Habari za Punde

Mjue Masoud Ali Mohammed: Afisa Mdhamini Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora Pemba

 Na Haji Nassor, Pemba
VIJANA wa taifa la Tanzania sasa wameshafikia zaidi ya 16 milioni (sensa 2012).



Ndani yake wamo wasomi waliobobea, kwenye fani tofauti ambazo naanimi wakiungana pamoja, taifa hili linaweza kupiga hatua kubwa tena ya kisayansi.

Wangapi wamekuwa wakitorokea nchi za mashariki ya mbali, eti kusaka maisha bora, na haya yamekuja baada ya waasisi wa taifa hili rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na mwenzake wa Zanzibar sheikh Abeid Amani Karume kutukomboa.

Wastani wa vijana 50,000 kila mwaka wanaripotiwa kumaliza elimu yao ya juu hapa Tanzania, iwe ni daktari, mawasiliano ya umma na habari, uhandisi, ualimu, kilimo na hata kwenye sayansi ya siasa na utawala.

Taifa hili lazima iwe ni majabu, kwamba eti itokezee skuli iwe na uhaba wa waalimu na kwa mfano serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ifike pahala hata iwaajiri waalimu kutoka nje ya Tanzania.

Inawezekana huku ni kukosa uzalendo, kutopenda taifa, ndugu, jamaa na marafiki kwa hawa vijana wanaomaliza fani kama ya ualimu na kukimbilia nchi jirani kama za Kenya, Uganda, Rwanda na au nje ya Afrika.

Hawajiulizi kwamba kama waasisi wa taifa hili wengekimbilia nje ya nchi, leo na kesho tungekuwa bado wanyonge wa kielimu, uchumi na hata ubora wa siasa uliopo sasa usingejitokeza.
Nia thabiti ya vijana wetu hasa wenye utaalamu na walioupatia ndani ya taifa letu, na kisha kuwanufaisha wengine inauma sana, uko wapi uzalendo, mapenzi ya utaifa, na malengo ya kufikia tutakapo.

Kwenye takwimu ya vijana zaidi ya 16 milioni wa Tanzania, kijana Masoud Ali Mohamed nae ameongeza idadi hiyo kwenye sensa ya watu na makaazi ilioendeshwa nchi zima mwaka 2012.


KIELIMU MASOUD

Kijana huyo aliezaliwa mwishoni mwa miaka ya sabini (1978) katika kijiji cha Ole wilaya ya wete Pemba, na kuanza kunolewa kwa elimu yake ya msingi katika Skuli ya Ole hadi darasa la tatu kijijini hapo kuanzia mwaka 1987-1990, na kisha kuhamia kisiwa cha Unguja.

Masoud akiwa kwenye heka heka za kujitafutia elimu zaidi miaka kuanzia ya 1990-1998 alizikalia kitako skuli za Kajificheni kisha Hamamni kwa elimu ya msingi na sekondari, kabla ya kujinga na elimu juu ya kidato cha tano na sita skuli ya Lumumba mwaka 1999/2001.

Masoud akiwa kwenye ngarambe za kada ya kielimu, alikuwa tofauti na vijana wengi wa sasa, ambapo yeye alikuwa akifuatilia sana hotuba za wasisi wa taifa hili, hadi kufika wakati wenzake wakidhani anaweza kufeli masomo yake.

“Mimi na hotuba za Nyerere au Karume, ni sawa na mwalimu Nyerere na Azimio la Arusha, huwa naamini ndani ya moyo wangu kuwa  maneno ya wazee hawa yana falsafa iliyotukuka na chakula cha ubongo wenye kuhitaji maono ya hali ya juu.’’,alidokeza akizungumza nami.

Mwaka  2001 aliajiriwa na wizara ya elimu, akiwa mwalimu katika skuli ya sekondari ya Benbela na kubadilishwa jina na hata wazazi wake, kwa  kumuita mwalimu Masoud, mwaka mmoja baadae yaani 2002, kijana huyo alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ‘Mlimani’ kuchukuwa Shahada ya kwanza kwenye fani ya sayansi ya siasa na utawala (BA PSPA).

“Niliamua kuchukua fani ya ‘Political science’ kwani niliamini ni miongoni mwa fani zenye mchango mkubwa chanya hasa katika siasa hizi za Nchi changa na kuweza kutoa mchango mkubwa kwa Taifa langu’’,alifafanua.


Akiwa chuoni hapo Massoud kutokana na utundu wake wa kimasomo, aliwahi kukabidhiwa vyeti mbali mbali kutokana na ushiriki adhimu na wenye mchango mkubwa katika jumuia kadhaa zilizokuwepo chuoni hapo, aliwahi kutunukiwa vyeti katika masuala ya haki za binadamu, “Red Cross”na Jumuia ya wanafunzi wa sayansi ya siasa na utawala.
Aliwahi kushiriki mijadala na makongamano mbali mbali yaliokuwa yakiandaliwa chuoni hapo, na hata tasisi nyengine, ambapo alikiri kwamba ndio yaliomutesha mbawa hadi leo hii kufikia kujiamiani.
Baada ya kumaliza miaka mitatu chuo kikuu cha Dar es Salaam alitunukiwa Shahada ya heshima BA (Honours) katika fani ya Sayansi ya Siasa na Utawala/Uongozi wa Umma (BA (Honours) in Political Science and Public Administration.
Omar Hassan Ali ambae alisoma na Masoud kwenye elimu ya sekondari, alisema alikuwa mtulivu na hakuwa na marafiki watundu na hadi kumpachika jina la ‘sheikh Masoud’ wakati huo ila alikua na kipaji cha ajabu katika masomo ya Historia, Civics na Kiswahili.
“Kwa kweli Masoud nilikuwa namfahamu sana, na wapo waliosema pamoja na kutokua mchangamfu anaweza kufika mbali, maana alikuwa anafuatilia masomo yake kwa karibu”,alifafanua
Mwalimu aliewahi kufundisha na Masoud Ali Mohamed katika Skuli ya Benbela, mwalimu Ali Haji Ali alisema miongoni mwa waalimu wanzake waliokuwa makini na kazi hiyo ya ualimu, ingawa kwa muda mfupi mmoja wao ni mwalimu Masoud (sheikh Masoud).
“Mimi nilikuwa karibu sana na waalimu wote, lakini mwalimu Masoud, nilikuwa karibu nae zaidi, maana nilikuwa napata kitu kipya chenye maana kitaaluma na maisha kila siku kutoka kwake”,alifafanua.
Hassan Ramadhan rafiki wa Masoud anaeishi Vuga mjini Unguja, alisema kijana huyo pamoja na umri wake kumruhusu kufanya mambo ambayo yalikuwa yakitendwa na rika lao, yeye alikuwa zaidi kwenye masomo yake.
Katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Kusini Ramadhani Mcheju anamueleza Masoud kama kijana aliyeshiba uzalendo kwa Taifa lake na mwenye maadili ya hali ya juu sana na mapenzi makubwa kwa Chama cha Mapinduzi.
“Unapoona kijana aina ya Masoud mwenye elimu yake, maisha yake na akaamua kujitoa muhanga kukipigania Chama cha Mapinduzi hasa maeneo ya Pemba, lazima ujuwe huyu ni kijana mwenye upeo na uzalendo wa kipekee na kinachomuongoza Masoud ni imani ya kuwa CCM ndio mkombozi wa mnyonge na chama chenye historia iliyotukuka kwa Taifa hili”, anaeleza Katibu Ramadhani Mcheju.
Masoud baada ya kumaliza chuo kikuu cha Dar-es Salaam mwaka 2005, mwaka mmoja baadae alifanikiwa kujinga na chuo kimoja kilichopo Mkoani Mbeya Tanzania muda wa miezi tisa kwa ajili ya kupata mafunzo ya ziada mwaka 2007 alimaliza.   
KISIASA MASOUD
Masoud ambae hakuficha kwamba ni mwanchama hai na madhubuti wa CCM alisema anazo sababu zaidi ya kumi nzito za kuwa mwanachama wa chama hicho, moja akitaja kwamba kina dira madhubuti isiyoyumba na ndio chama pekee chenye sura ya kitaifa, kimuundo na kiitikadi.
“Nangalia Afrika ni chama gani kinafanana na CCM cha Tanzania, lakini huwa nashindwa kufafanisha kutokana na CCM kwanza kuwa na histori isiofutika na hasa wakati wa TANU na ASP kuwang’oa madhalimu wa taifa.
Mbona Masoud inaaminika kwamba wasomi wengi wenye fani kama yako, twaelezwa kwamba wanakimbilia vyama vyengine wewe iweje na CCM? nilimuliza na kusema sio sahihi.
“Unajua unapomaliza sayansi ya siasa na uongozi kuelewa historia ya nchi yetu kupitia hotuba mbali mbali za waasisi wetu na ukazifahamu malengo na thamani yake, lazima wewe utaingia CCM au utaipigia kura wakati ukifika, vinginevyo hutakuwa mzalendo wa Taifa lako’’,alisema.
Masoud alifafanua zaidi kwamba waasisi wa taifa hili walifanya kazi kubwa hadi leo ikapatikana idadi kubwa ya vijana ambao ni wasomi, sasa hoja yenye mantiki ya kuwapinga inatoka wapi, alihoji.
Kijana Masoud ambae alikata kadi ya chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1998 tawi la Shangani mjini Unguja, ambapo baadae mwaka 2007 alishajipanga kuingia ndani ya chama kiuongozi, yeye ni muumini mkubwa sana wa muungano na kusema una faida lukuki.
 “Angalia faida ya Muungano wetu wa mwaka 1964, mimi nimezaliwa wilaya ya Wete Pemba mwaka 1978, lakini miaka 30 baadae nikiwa Bukoba Mkoa wa Kagera niligombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM hasa UVCCM mwaka 2008 na nilichaguliwa kwa nafasi zote nikawa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa wa UVCCM Kagera.
Aidha Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya UVCCM, Mjumbe wa Baraza la Wilaya UVCCM Bukoba Mjini, Mjumbe wa Kamati Tekelezaji ya Wilaya ya Bukoba Mjini UVCCM, pia Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa UVCCM Bukoba mjini, hizi zote ni nafasi za siasa ambazo aliwahi kuzihudumu kijana huyu.
Kilichompeleka huko ni kazi yake ambayo hakupenda kuitaja, ingawa baada ya kukaa huko tokea miaka ya 2007 hadi mwaka 2010 alipojitosa katika kinyang’anyiro kizito cha kuwania Ubunge kupitia CCM jimbo la Ole Wilaya ya Wete, Mkoa Kaskazini Pemba na hatimae alishinda kura za maoni na kuteuliwa Halmashauri Kuu ya Taifa kuwa mgombea Ubunge Jimbo hilo ila kura hazikutosha katika uchaguzi mkuu .
Akiwa ndani ya siasa, aliona kila kitu ni rahisi kukitekeleza hasa kwa vile tayari ameshamaliza elimu yake ya masuala ya kisiasa, ingawa ushauri na maelekezo alisema kwake ndio chakula.
“Unajua siasa ukishapata waelekezaji wazuri basi hakuna ambalo utashindwa kulifanya, maana mimi mwenyewe nilikuwa nashauri wadogo zangu, ingawa sisahau pia hotuba za wasisi wetu’’,alisema.
Hasnuu Faki Hassan kutoka Jimbo la Ole, Pemba ambaye pia ni Daktari katika hospitali ya Chake akizungumza kwenye moja ya kongamano ambalo Masoud alitoa mada ya katiba pendekezwa, alisema atawashawishi wanaccm kumpitisha tena kijana huyo kugombea Ubunge Jimbo la Ole.
“Mimi tokea nizaliwe sijakumbana na kijana mwenye upeo na uelewa hasa wa mambo ya kitaifa na uzalendo kama alivyo kijana Massoud, na nitawashawishi wengine ili Masoud kama yuko tayari aje agombee jimboni’’,alieleza.
Masoud alisema hatosahau ndani ya uongozi wake wa UVCCM wakati akiwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa Dodoma alipohudhuria Mkutano mkuu wa saba wa UVCCM na hapo ndipo alijiridhisha zaidi kuwa CCM ni chama cha Ukombozi na chama cha Kitaifa.
KWENYE KATIBA.
Yeye binafsi alisema hakutarajia hata siku moja kwamba ingetokezea wananchi wa Tanzania kushirikishwa juu ya utungwaji wa katiba maana imekuwa ni jambo adimu hasa kwa siasa za kiafrika.
Masoud alisema wakati akiwa chuo kikuu na hata skuli kusoma elimu ya sekondari alikuwa akisikia kwamba katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imekua na mapungufu.
Lakini hata yeye baada ya kuisoma na kuiangalia, aliona hayo ingawa bado ni Katiba bora, Uongozi wa rais Dk Jakaya Mrisho Kikwete na Dk Ali Mohammed Shein ndio walioanzisha mchakato wa kuandikwa kwa katiba hiyo jambo ambalo litawafanya wakumbukwe milele.
Hatua ya kukusanya maoni, hadi kufikia ngazi ya wilaya na hatima bunge maalumu la katiba, na vijana kushiriki, kwa Masoud anasema hiyo ni heshima kubwa.
“Ukitaka kuzihesabu nchi zilizofanya zoezi la kuandika katiba mpya kama ilivyofanya Tanzania ni chache sana, sasa lazima vijana waheshimi hili na kuona kwamba ni fursa adhimu’’,alisema.
Hadi sasa anasema hajafahamu lengo, dhamira na makusudio ya wale wanazunguka nchi zima kuwataka wananchi waipigie kura ya ‘HAPANA’ katiba hiyo.
Kwake yeye anaona kama anapata shaka, kwamba inawezekana makundi hayo ya watu iwe ni wanasiasa, makundi ya dini, asasi za kiraia nia yao hasa sio katiba inawezekana na kuuchukia Mungano.
Wapo wanasiasa walikua na madai ya muda mrefu kwamba Katiba iliopo ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania inaishusha hadhi Zanzibar na kukosa hata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa.
Alidondoa baadhi ya vipengele ambavyo yeye vinamshawishi kuipigia kura ya ‘NDIO’ katiba hiyo, kama kwenye Ibara ya 57, ambayo imetaja haki za wanawake moja kwa moja, huku kwenye katiba ya sasa hilo likikosekana.
Alitaja Ibara nyengine ya 78 (i) juu ya wajibu wa viongozi wakuu kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliasisiwa na viongozi wakuu wa nchi mbili hizi.
“Kwangu mimi anaepinga Muungano, hasa muungano huu tulionao ni sawa na mhaini” ,alisema Masoud.
Suala la tume huru ya uchaguzi, alisema nayo imewekwa kwenye Ibara ya 252, ambalo kubwa na la kujivunia Masoud alisema ni kupewa uwezo kisheria Zanzibar kukopa ndani na nje.
Kubwa aliwaasa hasa vijana wenzake kuhakikisha katiba hiyo inayopendekezwa wakati ukifika wanaipiga kura ya ‘NDIO’kwani watakuwa wamelitendea haki Taifa lao na historia itakuja kuwatukuza kwa vizazi vijavyo.

RUSHWA
Kijana huyo amekuwa akiwachukia kwa kinywa kipana walarushwa na watoaji, na katika hili haangalii chama, bali anavyotaka ni kuhakikisha viongozi wanatekeleza maagizo ya waasisi wa taifa hili kwa vitendo.
“Vitendo vya rushwa vimekuwa wazi wazi hasa nyakati kama hizi za kuelekea uchaguzi mkuu wa vyama vingi, lakini ni vyema wenye mamlaka ya kufanya hivyo wawe makini’’,alisema kwa uchungu.
 Na ndio maana kijana huyo alilishukuru sana bunge maalumu la katiba kwa kuipitisha sura ya nne, Ibara 249 ambacho kimeeleza uanzishwa wa chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa.  
MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Kwenye hili anasema halifai kuingizwa kama jambo la kisasa, maana ndio utanzania wa wananchi hata walioko Zanzibar na wamekuwa wakijivunia pahala popote wendapo.
Haridhishwi hata kidogo na wale wenye kuomba dua kwamba eti siku moja uwe haupo, huku akiamini kwamba inawezekana wanafanya hivyo wakikosa kujua athari na madhara yake hasa kwenye uchumi na usalama wa nchi yetu.
“Hebu tujifunze kwa wenzetu ni nchi gani iliyowahi kuungana baadae zikatengana na zikaendelea kubakia salama, jibu ni kuwa hakuna, angalia pale Sudan Kaskazini na Sudan Kusini, watu wasome historia za nchi nyingi, wasilazimishe kutufarakanisha kwa faida za kisiasa”, alifafanua Masoud.
“Waliowengi wanadhani siasa ni kusimama kwenye jukwaa na watu wakacheka na wengine wakakupigia kofi unapoeleza mambo ambayo taifa linaweza kuanza mwanzo kujulikana ulimwenguni”,alifafanua.
Alitaja faida moja kubwa ya Muungano huo kwamba hakuna mtanzania bara wala mzanzibari anaemkebehi mwenzake, bali kila mmoja anajinasibu kwa utaifa wa Tanzania uliopatikana kwa Mungano.
Aliwaasa wanasiasa na hasa vijana wenzake kuacha kuchezea shilingi chooni ikitumbukia moja kwa moja moja ni sawa na kua na utawala wa kikoloni, maana nchi daima haitotulia tena.
“Muungano huu hasa unaimarika vyema na kunawiri unapokua kwenye serikali mbili kama ilivyo kwenye Ibara ya 1 ya katiba ya sasa ya mwaka 1977 na katiba inayopendekezwa kwenye Ibara kama hiyo’,alisema kwa kunukuu katiba.
UZALENDO
Bado kijana Masoud hajapata taswira ya uhakika kuona vijana waliosomeshwa kwenye wakati mgumu ndani ya taifa hili kisha kwenda mashariki ya mbali kuwanufaisha wengine.
Yeye alisema zipo wilaya za Tanzania bara kwenye skuli zake tena za sekondari zinauhaba mkubwa wa waalimu au kama ni hospitali kuna upungufu wa madaktari wakati waliokuwepo wanatoa huduma kwa wengine.
Alionesha uchungu na kusema kuwa ndani ya Ibara ya 52 ya katiba inayopendekezwa, elimu kwa kila mtanzania ni haki yake, ingawa anawashangaa wengine haki hiyo kuipeleka nchi jirani.
KIJAMII
Aliesema amekuwa akipata ushawishi sana kutoka kwa vijana hasa waliosoma pamoja kwamba, atafute nchi akasake maisha, ingawa dhamira yake ni kuoja jamii ya Tanzania inaendelea kupata mafanikio kupitia mawazo yake na ni sehemu ya kulipia fadhila kwa Taifa lake.
“Hebu fikiria kama akina Mwalimu Nyerere na Mzee Karume wangekimbia nchi kwa visingizio vya kutafuta maisha binafsi, ile dhamira yao ya dhati ya kuikomboa nchi yetu je ingefanikiwa? jibu ni hapana!” alisema Masoud.
Hafurahishwi hata kidogo kuona jamii inakosa wasaidizi wakati wazazi na Serikali wameshatumia unyonge wa fedha zao kumsomesha kijana kisha kusahau aliokotoka.
“Mimi ninahamu kama nikifanikiwa kiuwezo, basi nitembelee vijiji vyenye shida sana niwatatulie ili nijiwekee historia na huku ndio kutekeleza hutuba na maagizo ya wasisi wa taifa hili’’,alifafanua.
Kijana Masoud amewataka vijana wenzake kuendelea kufikiria njia sahihi ya kuliinua taifa hili na badala ya kupanga mipango na mikakati ya kwenda kutafuta maisha nchi nyingine kwani kufanya hivyo ni kielelezo cha kukosa uzalendo.
Hata hivyo amewataka vijana wasiogope kuijingiza kwenye masuala ya uongozi, akiamini kwamba huko ni sehemu mojawapo wanakoweza kutoa wigo mpana juu ya kulitendea mema taifa lao.
HALI YA NDOA
Katika kuhakikisha Massoud kwa nia yake ya kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema alijipoza kwa mpendwa wake anaetokea Mkoa wa Mara na kukubali kufunga ndoa nae, na tayari ameshapata matunda kwa kuwa na mtoto mmoja.
Massuod yeye ni kijana wa kwanza kuona mwanga kwenye familia ya watoto kumi na moja ya bawana Ali Mohamed Ali na bibi Maryam Massoud Nassor ambao wote bado wako hai wakiendelea kufaida matunda ya mtoto wao.
URAFIKI
Kijana huyo, amekiri kwamba hakuna hata mtanzania mmoja anaemkaribia kwa kuwa na idadi kubwa ya marafiki weme, ambapo hata Maulid Shibu Said rafiki yake wa karibu anao wengi wanaofanana.
UONGOZI.
Rais Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe: dk Ali Mohamed Shein, alimteua kuwa Afisa Mdhamini Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora Pemba, na sasa anaiongoza wizara hiyo.

Kubwa kwenye mikakati yake, ni kuona kila mmoja anafanya wajibu wake, nay eye kusimamia haki zake bila ya ubaguzi wala kupendelea akiamini kuwa, kufanya hivyo ni kutekeleza sheria za kazi kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.