Na Mwandishi wetu
MAMA wajawazito,
watoto wachanga na wanaozaliwa wakiwa na uzito wa chini (njiti) katika
hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, sasa hawatakuwa na tatizo la upungufu wa hewa ya
oxygen, baada ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kutoa shehena kubwa ya hewa
hiyo.
Benki hiyo imetoa
mitungi mikubwa 150 yenye gesi hiyo, ambayo mbali ya kusaidia makundi hayo pia
itatumika katika vyumba vya upasuaji na kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalum (ICU).
Kabla ya kukabidhiwa
msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wizara ya afya, Dk. Jamala Adam Taib, alisema
hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa hewa ya oxygen na ilikuwa ikihitaji
kama mitungi 300 ili kufanikisha utoaji huduma.
Alisema kwa
kawaida gesi hiyo inaagizwa kutoka Dar es Salaaam, hata hivyo inachukua muda
kuwasili kutokana na uhaba wa mitungi lakini pia tatizo la usafirishaji kwa
kuwa inasafirishwa kwa majahazi.
Hata hivyo,
alisema mpango wa baadae wa serikali ni kuzalisha kuzalisha gesi hiyo nchini.
Akikabidhi msaada
huo kwa Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo, Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Juma
Ameir, alisema msaada huo unalenga kuokoa maisha Wazanzibari.
Alisema PBZ ni
benki ya wananchi, hivyo itatumia kila faida inayopata kusaidia miradi na
huduma mbali mbali za wananchi ikiwemo huduma za afya.
Nae Waziri
Mahmoud, alisema gesi hiyo itaelekezwa katika wodi ya wazazi, watoto na katika
maeneo mengine muhimu ikiwemo vyumba vya upasuaji.
Aliipongeza PBZ
kwa kuguswa na maisha ya wananchi hasa akina mama na kuzitolea wito taasisi
nyengine za fedha kuiga mfano wa benki hiyo.
No comments:
Post a Comment