingatia matakwa ya kimahitaji sasa naya baadaye katika harakati za ujenzi wa nchi.

Ø  Kujengea taswira wananchi kuamini na kukubali mabadiliko yanaweza pia kuletwa na wanawake

Vyombo hivi lazima vifanye kazi ya ziada kuwaelimisha na kuwapa ujuzi na mawazo mbadala wananchi kwamba ujenzi wa demokrsia inayozingatia usawa wa jinsia ni matokeo ya mchango wa vyombo vya habari kutimiza wajibu wake ipasavyo, kwani katika hatua za ujenzi wowote demokrasia ni kuamini kwamba hata mwanamke anaweza kuwa na mchango mkubwa na kuwa kiongozi imara wa kushajiisha mabadiliko yanayohitajika.

4.0 VIKWAZO VINAVYOWAKABILI WANAWAKE KUFIKIA MALENGO YA UONGOZI WA KISIASA

Ø  Ubaguzi wa jinsia na kutozingatia Jinsia
Suala la ubaguzi wa kijinsia na kutozingatia jinsia kwa vyovyote vile linabakia kama changamoto kubwa katika jamii kwani wapo watu hadi leo wamekuwa wakiwakosesha nafasi wanawawake kwa sababu tu ya uwanawake wao na kutofahamu umuhimu wa wanawake . Hili ni jambo baya ambalo linahitaji kupigwa vita na wanahabari kwani litakapoachwa litaendelea ni kikwazo kikubwa cha kuwazuia wanawake wenye nia na moyo ama ndoto za kushika uongozi kufifia.
Ø  Kuhakikisha kwamba wajitahidi kupiga vita Rushwa
Suala la Rushwa linachukua nafasi pana katika kuwanyima haki wanaostahiki. Na jambo hili limekuwa likijitokeza sana katika michakato mbali mbali ya harakati za uchaguzi wa hata ule unaoitwa wa kidemokrsaia .
Kutokana na kushamiri kwake limekuwa likiwaathiri sana wanawake kukosa kutimiza ndoto zao kwani ikumbukwe kwamba rushwa ni maovu kama yalivyo mengine ya uvunjivu wa haki za binaadamu , kutowajibika kwa viongozi ama ubadhirifu wa mali za umma. Waandishi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kufichua na kuyapiga vita maovu ya namna hiyo ili kulifanya taifa kuwa na demokrsia ya kweli na wanawake wenyesifa waweze kupata nafasi .
Kwa bahati mbaya hata baadhi ya  waandishi wamekua na mifano kadhaa hapa Tanzania kwamba wapo wamejengea utamaduni wa aina hiyo wa kudai wao rushwa na kuwa wabadhirifu badala ya wao kupiga vita mambo ya namna hii.
Ø  Uwezo duni wa  kielemu na kujieleza kwa baadhi ya wanawake
Hili ni tatizo kubwa kwa baadhi ya wanawake wenye hamu na nia ya kushika dhamana na madaraka ya kisiasa . Inahitajika  kwa jumuiya na taifa kwa jumla kujitolea sana kuwasomesha wanawake ili kuwa na elimu ya kutosha itakayowawezesha kuwa na vigezo vya kiushindani na kuonekana kwamba kiwango chao cha elimu kinafaa na ni cha kinatosha sana kupewa dhamana mbali mbali za uongozi. Vyenginevyo, udhaifu huu unaweza kutumika sana kuwadhalilisha na kuwabagua wanawake wenye nia  na hivyo kusababisha kunyimwa nafasi na fursa wazitakazo kwa wepesi sana.
Ø  Umasikini na kipato duni kwa wanawake waliowengi
Umasikini nao unachukua nafasi nyengine, kwani badala ya mwanamke kufikiria mbinu bora ya ushindani akili yake inakuwa mbali kuangalia mahitaji yake muhimu ya kukidhi maisha ya kila siku. Mwanamke mwenye uwezo mkuwa wa kiuchumi anayo nafasi kubwa kwanza kukubalika ndani ya jamii miongoni mwa wanawake na hata wanaume lakini pia anayofursa muhimu ya kuchangia moja kwa mja kutatua kero za wanajamii na hivyo kuonekana kwamba anafaa sana kuwa kiongozi. Mifumo ya umiliki wa rasilimali inayotoa ridhaa  kwa wanaume kumiliki zaidi nayo inachangia kuwepo kwa hali ya umasikini kwa wanawake waliowengi.
Ø  Ukandamizaji wa baadhi ya mifumo ya utamaduni, mila na silka
Ukandamizaji nao unachukua nafasi pana kwani jamii ya wazanzibari na watanzania kwa jumla bado wanaendelea kuamini na kutumikia mifumo kandamizazaji ambayo haitoi nafasi  kwa wanawake  kutimiza ndoto za masuala yao likiwemo hili la uongozi.
Hadi leo bado zipo jamii kutokana na imani za kiutamaduni, mila na desturi zao zinaamini kwamba kiongozi bora lazima awe mwanamme jambo ambalo sio sahihi kwani tafiti za kitaalamu zinaonesha kwamba hata mashirika na taasisi zinazoongozwa na viongozi wanawake zimepata maendeleo makubwa na ya haraka kuliko zile zinazoongozwa na wanaume.
Ø  Kuwepo misimamo mikali dhidi ya wanawake
Bado ipo misimamo mikali ya dharau dhidi ya wanawake katika jamii. Wapo watu ambao kwa maumbile tu ya wawanawake wao wameonekana kutowajali wanawake na hivyo kuwadharau, kuwakebehi na kuwavunja moyo wanawake wanaopigania mabadiliko ya kimapinduzi ya kukataa mifumo kandamizi ambayo imekuwa ikiwanyima sana haki na fursa wanazozihitaji za kushika madaraka na uongozi wa ngazi mbali mbali mbali.
Misimamo ya aina hii bila shaka ni adui mkubwa wa jitihada za wanawake na inahitaji kupigwa vita ili jamii iondokane na hali hiyo , ingawa suala hili halipo kwa waliowengi kuwa na misimamo mikali dhidi ya wanawake lakini dharau zinazotokana na misimamo hiyo zimekuwa zikileta athari kubwa kwa wanawake.
Ø  Kujiingiza katika makundi
Wapo wanawake ambao hujaribu sana kutengeneza na kujiingiza kwenye makundi , jambo hili limekuwa likiwaacha nyuma wanawake wengi ambalo kwa kiasi kikubwa linashabihiana na ubaguzi kuwaona wengine iwapo hawamo katika kundi fulani basi hawafai. Mathalani imani za makundi ya siasa nayo imekuwa sumu kubwa katika kuwabeza wanawake na hata kubezana wao kwa wao ijapokuwa wengine wanauwezo mkubwa, lakini baada ya kutafautina katika itikadi na imani basi thamani ya mwengine miongoni mwao hushuka na kuonekana kwamba si wamaana licha kwamba inawezekana kwamba akawa na uwezo mkubwa kifikra, utendaji na uwajibikaji.
Ø  Baadhi ya wanawake kukosa ujasiri
 Baadhi yao wanakosa ujasiri na kujiamini. Jambo hili limekuwa likiwaathiri sana kwani ujasiri na kujamini ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya kushika madaraka ya kisiasa sio tu kwa wanawake, lakini hata kwa jinsi nyengine. Wanawake wanapaswa kujitambua na kuwa na ujasiri na moyo wa kujaribu na kujitoa kama walivyo wanaume wakiamini kwamba kushindana kuna kushinda na kushindwa wala kushindwa isiwe ni sababu ya kujipima kwamba ni dhaifu sana na kufaulu ikawa ndio sababu ya uwezo uliotukuka.
Ø  Kutofahamu sera na miongozi mbali mbali inayotetea wanawake
Kikwazo changine ni hichi cha baadhi ya wanawake kutokufahamu vyema sera na miongozo mbali inayotolewa kwa ajili ya kusaidia wanawake kufikia malengo ya kushika uongozi wa kisiasa. Miongozo na sera ni miongoni mwa mambo ya msingi ambayo inaweza kuchangia sana uhamasishaji, ushajiishaji na kuongeza uelewa katika kupigania haki, umoja na usawa wa kijinsia. Kutokufahamika ipasavyo inaweza kuwa kikwazo kikubwa ya mwanamke kutotimiza malengo ya namna hiyo na hivyo kuikosa fursa ambayo engepaswa kuipata.
5.0. CHANGAMOTO KWA WANAHABARI KUWASAIDIA WANAWAKE
Katika kutimiza wajibu wao wa kuwasaidia wanawake  kujikwamua na vipingamizi mbali mbali nchini Wanahabari nao wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika kutimiza wajibu na majukumu yao.
Ø  Uhaba mkubwa nyenzo za kutendea kazi
Ili kufanikisha kazi za uimarishaji wa haki na usawa wa kijinsia kwa waandishi kunahitajika kuwepo nyenzo za kutosha zinazoweza kusaidia utekelezaji wa majukumu yao Ipasavyo . Vyombo vingi na wanahabari wenyewe hawana uwezo kinyezo kutokana na umasikini unaochangia kuwepo bajeti na maslahi duni wayapatayo. Wengi wao hawawezi kuwafikia vyema wanawake hasa wa vijijini katika kuwasaidia pale wanapokuwa na masuala ya msingi ambayo ni muhimu kufahamika na wengi. Maeneo mengi ya vijiji yana matatizo kadhaa wa kadhaa ya kijamiii na kiuchumi ambyo kutatuliwa kwake na serikali ni sehemu ya uimarishaji haki.
Ø  Uwezo mdogo wa utambuzi na uchambuzi wa sera
Ili kutimiza haja ya uwanaharakati wa kuwasaidia wanawake, mwanahabari anapaswa kujiamini katika utekelezaji wa kazi zake kwa kuwa na upeo. Wanapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kutambua na kuchambua mambo mbali mbali zikwemo sera na sheria au taratibu ili kuwa na uhakika na kazi zao.
Kuwa na uwezo huo bila shaka ni kuchangia kukua kwa demokrasia, lakini kwa bahati mbaya waandishi tuliowengi hatuna upeo mkubwa wa mambo ya namna hiyo. Matokeo yake wengi wetu tumekuwa tukifanya kazi za uwakala, wa kuripoti yaliyotendwa kwa kuwatumikia baadhi ya watu kwa maslahi binafisi .
Ø  Rushwa na kukosekana moyo wa uzalendo
Katika kazi ya kujenga  uzalendo na usawa wa kijinsia mwanahabari  lazima achukue nafasi kubwa katika kukabili majukumu yake na ni wazi atakumbana na majaribu tofauti ya kudhoofisha juhudi na uzalendo wake ili alinde maslahi ya mtu ama kundi fulani. Tunaelewa kwamba baadhi ya  waandishi tumejenga utamaduni wa aina hiyo. Ingawa tunaelewa kwamba rushwa ni dhambi kubwa ya kimaadili na ni kosa la jinai lakini limekuwa likijitokeza sambamba na kuwatumikia watu kuwakandamiza wengine.
  6.0 HITIMISHO
Kuwepo kwa mabadiliko ya kujali usawa wa kijinsia yanayopelekea mfumo mbali mbali  iliyozoeleka kubadilika na wakati mwengine kuingiza na kuasisi mipya ya uendeshaji shughuli za uongozi na  kiserikali na dola pia ndiko kunakochangia kuwepo kwa matatizo ya kimazoea na utaalamu juu ya utambuzi wake na mbinu sahihi za kuyakabili . Ikumbukwe kwamba hali kama ya ujenzi na uimarishaji wa haki na uswa wa jinisia, kimsingi kunahitajika jitihada za pamoja katika kuyapatia ufumbuzi  vikwazo , changamoto na matatizo mbali mbali na kuweza kufikia lengo. Lakini ni lazima wanahabari kuwa bega kwa bega na wanawake katika kutimiza wajibu na jukumu lao la msingi la kuisaidia jamii katika kuleta mabadiliko wayatakayo. Haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa Mfumo  mpya na kuachana na ile ya mazoea kitaifa naKimataifa ni muhimu sio tu hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla lakini ni kila kona ya dunia .
Vyombo vya habari vinabaki na nafasi yake muhimu ya kuelimisha, kutoa taarifa, kuhamasisha na kukosoa , kuelekeza na kuchambua mambo yenye maana na tija kwa jamii hasa inayohusu maendeleo ya mfumo mbali mbali ya uendeshaji nchi na haki za wananchi zinavyochungwa, kutunzwa na kulindwa kupitia mifumo hiyo ya uendeshaji wa dola.
Wanahabari bado wanapaswa wabakie kama ni mkombozi pekee , sahihi na imara kwa wanawake kwa kuwa na agenda muhimu inayolenga kusaidia mabadiliko ndani ya jamii .
Jamii inahitaji waandishi wenye ujuzi na maarifa ya kisera, kisiasa na kimazingira pamoja na kufahamu vyema utamaduni, mila na silka za jamii ili kuleta mabadiliko sahahi yanayohitajika.
Aidha, kuna haja kubwa kwa wanasiasa na viongozi kuweka misimamo mizuri ya utetezi, sio tu kwa nadharia, lakini katika utekelezaji wa utetezi  wa kweli unaozingatia maslahi kamili ya nchi na wananchi na kuzingatia sana Usawa na haki za kijinsia kwa kujali  Sheria, haki na kuwajibika ipasavyo kwa kila mmoja. 
Masuala muhimu yaliyojadiliwa katika uwasilishaji  huu yanapaswa kufanyiwa kazi kwa nguvu zote sio tu kwa waandishi wa habari, lakini pia taasisi, wanasiasa na jamii kwa jumla

Ahsanteni Sana.

MAREJEO
·                    Alexander A.J (2003), Taking Sides Clashing Views on Controversial issues in Mass Media. Dushikin Publishing Group, USA.
·        Media Council of Tanzania (2013),Training Manual on Gender and Media.
·        Ayubu Rioba& Fiili Karashani (2002), Write or not to write Ethical concern in Journalism.
·        John. C. (1998), Studing Media, Problem of theory and Method, Mc. Graw Hill, USA.
·        Baraza la Habari Tanzania, (2009), Kupasha habari za Uchaguzi, Ecoprint Ltd. Dar es Salaam, Tanzania.
·        Katiba ya Zanzibar (1984), Toleo la 2010.
·        UNICEF (2003),Haki za Binaadamu, Nyaraka za msingi.Runjiv Kapur
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.