Habari za Punde

Kongamano la Vijana Zanzibar.

Na.Mwashungi.Tahir,/Rahma.Khamis.Maelezo-Zanzibar.             
Vijana nchini wametakiwa kuongeza bidii ya kujituma na kujiajiri wenyewe ili kujiletea maendeleo endelevu.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana Kazi,uwezeshaji Wazee,Vijana wanawake na Watoto Maua Makame Rajab wakati akifungua Kongamano la vijana ikiwa ni shamra shamra ya Siku ya Vijana duniani huko katika Ukumbi wa Hailesalas miji Zanzibar.

Amesema kujiajiri ni njia nzuri ya kupambana na umaskini katika jamii na kuepukana na tabia ya kutegemea Serikali pekee kuwaajiri Vijana hao.

Maua amefafanua kwamba ili Vijana waweze kujiajiri kwa wepesi ni vyema Vijana hao wakashirikiana na wenzao kujiunga katika vikundi vya ushirika.
Kwa kufanya hivyo kutawasaidia Vijana hao kujikwamua katika dimbwi la umaskini na kuepukana na vitendo viovu ambavyo vijana wengi siku hizi hujiingiza katika makundi maovu ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya na udhalilishaji wa kijinsia.
Aidha Naibu huyo amewatia moyo Vijana hao na kuwaambia kuwa hakuna lisilowezekana pale watakapojipanga kupambana na changamoto za uhaba wa ajira kwa ktumia fursa zilizotolewa na Serikali ikiwemo mikopo ya kujiwezesha kimaisha.
Akitoa mada katika Kongamano hilo Naibu Waziri wa kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar,Lulu Msham amesisitiza Vijana hao kukubali kijiunga katika ushirika na kujiendeleza katika vikundi ili kuepukana na tabia ya ombaomba.
 “Vijana   tujitambua na tujuwe wajibu wetu kwa kujijengea maadili mema katika jamii na tujiepushe na kujiingiza  katika vitendo vya uvunjifu wa Amani kwani tukifanya hivyo tutajiondeshea uaminifu Nchini,”alisema naibu waziri .
Aidha ametoa wito kwa vijana kuzichangamkia fursa za kugombea nafasi za uongozi na kujitokeza kwa wingi hasa wanawake ambao bado wapo nyuma kiuongozi.
Akifunga Kongamano hilo la siku moja Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Kitwana Mustafa amewataka vijana kutafuta elimu na kuwa na maadili mema na kuweka ushirikiano katika kazi zao za kila siku.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana kimataifa yanatarajiwa kufanyika kesho katika Uwanja wa Mnara wa Kisonge ambapo kauli ya mwaka huu  kuelekea 2030.

Tokomeza Umaskini kwa Uzalishaji Endelevu na Matumizi yenye Tija.
                                                   

IMETOLEW NA IDARA YA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.