Habari za Punde

Balozi Seif: Wananchi, taasisi za kijamii zina wajibu kusaidia wazee wasiojiweza, watoto mayatima


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi msaada wa Vyakula va vifaa kwa ajili ya Wazee wasiojiweza na Watoto Yatima vilivyotolewa na Serikali ya Ras Al – Khaimah hafla iliyofanyika Nyumbani Kwake Mtaa wa Kama nje kidogo ya Kaskanizi Magharibi ya Mji wa Zanzibar.

Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga. Kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar Bibi Wahida Maabad Mohammed pamoja na Mkuu wa Fatwa na Utafiti Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar  Sheikha Nooman Jongo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu aliyevaa kofia ya Buluu akimkaguza Balozi Seif  kwenye Moja ya Matangi ya  kuhifadhia  Maji Chumbuni yaliyogharamiwa na Serikali ya Ras Al – Khaimah na kuzinduliwa rasmi Mwezi Septemba Mwaka 2015.

Nyuma Kushoto ya Balozi Seif ni Mshauri wa Mfalme wa Mamlaka ya Rais Al –Khaimah ambae pia ni Mwakilishi wa Kampuni ya Rak Gas ya Ras Al-Khaimah  Bwana Kamal Ataya.
Picha na – OMPR – ZNZ.Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Wananchi waliojaliwa kipato, mashirika  pamoja na Taasisi za kijamii bado zina wajibu wa kusaidia Wazee wasiojiweza na watoto Yatima ili kuwapa matumaini ya kuendelea kuishi kwa amani na upendo ndani ya Jamii.

Alisema utaratibu huo endapo utaendelea kutekelezwa kwa nia safi unaweza kusaidia kwa kina  kuondoa fikra potovu zinazoweza kujengwa na  Wazee na Watoto hao katika kudhania kwamba wanatengwa ndani ya jamii.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati wa kukabidhi vyakula mbali mbali na vifaa vilivyotolewa msaada na Serikali ya Ras Al – Khaimah chini ya Mtawala wa Nchi hiyoEmir Saud Bin Saqr Qasimi hafla iliyofanyika Nyumbani Kwake Mtaa wa Kama nje kidogo ya Kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar.

Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na Mchele, unga wa Ngano, Tende, Sukari, Mafuta, Mafriji, Baskeli kwa ajili ya watu wenye ulemavu { Wheel Chairs } pamoja na Mas-hafu vimekabidhiwa kwa Uongozi wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na Uongozi  wa Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar.


Balozi Seif alisema Serikali ya Mamlaka ya Ras Al –Khaimah imekuwa na utamaduni wa kusaidia Jamii ya Wazanzibar wenye mazingira magumu na wale walioondokewa na Wazazi wao kwa muda sasa utaratibu unaopaswa kuungwa mkono na wale wenye uwezo wa kufanya hivyo.

Akipokea msaada wa vyakula na Vifaa hivyo Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kwa niaba ya Taasisi hizo mbili aliwashukuru Viongozi na Taasisi za ndani na nje ya Nchi zinazoendelea kuwajali Wananchi hasa makundi yanayostahiki kuangaliwa kwa kupatiwa huduma muhimu za zile za lazima.

Sheikh Soraga alisema katika kutilia mkazo uzito huo wa kutolewa misaada kama hiyo alikariri   Moja ya Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Nabii Muhammad {SWA } inayosisitiza kwamba asiyewajali Watoto na Wazee wasiojiweza hayumo katika Uislamu.

Alisema suala la kuyashughulikia makundi maalum kama wazee na watoto wadogo ndani ya Jamii ya wanaadamu na hasa waumini wa 
Dini ya Kiislamu ni wajibu usiyoepukika kwa kila Muunini.

Katibu huyo wa Mufti Mkuu wa Zanzibar alifafanua wazi kwamba msaada huo uliotolewa na kuelekezwa kwa wazee na watoto Yatima si mdogo na inapaswa kushukuriwa kwa ihsani zote.

Serikali ya Mamlaka ya Ras Al – Khaimah imekuwa mdau  mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wake katika kushirikiana kwenye kuimarisha miradi ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Miongoni mwa ushirikiano huo ni pamoja na uendelezaji wa Mradi wa uchimbaji Visima 100 vinavyokadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani Kati ya Milioni Tano na Sita lengo likiwa ni kuimarisha huduma za maji safi na salama Unguja na Pemba katika Maeneo yote Mijini na Vijijini.


Visima 50 vilivyochimbwa kwenye mradi huo katika awamu ya kwanza kila kimoja kina uwezo wa kutoa maji Lita 17,000 kwa saa moja wakati Matangi Sita yaliyojengwa ndani ya mradi huo yana uwezo wa kutunza Maji Lita Laki 200,000 kwa kila Tangi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.