STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 14.06.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa uhusiano na ushirikiano mzuri ndani ya miaka 52
kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China umeweza kuleta mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta mbali mbali za
maendeleo hapa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika mazungumzo kati yake na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa
China aliyeko Zanzibar Xie Yunliang, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
kuaga kufuatia kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa China na Zanzibar zinauhusiano wa muda mrefu
ambao unaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na nchi hiyo kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hizo za maendeleo zikiwemo
elimu, kilimo, afya, viwanda, miundombinu na nyenginezo huku akiipongeza nchi
hiyo kwa kuimarisha uchumi wake.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alimpongeza Rais wa nchi hiyo Xi Jinping kwa kuanza kutekeleza miongoni
mwa miradi waliyokubaliana katika mazungumzo kati yake na kiongozi huyo wakati
alipofanya ziara hapa Tanzania pamoja na Dk. Shein alipofanya ziara nchini humo
kufuatia mwaliko wa kiongozi huyo.
Aidha, Dk. Shein
alitoa pongezi na shukurani za pekee kwa China kwa kuiunga mkono Zanzibar
katika ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mazee huko kiswani Pemba ambapo ujenzi
wake huo unatarajiwa kukamilika kati ya
mwezi Ogasti na Septemba mwaka huu.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa ufadhili pamoja na nafasi za masomo zinazotolewa na nchi
hiyo kwa Zanzibar nazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha
sekta ya elimu hapa nchini.
Pia, Dk. Shein
aliipongeza nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya afya kwa kuendeleza utamaduni wa kuwaleta Madaktari bingwa kutoka nchini
humo wakiwemo kutoka Jimbo la Jiangsu.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa kuwepo kwa ziara za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na viongozi wa siasa kati ya nchi hiyo na Zanzibar zitazidisha kupanua
wigo wa maendeleo kati ya viongozi wa pande mbili hizo.
Dk. Shein alisema kuwa
kumalizika kwa ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha
Abeid Amani Karume kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wageni
wanaokuja kuitembelea Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya
Mashirika ya ndege kufanya safari zao hapa nchini.
Nae Balozi Mdogo wa
Jamhuri ya Watu wa China aliyeko Zanzibar Xie Yunliang ambaye anamaliza muda
wake wa kazi hapa Zanzibar alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea
kuiunga mkono Zanzibar kwa lengo la kuzidisha uhusiano uliopo.
Balozi Xie aliipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa mafanikio
makubwa yaliopatikana katika kuimarisha na kuendeleza sekta za maendeleo na
sambamba na kukuza uchumi Zanzibar.
Balozi huyo
alimuhakikishia Dk. Shein kuwa chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping China
itaendelea kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
mazungumzo yote yaliyofanyika kati ya kiongozi huyo na Dk. Shein yanafanyiwa
kazi ya utekelezaji.
Pamoja na hayo, Balozi
Xie alisema kuwa nchi yake itahakikisha inaendeleza ujenzi wa miradi yote
iliyoanzishwa hapa Zanzibar pamoja na kuendeleeza mengine mipya huku akisisitiza
kuwa ujenzi wa kiwanja cha Mao Tse Tung unaotarajiwa
kuanza hivi karibuni ni fahari kwa nchi hiyo kwani inalitukuza jina la kiongozi
mkuu wa nchi yao.
Aidha, Balozi huyo
alimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa Hopsitali ya Abdalla Mzee iliyopo kisiwani
Pemba unatarajiwa kumaliza kati ya Ogasti na Septemba mwaka huu huku akimueleza
kuwa ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri tayari mchakato wake umeanza pamoja na
ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume
nao umo ukingoni kumalizika.
Balozi huyo mdogo
alisema kuwa China itaendelea kutoa nafasi za masomo na ufadhili kwa Zanzibar
pamoja na kueleza azma ya nchi hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uvuvi wa bahari kuu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment