Habari za Punde

Hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Zanzibar

HOTUBA YA  MAONI YA KAMATI YA MAWASILIANO NA UJENZI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO  NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, MAJI, NISHATI NA MAZINGIRA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu, Mwingi wa Rehema na Mwenye Kurehemu aliyeumba Mbingu na Ardhi, ambaye ametujaalia uzima na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa ndani ya Baraza lako tukufu, tukitekeleza majukumu yetu mbali mbali ya kuwatumikia wananchi wetu ambapo leo tunajadili Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Spika,
Kwa dhati kabisa, napenda pia kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Spika,
Nichukuwe nafasi hii pia kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mheshimiwa Salama Aboud Talib, Mheshimiwa Juma Makungu Juma pamoja na Katibu Mkuu alhaj Alkhalil Mirza na watendaji wengine  wote wa Wizara hii kwa mashirikiano yao ya dhati kwa  Kamati wakati wote tulipokuwa tukipitia na kujadili Bajeti ya Wizara hii. Tunawashukuru sana.



MheshimiwaSpika,
Aidha, napenda kuipongeza tena Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa kuweza kuwasilisha mbele ya Baraza lako tukufu Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa umahiri na ufanisi mkubwa katika mfumo wa bajeti unaozingatia programu “Program Based Budget”(PBB).


Mheshimiwa Spika,
Sitakuwa nimetenda haki iwapo nitaendelea na hotuba hii bila ya kutoa shukurani za pekee kwa Waheshimiwa Wajumbe na Makatibu wa Kamati yangu, ambao tumeshirikiana kwa umoja wetu kuyapitia na kuyachambua makadirio haya ya Bajeti ya Wizara hii na hatimae kuyakubali bila ya marekebisho yoyote.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuheshimu, kuthamini na kutambuwa mchango wao mkubwa kwenye Kamati hii hadi kufanikisha kazi hii iliyokusudiwa, naomba niwataje kwa majina Waheshimiwa Wajumbe na Makatibu wa Kamati hii ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo:-

1. Mhe. Hamza Hassan Juma                               Mwenyekiti
2. Mhe. Suleiman Sarhan Said                              M/Mwenyekiti
3. Mhe. Abdalla Ali Kombo                                 Mjumbe
4. Mhe. Nassor Salim Ali                                        Mjumbe
5. Mhe. Said Omar Said                                        Mjumbe
6. Mhe. Mohamedraza Hassanali                           Mjumbe
7. Mhe. Bahati Khamis Kombo                               Mjumbe
8. Mhe. Kadija Omar Kibano                                Mjumbe
9. Mhe. Mwanaidi Kassim Mussa                           Mjumbe
10. Ndg. Fatma Omar Ali                                    Katibu
11. Ndg. Himid Haji Choko                                 Katibu

MheshimiwaSpika,
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Baraza la Wawakilishi ililiidhinishia Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Matumizi yenye jumla ya Tshs. 7.198, 900,000 bilioni kwa ajili ya Fungu N01 kwa matumizi ya kazi za kawaida. Aidha, Baraza pia ililiidhinishia Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kutumia jumla ya Tshs. 28.750,560,000 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za maendeleo. Vile vile, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara iliidhinishiwa kukusanya jumla ya Tshs. 4,799,625,000 bilioni kama ni mapato yatokanayo na vianzio mbali mbali katika Taasisi zake, ambapo hadi kufikia Machi, 2016 Wizara ilikuwa imeshakusanya jumla ya Tshs. 3,596,948,678 ambazo sawa na asilimia 75% ya makadirio kwa mwaka

MheshimiwaSpika,
Imeelezwa katika hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira imepangiwa jumla ya Tshs.9,555,400,000 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na Tshs. 47,900,786 bilioni kwa ajili ya kazi za maendeleo. Aidha, Wizara inakadiriwa  kukusanya jumla ya Tshs. 6.100,000,000 bilioni kutoka katika vianzio mbali mbali vilivyomo katika Taasisi zake.Aidha, katika utaratibu mpya wa Bajeti inayozingatia Programu (PBB), Wizara hii imepangiwa kutekeleza Programu Kuu Nne (4) na Programu Ndogo Nane (8). Kama zilivyofafanuliwa wakati hotuba hiyo ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu kama Kamati nyingine imefanyakazi ya kuipitia na kuichambua bajeti katika mzingira magumu kwani imekubali kupitisha mipango na bajeti zake bila ya hata kwenda kukagua na kuona hizo shughuli zilizopangwa kutekelezwa hasa kutokana na kuchelewa kuanza shughuli zetu Barazani katika kipindi hiki lakini nnaamini kua kwa Bajeti ijayo tutaweza kumsaidia sana Mhe.Waziri kwa kumpa ushauri mzuri katika kufanikisha majukumu yake.
Kamati yangu pia inasisitiza  Wizara kuwa makini sana na matumizi ya fedha zitakazoingizwa katika Programu hizo kwani licha ya uhaba wa fedha, matokeo ya fedha zitakazoingizwa yatahitaji kuonekana na kupimwa kwa  umakini na ufanisi mkubwa hususan katika utekelezaji wa Programu hizo Muhimu.

PROGRAMU YA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI

Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyoelezwa Programu hii kuwa ina jukumu kubwa la kuhakikisha kunakuwepo upatikanaji wa Huduma bora za Nishati, Umeme na Maji  katika Visiwa vyetu hivi viwili kwa upande wa Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vidogo vinavyoishi watu hapa Zanzibar, kuzingatia na mahitaji ya wananchi wetu. Aidha, kupitia Programu hiiutekelezaji wake ni Usimamizi wa usambazaji wa mafuta nchini, Usambazaji wa huduma za umeme, Uhifadhi wa maeneo ya vianzio vya maji, Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa watumiaji wa mijini na vijijini.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu kupitia Programu hii inapenda kuchua fursa hii tena kuwapongeza Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kupitia Mamlaka yaMaji (ZAWA), kwa jitihada zao kubwa za kuhakikisha kuwa hadi wananchi wanaoishi vijijini kuwa wanapata huduma ya maji safi na salama. Kama tunavyojua kwa upande wa usambazaji maji vijijini kwa hivi sasa Zanzibar inaongoza kwa Nchi za Bara la Afrika kwa kuwafikishia huduma ya maji huko vijini, pamoja kwamba bado kuna baadhi ya vijiji bado havijafanikiwa kupata huduma hii lakini kupitia mradi wa uchimbaji visima wa Raas-El- Khaima tunategemea kwa kipindi kifupi tu cha hapo baadae basi wananchi wengi zaidi wataweza kupata huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyao. Aidha,changamoto kubwa tunayoiona kwa kuvikamilisha visima hivyo kwasababu mkataba wake ni kuchimba visima tu lakini huduma nyingine za ununuzi wa Pump na usambazaji wa mabomba ni jukumu la SMZjambo ambalo bado kutokana na gharama kubwa linaweza kuchukua muda mkubwa kuweza kukamilisha visima hivyo ili kuwezakufanikiwa kutoa huduma hiyo, kwa kua hivi sasa visima vingi tayari vimeshachimbwa kupitia mradi huo na uwezo wa Serikali kupitia Mamlaka kwa hivi sasa ni mdogo kuweza kukamilisha, basi tunamuomba Mhe. Waziri kufanya safari maalum kwenda Raas-El-Khaima ili kufanya mazungumzo zaidi ili Serikali ya Raas-El-Khaima waongeze mkataba mpya wa kusaidia kusambaza maji kupitia visima hivyo, kwani lengo la mradi huo ni kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa maji kwani maji yameshapatikana lakini hayajawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa.



Mheshimiwa  Spika,
Pamoja na jitihada hizo za Serikali kuwasogezea huduma ya maji safi na salama wananchi wake, lakini bado kuna wananchi ambao wanajenga karibu na vianzio vya maji na kupelekea uhaba wa upatikanaji wa maji lakini pia kuchafua maji kutokana na uchafu wa majumbani.

Mheshimiwa Spika,
Kama tulivyoeleza upatikanaji wa maji vijijini umepiga hatua kubwa lakini bado kwa Mkoa wa Mjini na Magharibi hususani Wilaya ya Mjini Unguja bado tatizo la upatikanaji wa maji limekua ni tatizo kubwa kwani kuna baadhi ya maeneo upatikanaji wake ni mdogo sana jambo ambalo linawafanya wananchi wengi kununua maji ambayo hawana uhakika wa ubora na usafi na bila ya kujua yanatoka wapi. Kamati yangu inataka kujua vipi ule mradi wa Japan kupitia Mkoa Mjini naMagharibiambao ulitegemewa kuliondoa tatizo hilo sijui umefikia wapi? Pamoja na changamoto mbali mbali zinazoikabili Mamlaka ya Maji kwa kua kamati yangu haikupata muda wa kuweza kukagua na kujua matatizo ya Mamlaka hii naomba kamati yangu ipewe muda tunaamini kwa mwaka ujao baada ya ukaguzi tutaweza kuishauri vizuri Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ili kuhakikisha wananchi wote ambao mtandao wa maji umepita basi wanapata huduma ya maji kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu inaitaka Mamlaka ya maji kwa kushirikiana na masheha kuandaa utaratibu wa mawasiliano ya karibu ili kutoa taarifa ya mabomba yanayovuja maji kwani kuna maeneo mengi hapa mjini mabomba ya maji huwa yanavuja maji kwa muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati kwa wakati na hii pia hupelekea maji mengi kupotea na kuwakosesha wengine kupata huduma hii muhimu kwa binaadamu.



Mheshimiwa Spika,
Vilevile, Kamati yangu inaitaka Mamlaka kuweza kuwaajiri vijana ambao wapo Wizarani kwa muda mrefu na wengine wanadhamana muhimu lakini bado wapo kama wafanyakazi wa muda bila ya kuajiriwa,hii inaweza kupelekea kutokua waaminifu na kuweza kufanya udokozi kwani hawana uhakika wa ajira yao, Hivyo, Kamati yangu inaitaka tena Mamlaka kuweza kuwapatia posho la usafiri linalostahiki kwa watumishi wao ambao hupangiwa kufanya kazi mashamba kwani mshara wao sehemu kubwa huutumia kwa usafiri jambo ambalo huwarudisha nyuma katika mipango yao ya kimaisha.

Mheshimiwa Spika,
Pia, Kamati yangu kupitia Programu hii inaiomba Wizara husika kuwaongezea uwezo na ujuzi watendaji wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) katika utendaji wao wa kazi za kila siku. Ili kuweza kuondoka na kadhia ya utendaji wa kazi kimazoea hali ambayo kupelekea kuikosesha Serikali mapato kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana katika maeneo yetu ya mjini na vijijini kwa Unguja na Pemba. Kamati inaishauri Mamlaka ya Maji (ZAWA) kuanzisha utaratibu maalum wa ulipaji wa ada yamaji kwa njia ya simu za mkononi ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya huduma ya maji, kwani wakati mwingine mtu huwa anaona taabu ya kufuata maeneo ya kulipia maji lakini kupitia huduma ya simu ya mkononi ni wakati wowote anaweza kulipa bila ya usumbufu wa aina yetote, pia kamati yangu inaitaka mamlaka kuboresha huduma zao za ulipaji bili za maji kwani inaonekana hauko salama sana na unashawishi mkusanyaji kuweza kuchota kwani pesa ina bilisi mbaya, pia tunaishauri Mamlaka ya Maji kutengeneza Database ya wateja wake wote ambao wanaopata huduma ya maji ili kuweza kua na uhakika wa makusanyo wanayoyarajia kuyapata kwa kila mwezi, katika utaratibu huo wanaweza kuweka utaratibu wa kulipa kwa mwaka au kila miezi mitatu au sita jambo ambali litaweza kuongeza mapato na ya uhakika zaidi, pia katika kuboresha mapato na kudhibiti matumizi ovyo ya maji basi Kamati yangu inashauri Mamlaka inunue mita za kusoma maji yanayotumika na kutoa bili sahihi kwa mtumiaji.

Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu inaishauri Mamlaka ya Maji kwa kuweka  mabomba yalioimara ili kuweza kuwarahisishia wananchi kupata huduma hizo kwa urahisi. Pia kubadilisha yale mabomba ya zamani yaliyochakaa ambayo baadhi yao yamekua yakivujisha maji, na mengine hata spea zao zimekua taabu kupatikana kwenye soko kwa hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu haijaridhika hata kidogo kutokana na kiwango kidogo cha makusanyo ya ada ya maji ambapo kama alivyoelezea Mhe. Waziri kuwa kati ya malengo waliyojiwekea kukusanya Tshs. 5.1 Bil hadi March wameweza kukusanya 1,9 Bil kiasi cha asilimia 37% tu, kiasi hiki ni kidogo sana kwa hiyo tunaitaka Mamlaka kuhakikisha kwa mwaka ujao wanaweza kukusanya pesa zote walizokadiria na kama nilivyoelezea hapo mwanzo Kamati yangu inaahidi kutoa msaada wa mawazo na fikra mpya ili kuhakikisha kwa mwaka ujao lengo hili linafanikiiwa kwa 100%.

SHIRIKA LA UMEME
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inalipongeza sana Shirika la Umeme Zanzibar kwa kuweza kuwapatia huduma ya umeme wananchi wote wa Zanzibar mijini na vijini, kama ilivyo huduma ya maji Serikali yetu kupitia Shirika la Umeme imeweza kuwasambazia huduma hii wazanzibari karibu asilimia 80 ni mfano wa kuigwa katika nchi za Afrika ya Mashariki na kati pamoja na Nchi nyingine za Dunia ya tatu, kutokana na huduma hii hasa vijijini wananchi wengi wamekua wakijiongezea mapato kupitia biashara mbali mbali ikiwemo sekta ya uvuvi. Pia Kamati yangu inalipongeza Shirika la Umeme kwa kuweza kuwapatia wananchi huduma wa uungaji wa Umeme kwa njia ya mkopo kwani hali za wananchi wetu kiuchumi ni duni lakini kupitia huduma hii imeweza kuwaungia kwa malipo kupitia bili zao, hii pia imeweza sana kuwapunguzia umaskini.
Vilevile,Kamati inaishauri Wizara kukaa pamoja na Shirika la Umeme, ili kuweza kutafuta mbinu mbadala ya kulitatua tatizo la foleni katika vituo vinavyotoa huduma za uuzaji umeme hususan kwa Wilaya ya Mjini (Unguja).Aidha,Kamati inaishauri Wizara kupitia Shirika la Umeme, Zanzibar kuongeza vituo vya uuzaji umeme huo katika maeneo mbali mbali ya mjini ili wananchi waweze kuondokana na usumbufu unaojitokeza katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na hali hiyo, Kamati yangu haikusita kuishauri Shirika la Umeme, Zanzibar kuanzisha kituo kimoja cha kuuzia umeme kisiwani Pemba katika mji wa ChakeChake. Ili kuweza kuwasaidia wananchi kupata huduma hii kwa wakati na wepesi zaidi.

Mheshimiwa Spika,
Kamati pia inasikitishwa na taarifa za ucheleweshwaji wa mapato kutoka katika taasisi za Serikali ya Zanzibar na baadhi ya Jamhuri ya Muungano ambayo yangeliweza kulisaidia  Shirika la Umeme katika kutimiza majukumu yake suala ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha kazi za ZECCO ikiwemo kutoa huduma kwa wateja wapya na kulipia madeni makubwa yanayoikabili kutoka Tanesco. Kwakuwa Kamati yangu inaamini taasisi zote zinaingiziwa fedha katika vifungu vyao ambazo wanatakiwa kulipa bili ya Umeme. Kamati yangu kwa bajeti inayokuja haitokubali kuipitisha Bajeti ya Wizara yoyote ambayo inadaiwa na Shirika la Umeme kwani wanalipa mzigo mkubwa wa madeni Shirika ambalo bado linatoa huduma ya Umeme kwa hasara kutokana na bei wanayouziwa na Tanesco, kwa hiyo Kamati inatoa angalizo hili kwa Mawaziri kwani shughuli zao bila ya Umeme basi hawawezi kutoa huduma katika taasisi zao, ili kuweza kuondoa kadhia hiyo bado Kamati yangu inaitaka Shirika la Umeme kuwawekea Mitre za Tukuza Wizara zote ili kuliwezesha Shirika kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuondokana na mzigo wa madeni wa kila siku kutoka Tanesco, na kwakua katika Bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Waziri wa Fedha wa SMT alieleza kua suala la madeni ya Bili ya umeme kwa taasisi za SMT hivi Serikali kupitia Wizara ya Fedha ya SMT zitalipwa moja kwa moja kutoka kwenye mafungu ya Wizara Kamati yangu imefarijika na mpango huo ,kwa hiyo tunamuomba Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme kumuandikia Katibu Mkuu Wizara ya Fedha SMT na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi SMT kuhusu deni lao pamoja bili mpya ili kuwajuulisha kua malipo mengine yalipwe moja kwa moja kwa Shirika la Umeme Zanzibar,kwa hiyo hili naomba Waziri alifanyie kazi kupitia ZECO. Kamati yangu hadi tunaandika ripoti hii Shirika linazidai taasisi hizo za Serikali karibu Tshs.30,046,626,237.98 kwa kweli hili deni kubwa sana nawaomba waheshimiwa tulisaidie Shirika letu kuweza kupwa pesa zao ili liweze kutuhudumia ipasavyo.

Mheshimiwa  Spika,
Kwa upande wa Pemba Kamati yangu inaishauri Serikali kuwavutia wawekezaji katika kisiwa cha Pemba ili kuweza kusaidia kununua huduma ya Umeme kwani Shirika linapata hasara kubwa kwa kulipa gharama kubwa kwa Tanesco kwa Umeme katika kisiwa cha Pemba kulingana na mapato yanayopatikana katika kisiwa cha Pemba.
Pamoja na hayo Kamati yangu inalitaka Shirika kujiandaa na upatikanaji wa Gesi asilia hapa Zanzibar ili kuweza kuzalisha Umeme kwa bei ndogo kupitia umeme wa Gesi kama ilivyo kwa upande wa wenzetu kule Tanzania Bara, kwani bado wananchi wetu wanapata huduma ya umeme kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na yote,  Kamati yangu inalipongeza Shirika kwa utoaji wao wa huduma kwa haraka hasa pale inapotokea hitlafu kwenye maeneo tofauti bila ya kujali wakati ikiwa usiku au mchana. Kamati yangu pia inalipongeza Shirika kwa kuhakikisha wateja wote hivi sasa wanapatiwa huduma ya Umeme wa Tukuza jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato kwa Shirika.

IDARA YA NISHATI NA MADINI
Mheshimiwa Spika,
Naipongeza Idara hii yahuduma zaNishati kwa kazi nzuri inazozifanya na tafitinyingi wanazozifanya hasa kwa upatikanaji wa Umeme mbadalaikiwemo upepo na Solar kwa kushirikiana na Mashirika mbali mbali ya Kimataifa, pamoja na pongezi hizo lakini tunaitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji na Mafuta (ZURA) katika kudhibiti mwenendo wa biashara ya uagizaji na uingizaji wa mafuta wawe makini sana kwani hivi sasa kuna malalamiko mengi kwa baadhi ya watumiaji wa mafuta kwenye vipando ikiwemo magari wakati mwingine huuziwa mafuta machafu ambapo hupelekea kuwatia hasara kubwa kwa uharibifu katika mashine zao za magari kutokana na mfuta machafu yasiyokua na viwango. Kutokana na hali hiyo, Kamati yangu inaitaka Wizara kuhakikisha inatafuta Kampuni ya kuyapima na kuyakagua viwango vya mafuta kama wanavyofanya wenzetu T’bara kwa upande wa Mamlaka ya Kudhibiti Mafuta ( EWURA).

 Mheshimiwa  Spika,
Katika suala hili tunamtaka Mhe.Waziri akija kufanya majumuisho atuelezee wananpango gani wa kuwa na taasisi kama hiyo hapa Zanzibar ili kupunguza hasara kwa wenye vyombo vya moto kwani hata wakipata matatizo hakuna fidia yoyote wanayolipwa aidha na Mamlaka au wamiliki wa vituo vya mafuta.

PROGRAMU YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Mheshimiwa Spika,
Lengo kuu la Programu hii ni kuhakikisha usimamizi thabiti wa masuala yote yanayohusiana na mazingira na kudhibiti athari za kimazingira na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, hapo awali utekelezaji wa Programu hii ulikuwa ukitekelezwa na Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais na baada ya mabadiliko ya Wizara utekelezaji wa Programu hii utasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.



Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Programu hii iliombewa kuidhinishiwa kutumia jumla Tshs. 624,076,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Usimamizi wa Mazingira  na Mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, kati ya fedha hizo zilizoidhinishwa ilikuwa Tshs. 174,076,000 kutoka Serikalini na Tshs. 450,000,000 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Umuhimu wa kudhibiti matumizi mabaya ya kimazingira yanayoendelea katika baadhi ya sehemu kwa upande wa Unguja na Pemba. Kamati inaiomba Wizara kupitia Mradi wa Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi utakaosimamiwa na wafadhili wa UNDP, DFID na AFDB pamoja na Serikali yetu, kuweza  kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari mbali mbali  juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kuzisaidia jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.Aidha, Kamati pia inaishauri  Kamati zote za masheha kuunda Kamati za mazingira katika Shehia zao ili kuweza kusaidia na kulinda maeneo yetu yasiharibiwe na yalindwe kwa mujibu wa Sheria za Mazingira.

Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu imegundua hivi sasa kuna maeneo mengi hapa Zanzibar hasa yaliyoko kwenye fukwe mbali mbali hivi sasa yamekua yakivamiwa na maji ya Bahari na hata kwenye maeneo ambayo yalikua wanachi wakiyatumia kwa ajili ya Kilimo hivi yamejaa maji chumvi ya Bahari hasa kwa upande wa kisiwa cha Pemba, watu wengi wameingia kwenye umasikini baada ya maeneo yao ya kilimo kuingia maji ya chumvi, kwa upande wa ukanda wa Maisara kwa Unguja hata yale maeneo ambayo tumekua tukiyatumia kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye fukwe hivi yameanza kujaa maji na inakua shida kuyatumia wakati wa maji kujaa wakati hapo mwanzo tukiyatumia muda wote.


Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu inaomba ufafanuzi kuhusu Zanzibar inavyofaidika na misaada ya kimataifa kupitia programu za Kimataifa za kusaidia hifadhi ya mazingira Duniani kama ipo basi tungelipenda kuona ni miradi gani tunayosaidiwa, kwani tunasikia katika mikutano mbali mbali ya Kimataifa kuwa mataifa ya Dunia ya tatu yamekua yakidai fidia ya uharibifu wa Mazingira unaofanywa na Mataifa makubwa Duniani kupitia moshi wa viwanda vyao ambo unaathiri sana uharibifu wa “OZONE LAYER”ambapo inasababisha joto kali lakini pia husababisha mvua kubwa sana za” Alninyo” na mfano mzuri mvua za hivi karibuni zilizonyesha hapa Zanzibar zimesababisha maafa makubwa sana lakini hatukusikia mfuko wa mazingira kuweza kuwasaidia wananchi walioathirika, kwani kuna maeneo tangu tuzaliwe yalikua hayajai maji lakini hivi sasa miji yote wakati wa mvua basi wananchi tunasubiri kuzama jambo ambalo wazanzibari tumeanza kuingia kwenye taharuki kubwa hadi mvua zipite kwa hiyo suala hili ni lazima tupate maelezo ya kina sababu zinazosababisha mvua siku hizi kuwa kubwa sana na joto kwa nini limekua kali sana. Lakini pamoja na yote hayo Idara hii inafanya kazi nzuri na tunaomba waendelee na jitihada hizo za kutupatia elimu ya mazingira.

MheshimiwaSpika,
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kwa kua Kamati yangu haikuwahi kufanya ziara kwenye Wizara na kuona utendaji wao nitamuomba Waziri akija hapa aje atueleze kuhusu baadhi ya miradi mikubwa inayojitokeza hapa Zanzibar hususan Mradi wa Ujenzi mkubwa unaoendelea hapo Mtoni Unguja mradi ambao unafukia eneo la Bahari kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo ya baharini na michezo mingine ya watoto , kamati yangu inataka kujua tu je ni athari gani inaweza kupatikana kupitia mradi ule? Je mradi ule hautoathiri mkondo wa njia ya Meli kubwa zinazopita kuingia kwenye Bandari ya malindi na ujenzi mpya wa Bandari ya Mpiga Duri?.



Mheshimiwa  Spika,
Kwakua mradi huu ni mpya kwa hapa kwetu basi ni vyema tukapata taarifa sahihi kutoka Serikalini kwani katika nchi ya Dubai walipoanza kufukia Bahari na kujenga kisiwa na baadae kujenga Hoteli kulijitokeza athari nyingi ikiwemo maji ya Bahari kupanda kwenye maeneo mengine lakini kwa kuwa wenzetu wanauwezo mkubwa kiuchumi waliweza kuidhibiti hali hiyo,

PROGRAMU YA USIMAMIZI NA UPANGAJI WA MATUMIZI YA ARDHI

Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa majukumu makuu ya Programu hii ni  kuhakikisha kunakuwepo na usalama katika matumizi ya ardhi kwa maendeleo ya nchi yetu kiujumla. Aidha, Kamati yangu inaiomba Wizara husika kuwa makini katika utekelezaji wa Programu ndogo zilizomo ndani ya Programu hii kuu.

Mheshimiwa Spika,
Kama inavyofahamika kuwa moja kati ya changamoto inayowakumba wananchi wetu ni usalama wa umiliki wa ardhi zao, usajili wa ardhi kiholela (kinyume na taratibu za kisheria) pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi inayoendelea kila muda ukisonga mbele katika Mahakama zetu za ardhi. Na kamati yangu inaamini kadhia hii itamalizika tu pale ule mpango wa Wizara wa kusajili ardhi yote na kuwamilikisha wahusika basi kadhia hii itaisha kwani kuna maeneo mengi hasa kwetu vijini kuna mashamba ambayo tumerithishwa na wazee wetu kutokana na uzoefu tu lakini hata wao baadhi yao hawana hata hizo hati miliki lakini wameshajenga, wanalima na vijukuu vyao pia wanaendelea na maisha hapo, kwa hiyo mpango huo utasaidia kuondoa tatizo hilo.


Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imegundua kutokana na matatizo mengi yaliyojitokeza hasa kunyanganywa baadhi ya wawekezaji maeneo yao na mengine kufutwa kinyume na taratibu na mengine pia kuundiwa Kamati Teule na Baraza hili lakini hadi leo hutukuletewa taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza hadi leo hatujui kilichoendelea kwa hiyo ni vyema basi Wizara ikaandaa taarifa maalum ya utekelezaji wa maagizo yale ili kujiridhisha kua ile kazi kubwa iliyofanywa na Baraza na kutumia pesa nyingi imeleta matunda gani kwa jamii, lakini pamoja na hayo tunamuomba Waziri kuweza kuwarejeshea maeneo yao wale wawekezaji ambao tayari wanataka kuekeza kwenye Miradi Mikubwa ambayo itaongeza ajira kwa watu wetu lakini pia kuongeza wigo wa mapato yetu hasa ukizingatia kua Bajeti hii inalenga kutegemea mapato ya ndani zaidi kuliko kutegemea misaada kutoka nje ambapo kwa miaka ya hivi karibu imekua na masharti magumu kila kukicha.

Mheshimiwa Spika,
Kamati pia inaomba Kamisheni ya Ardhi kuandaa utaratibu maalum wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi mabaya ya Ardhi na athari kwa pamoja, ili kuweza kuondokana na kadhia hii ya migogoro ya ardhi zinazouzwa na kusajiliwa kinyume na taratibu zilizowekwa kisheria. Kutokufanya hivyo, ni kuiongezea mzigo Serikali na kuikosesha mapato yatokanayo na wawekezaji.

Mheshimiwa  Spika,
Katika eneo hili tunakuomba Mhe. Waziri uwe mkali hasa kwa baadhi ya waekezaji ambao wameyachukua maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji pamoja ya kuwa Ardhi ni mali ya Serikali lakini mwananchi anapokubali kupisha muekezaji basi alipwe fidia kwa mujibu wa makubaliano na sio kutumia nguvu na ubabe katika kuwadhulumu wanyonge haki zao. Aidha, katika jambo hili Kamati yangu haitokuwa tayari kuwaona wananchi wetu wakipokonywa haki zao za matumizi ya Ardhi zao na matajiri kwa kutumia uwezo wa kifedha waliokuwa nao, kwani na wao ni raia wa Nchi hii na ni wajibu wao kufaidi matunda ya Mapinduzi Matukufu ikiwemo kumiliki Ardhi zao. Na katika suala hili Kamati yangu inaahidi kuwasaidia wananchi wake kwa kila njia.

MAHKAMA YA ARDHI
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaipongeza Wizara kupitia Mahkama ya Ardhi kwa kazi nzuri ambayo hivi sasa wanaifanya kwani kwa mwaka uliopita kati ya kesi 168 zilizoripotiwa karibu kesi 138 zimeshatolewa maamuzi ambapo kwa Unguja kati ya kesi 118 zilizoripotiwa tayari 98 zimeshapatiwa hukumu na kwa Pemba kati ya kesi 50 tayari kesi 40 zimeshapatiwa hukumu ,hapa kwa heshima kubwa Kamati yangu inaipongeza Mahkama ya Ardhi kwa kufanya kazi zao vizuri na kile kilio chetu Waheshimiwa Wajumbe wako wa Baraza hili tukufu kuwa kesi za Ardhi zinachukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi na kuiomba Serikali kuunda Mahkama maalum ya Ardhi ili kushughulikia kesi hizo sasa dawa imepatikana kutokana kasi kubwa ya uendeshwaji wa kesi hizo, lakini tunawaomba pia Mahakimu wa Mahkama ya Ardhi waendelee kufanya vizuri na kuwa waadilifu kama walivyoanza hivi sasa isijekua ile kesi ya Mgema ukamsifu “TEMBO “ kulitia maji. Aidha, pamoja na pongezi hizo tunawaomba Mahakimu wa Mahkama za Ardhi kujitahidi kuwa waadilifu katika kuendesha na kutoa hukumu hizo kwani mara nyingi kesi hizo hutawaliwa sana sana na vishawishi vya matajiri kutaka kuweadhulumu haki zao wanyonge kupitia Mahkama hizo kwani wanyonge hawatokuwa na uwezo wa kuhonga ili kujiokoa na kunyang’anywa ardhi zao na mapapa ambayo yako vinywa wazi kwa gharama zozote ilimradi waweze kuwanyang’anya haki za watu kwa kuwatumia Majaji wa Mahkama hizo. Kwa hiyo, Mahakimu wajue kuwa wamebeba dhima kubwa kwa Mwenyeenzi Mungu kwani ardhi sio jambo la mchezo hata kidogo ,kwani ukisikia Mataifa makubwa Duniani wanapigana vita basi sababu kubwa ni kutaka kunyang’anya Ardhi za Nchi nyingine.



PROGRAMU NDOGO YA UPANGAJI WA MIJI NA MATUMIZI YA ARDHI.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu pia  inaipongeza Idara hii ya Mipango Miji na Vijiji kwa kuandaa upangaji upya wa Miji na Viji pamoja na matumizi bora ya Ardhi, ili kuwawezesha wananchi wetu kuweza kufaidika na matumizi bora ya ardhi kiuchumi na kijamii kwa maeneo yote ya Zanzibar. Pamoja na pongezi hizo Mhe. Waziri ameeleza kwenye kitabu chake kuwa Idara ya mipango miji tayari imeshapanga maeneo matatu ya wazi katika Eneo la Kibandamaiti, Eneo la Daraja Bovu na Eneo la Kiembe Samaki kupitia mfuko wa (Urbarn Development Fund) tunamuomba akija kufanya majumuisho atuelezee kuwa ni uboreshaji gani ambao unaokusudiwa kufanywa katika maeneo hayo niliyoyataja kwani wananchi wengi hawaijui mipango hiyo ili na wao kujitayarisha kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Pia, Mhe. Waziri katika kitabu chake ametuelezea kwamba katika mradi mpya wa mpango mkuu wa matumizi ya Ardhi, (Zanzibar Town Master Plan)kuwa kwa hivi sasa kitovu kikuu cha Mji Mkuu wa Zanzibar kinahama kutoka Mji Mkongwe na kuhamia maeneo ya ng’ambo bila shaka shughuli nyingi za za kijamii, maofisi kiuchumi na kibiashara na sehemu za mapumziko zitaongezwa na kuimarishwa katika maeneo ya ng’ambo ambapo kaulimbiu yake ni “Ng’ambo Tuitakayo”mpango huu kwa kweli ukifanikiwa utaiongezea haiba mji wetu wa Zanzibar kwani hivi sasa mji upo kienyeji sana na hata majengo yake hayailetei haiba nzuri mji wetu. Hivyo, tunaiomba Idara kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujua mipango yenu ili na wao waweze kutoa maoni yao na pia kutoa ushirikiano wakati wa utekalezaji wa mpango huo. PIa, Kamati yangu inaishauri Idara kuweza kuchora ramani ya mji wetu utakavyokuwa na kuweka mabango (BILL BOARD) makubwa sehemu zenye mikusanyiko mikubwa kwenye maeneo hayo ili wananchi kuona nikitu gani kilicholengwa kufanywa katika maeneo hayo.

PROGRAMU NDOGO NA USIMAMIZI WA SHUGHULI ZA UJENZI NA NYUMBA

Mheshimiwa  Spika,
Programu hii kama alivyoelezea Mhe. Waziri kuwa inatekelezwa na Idara ya Ujenzi na Shirika la Nyumba,Kamati yangu inaipongeza Idara kwa kazi walizozifanya katika kipindi hiki ikiwemo usafishaji wa makaro na uzibuaji wa mabomba ya maji machafu katika nyumba zetu za maendeleopamoja na uandaaji wa michoro mbali mbali ya ujenzi usajiliwa wakandarazi mbali mbalikazi hizi zote zinahitaji utaalamu mkubwakwa hiyo iko hajaya kuwalinda na kuwapa maslahi bora watumishi wake ili waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi.

PROGRAMU NDOGO YA UHIFADHI NA UENDELEZAJI WA MAMLAKA YA MJI MKONGWE
Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu pia inaipongeza Mamlaka ya Uhifadhi Mji Mkongwe kwa kuendelea kuulea na kuuweka Mji Mkongwe kuendelea kuwa na hadhi yake kuwa ni mji kati ya Miji Mikongwe Duniani ambayo ni urithi wa kimataifa, sisi wazanzibari tunapaswa tuulinde na tuuhifadhi kwa pamoja mji huu kwani ni sehemu ya kivutio kikubwa Duniani ambapo unaitangaza Zanzibar na kuweza kuwavutia watalii wengi pamoja na wanafunzi wakiwemo watafiti mbali mbali ambao hufika Zanzibar ili kuja kufanya shughuli zao za kitalii na kimasomo. Kwa maana hiyo, tunawaomba sana wale wote wanaoishi na kufanya shughuli zao za kimaisha za kila siku kuhakikisha kuwa wanatunza mazingira lakini pia kuhakikisha urithi huu haupotezi hadhi yake, kwa hiyo tunamuomba sana Mkurugenzi aendelee kusimamia na kuulinda mji wetu ili usije kupoteza hadhi yake kimataifa.



Mheshimiwa Spika,
Kamati inaipongeza tena Idara kwa kutafuta mradi wa ujenzi wa ukuta wa uzio wa Bahari hapo Mizingani ambapo Kamati yangu inatarajia kuwa baada ya kumaliza ujenzi huo basi utaweza kubadilisha haiba ya Mji wetu ili kuongeza kuvutiaMji wetu na pia kuongeza shughuli za kibiashara na kiuchumi ambapo tunategemea pia kutaongeza shughuli za ajira katka eneo hilo.

Mheshimiwa  Spika,
Kamati yangu inapongeza pia jitihada za Mamlaka ya Uhifadhi Mji Mkongwe, kwa kufanikisha upatikanaji wa ufadhili wa ukarabati mkubwa wa jengo la Beit-el-Ajabkupitia Serikali ya Oman. Aidha, Kamati yangu inamuomba Mkurugenzi asichoke ili kufuatilia ukarabati huo unaanza kwa muda uliopangwa kwani tangu nyumba hiyo ilipoporomoka jengo hilo limeikosesha Serikali mapato mengi ambayo yalikua hupatikana kupitia ada ya jengo hilo. Pamoja na hayo, Kamati yangu inaitaka Serikali baada ya kukamilika ukarabati huo basi kuwe na mfuko maalum ambao utakusanya mapato ya jengo hilo ili ziweze kusaidia kurekebisha pale patakapo leta khitlaf yoyote kwani makosa tuliyoyafanya kwa mapato yanayokusanywa huingia katika mfuko mwengine ambapo zikihitajika inachukua muda mwingi kupatikana kwa ajili ya kazi ilikusudiwa kufanyika.

UKARABATI WA JENGO LA CHAWA DARAJANI

Mheshimiwa Spika,
Kamati yanguinaipongeza Mamlaka kwausimamizi mzuriwa karibu waukarabati wa jengo hilo kupitia mfuko wa Hifadhi ya jamii ZSSFkutokana na umuhimuwa shughuli za uchumikwa wananchiwetu katika jumba hilo. Aidha, tunaziomba taasisizinazohusika na ujenzi huo kuhakikisha ukarabati huo unaenda kwa haraka ili wale wananchi waliokuwa wakifanya shughuli zao hapo waweze kurejea tena ili waweze kuendelea na shughuli zao za biashara kila siku, kwani katika kipindi cha ukarabati huo kutaleta usumbufu mkubwa kwa wao na familia zao lakini kama tunavyojua shughuli  maendeleo pia huleta changamoto lakini inabidi tuwe wastahamilivu, pamoja na hayo tunaiomba tene Idara husika kuhakikisha wale  wadau ambao walikuwepo mwanzo wenye maduka na wapangaji waliokuwepo mwanzo warejeshwe ili kuendelea na biashara zao na shughuli nyengine za kijamii kama hapo mwanzo.
Vile vile, Kamati yangu inapongeza Mamlaka kwa kuanzisha utaratibu wa kuratibu na kuyasimamia maeneo ya wazi na kuyasajili kwani katika miaka ya hivi karibuni kumekua na utaratibu wa uvamizi wa maeneo ya wazi aidha kwa kujengwa au kufanya shughuli neingine za kijamii na kibiashara na inapofika mtu kuondolewa basi anakua mkali hataki kuondoka na jambo hili mwisho hupelekea kuharibu ile haiba ya Mji mkongwe. Kamati yangu inaendelea kuiomba Mamlaka kuhakikisha hizo sehemu za wazi zilizobakia zinaendelea kuhifadhiwa ili kuwapa wananchi wengi kuweza kuzitumia. Pamoja na yote  Mamlaka hii inafanya kazi zake vizuri na tunampongeza sana Mkurugeni kwa Usimamizi wake imara.

Mheshimiwa Spika,
Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi imejadili na kuyakubali  mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2016/2017, na inawaomba Waheshimiwa Wajumbe wako wote waijadili, watoe  mapendekezo yao na hatimae kuipitisha Bajeti hii.

Mheshimiwa Spika,
Mwisho napenda kuwashukuru na kuwapongeza tena viongozi na watendaji wa Wizara hii kwa juhudi wanazochukua katika kutekeleza kazi zao pamoja na ushirikiano wao kwa Kamati hii. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa kunisikiliza kwa makini na utulivu wa hali ya juu wakati wote nilipokuwa nikiwasilisha hotuba hii.



Mheshimiwa Spika,
Naomba kuunga mkono hoja na naombakuwasilisha.






Ahsante,


……………………..,
Hamza Hassan Juma,
Mwenyekiti
Kamatiya Mawasiliano naUjenzi,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.