Habari za Punde

Watendaji Wizara ya Fedha watakiwa kubadilika

Na Skina Salum, WFM

WATENDAJI wa kitengo cha pencheni katika wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar wametakiwa kubadilika na kuweka mfumo mzuri wa kutunza kumbu kumbu za wastaafu ili kuepuka kuwapotezea haki zao.

Wito huo umetolewa leo na waziri wa fedha na mipago Dkt. Khalid Salum Mohamed alipofanya ziara ya kutembelea kitengo hicho ili kujionea namna wanavyofanya kazi.

Alisema kutokana na kitengo hicho kuhusika na haki na stahiki za watu waliomaliza utumishi wao kwa taifa hivyo suala la utunzaji wa kumbu kumbu zao ni muhimu.

Alisema endapo watendaji hao hawatochukua hatua hizo, malalamiko ya kuchelewa kwa malipo ya kiinua mgongo na pencheni yanayotolewa na baadhi ya wastaafu hayatakwisha jambo ambalo linaharibu nia njema ya serikali ya kulipa madeni ya wastaafu wote kwa wakati.

“Tumejipanga kupunguza muda wa kufanya malipo kwa wastaafu wetu na hili litawezekana iwapo mtakuwa na namna bora ya kuweka kumbu kumbu zao ili muda wasikae muda mrefu kusubiri malipo yao mara baada ya kustaafu”, alisema waziri Khalid.

Aidha aliwataka watendaji hao kubadilika kiutendaji na kuacha kufanya kazi kwa mazowea ili kuondoa mitazamo mibaya ya jamii juu ya kitengo hicho na serikali kwa ujumla.

Akizungumzia malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wastaafu kupokea malipo kidogo kulinganisha na hali ya maisha, Dkt. Khalid alisema serikali inalifanyia kazi jambo hilo kwa kuzingatia sheria inayosimamia utumishi serikalini na malipo baada ya kustaafu.

Aidha aliahidi kuzifanyia kazi changamoto alizozibaini na zilizoainishwa na watendaji wa kitengo hicho na kuwataka wakuu wa idara hiyo kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao ofisi kwake kila mwezi ili kupima ufanisi wa kazi zao jambo ambalo alilisisitiza katika vitengo vingine alivyovitembelea kabla.

“Kuna baadhi ya changamoto zinahitaji muda mrefu kutatuliwa, lakini kwa zile ambazo zinahitaji nguvu ndogo ni lazima tuzitatue kwa haraka ikiwemo hii ya kupata vitendea kazi vya kutunzia kumbu kumbu kwa njia ya kielektroniki”, alieleza Dkt. Khalid.

Awali akitembelea sehemu mbali mbali za kitengo hicho waziri huyo alishuhudia msongamano wa wastaafu unaosababishwa na ufinyu wa eneo jambo ambalo alisema linaleta usumbufu kwa watu wanaofika kupata huduma.

Nae mkuu wa kitengo hicho Abdulwahab Abdallah Mohamed alimueleza waziri Khalid kuwa wameanzisha mfumo wa kuhifadhi kumbu kumbu za wateja wao katika mfumo wa kompyuta ili kusaidia uhifadhi wake na urahisi wa kutoa huduma.

Alisema mpango huo ulioonesha mafanikio utasaidia kupunguza muda na kuwatambua kwa haraka watu wanaostahiki kupokea pencheni zao kuliko ilivyo sasa.

“Ili kukamilisha malipo inatulazimu tujiridhishe kupitia kila kumbu kumbu zinazomhusu mstaafu hali inayopelekea kutumia muda mwingi lakini tutakapokuwa tunatumia mfumo wa kielektroniki tutaweza kuwahudumia kwa haraka kwa kuwa taarifa zao zote zitakuwa katika mfumo mmoja”, alisema afisa huyo.

Aliongeza kuwa kitengo chake kinatoa huduma kwa zaidi ya wastaafu 5,000 kila mwezi kati ya wastaafu 11,000 wanaopata pencheni nchi nzima baada ya kumaliza utumishi wao katika taasisi mbali mbali za serikali na mashirika ya umma.

Sambamba na hilo Abdulwahab alieleza kuwa ili kurahishisha malipo kwa wastaafu na warithi wa marehemu, wameamua kuwagawa katika maeneo mbali mbali kulingana na wizara na taasisi walizokuwa wakifanyia kazi hatua ambayo imeonesha ufanisi.

Katika ziara hiyo ambayo ni mwendelezo wa ziara za waziri Khalid katika idara na vitengo vilivyomo ndani ya wizara yake, aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Ali Khamis Juma na Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Mwanahija Almas Ali ambapo aliendelea kusisitiza juu ya suala la uadilifu, uaminifu na uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa taasisi zilizomo ndani ya wizara yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.